Mradi wa maji wa Sh4.5 bilioni wazinduliwa, wananchi 44,939 kunufaika 

Mbeya. Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ussi amepongeza na kueleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Tukuyu, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya unaozalisha lita milioni 1.5 za maji kwa siku.

Mradi huo wenye thamani ya Sh4.5 bilioni, unatekelezwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Maji Safi naUsafi wa Mazingira Tukuyu (Tuwsa).

Akitoa taarifa ya mradi huo leo Jumapili Oktoba 12, 2025, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Maji na Usambazaji, Mhandisi Barnabas Konga amesema utekelezaji ulianza Agosti 2021 na unatarajiwa kukamilika Julai 2025, chini ya mkandarasi Make Engineering and Water Work Co. Ltd.

Amefafanua kuwa makadirio ya awali yalikuwa Sh4.5 bilioni, lakini gharama halisi imefikia zaidi ya Sh3.9 bilioni, huku kiasi cha fedha kilichopokelewa kikiwa zaidi ya Sh3.6 bilioni.
Konga amesema mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikishwaji wa wananchi na viongozi wa Serikali kwa karibu, kupitia mikutano ya hadhara na ziara za kujionea maendeleo ya ujenzi, hatua iliyowezesha upatikanaji wa maeneo ya miundombinu kwa urahisi.

Mhandisi Konga amesema mradi huo umeongeza uwezo wa huduma ya maji kutoka wastani wa lita milioni nane kwa siku, huku muda wa upatikanaji wa maji ukiongezeka kutoka saa sita hadi kufikia saa 23 kwa siku.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ussi, ameipongeza Mamlaka ya Maji Mbeya kwa utekelezaji bora wa mradi huo, huku akitoa maelekezo ya kuhakikisha taa zinawekwa katika eneo la mradi ili kuhakikisha usalama na mwanga wakati wote.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Uhuru kitaifa ,Ismail Ussi akizungumza na wananchi  Wilaya  ya Rungwe  Mkoa wa Mbeya (hawapo pichani) baada  ya kuzindua  mradi  wa maji wa Mji wa Tukuyu  wenye uwezo wa kuzalisha  lita 1.5 milioni.Picha na Hawa Mathias

Ussi amesema Serikali imefanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini na kuwataka wananchi kuithamini na kuilinda, badala ya kusikiliza maneno ya upotoshaji kutoka kwa watu wanaodai hakuna kilichofanywa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Ameeleza kuwa miradi ya maji ni miongoni mwa inayofanya vizuri zaidi nchini, hasa katika Mkoa wa Mbeya kwa kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.

“Ikumbukwe Samia Suluhu Hassan alipoteuliwa kuwa Rais, moja ya mambo aliyoyapa kipaumbele ni kufanya utafiti wa kina na kuondoa changamoto za upatikanaji wa maji nchini, jambo ambalo ametekeleza kwa vitendo,” amesema Ussi.

Kiongozi  wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa2025 , Ismail Ussi  akitete jambo na walimbiza mwenge mara baada ya kukagua  nyaraka kwenye uzinduzi  wa mradi  wa maji  wa Mji wa Tukuyu  Wilaya ya Rungwe wenye uwezo wa kuzalisha  lita za ujazo 1.5 milioni kwa siku.Picha na Hawa Mathias.

Ameongeza kuwa uamuzi wa Rais Samia kuunda Wizara ya Maji mahsusi kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kutatua changamoto za maji safi na salama, umechangia mafanikio makubwa katika sekta hiyo.

Mkazi wa Mabonde, Subira Mwakiposa amepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha miundombinu ya maji, akisema imefanikiwa kwa asilimia 100.
Amesema wanawake wanapaswa kumuunga mkono Rais Samia kwa vitendo, ikiwemo kumpa kura za kishindo ifikapo Oktoba 29, 2025, kutokana na mchango wake mkubwa katika kuboresha maisha ya Watanzania.