Moshi. Mgombea mwenza wa nafasi ya Urais kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Shoka Khamis Juma amesema endapo chama hicho kitaaminiwa na Watanzania kuunda serikali ijayo, kitafuta madeni yote ya mikopo ya wanafunzi waliokopeshwa kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Jumapili Oktoba 12, 2025, kwenye viwanja vya Manyema, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Shoka amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha maisha ya wahitimu na kuwawezesha kufanya kazi zao kwa uhuru.
“Sera yetu inatamka wazi kuwa elimu itakuwa bure kuanzia shule ya awali hadi vyuo vya elimu ya juu, vikiwemo vyuo vikuu. Hivyo wale wanaodaiwa kupitia HESLB watanufaika na sera hii, hata kama walihitimu kabla ya serikali ya ADC kuingia madarakani,” amesema Shoka.
Ameongeza kuwa Tanzania imejaliwa rasilimali nyingi zinazoweza kutumika kugharamia elimu bila kuwabebesha mzigo wa madeni wanafunzi.
“Hakuna haja ya kuwakopesha watoto wetu elimu. Tuwaache wasome bure, wafanye kazi kwa uhuru na kujenga maisha yao bila wasiwasi wa madeni,” amesisitiza.
Aidha, Shoka amesema sekta ya uvuvi ni miongoni mwa vipaumbele vya serikali yao, akisema wataanzisha uvuvi wa kisasa utakaosaidia kuzalisha samaki kwa wingi bila kuongeza maeneo mapya ya kufugia.
“Tutatumia teknolojia za kisasa kuzalisha samaki wengi zaidi kwenye mabwawa na maziwa tuliyonayo. Hii itaongeza ajira na kipato kwa wavuvi na wafanyabiashara wa samaki,” amesema.
Pia, mgombea huyo mwenza amesema ADC italiimarisha Jeshi la Polisi kwa kuongeza mishahara na marupurupu ili kuongeza morali na ufanisi katika kulinda usalama wa wananchi.
“Polisi wanapaswa kuwa na motisha. Tukiwaongezea maslahi, watatekeleza majukumu yao kwa uadilifu zaidi na kupunguza uhalifu,” amesema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ADC Taifa (Bara), Hassan Mvungi amewataka Watanzania kupuuza taarifa potofu zinazoenezwa kwamba uchaguzi mkuu hautafanyika.
“Hakuna aliyechaguliwa hadi sasa; kampeni zinaendelea kwa vyama vyote. Hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka,” amesema.
Mgombea Ubunge wa Moshi Mjini kupitia chama cha ADC, Hemed Mchomvu ameahidi kuboresha soko la Manyema lililopo Kata ya Bondeni ili kuwa mazingira bora kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa ufanisi.