Mwalwisi ashusha presha Mbeya Kwanza

BAADA ya Mbeya Kwanza kuanza msimu wa 2025-2026 kwa kuchapwa mabao 4-0, dhidi ya Mbuni, kocha mkuu wa kikosi hicho, Maka Mwalwisi amesema licha ya kichapo hicho kikubwa ila bado wana nafasi ya kurekebisha kasoro mbalimbali zilizojitokeza.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo amesema siyo muda wa kufikiria tena kilichotokea kwa sababu hakitabadilisha jambo lolote, hivyo kazi kubwa anayoifanya ni maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi ijayo ugenini tena Oktoba 17, dhidi ya TMA.

“Tulifanya makosa mengi katika eneo la kujilinda kiasi cha kuwapa wapinzani wetu nafasi ya kutuadhibu, ndiyo kwanza ligi imeanza na kama nilivyosema tangu mwanzo ushindani ni mkubwa, tunajipanga upya ili kurejesha ubora wetu,” amesema Maka.

Kocha huyo amesema kuanza mechi mbili mfululizo ugenini siyo jambo jepesi kutokana na uhitaji wa kila timu hasa inapokuwa nyumbani, ingawa baada ya kuanza vibaya wanaenda kujipanga upya, hasa katika eneo la kujilinda na lile la ushambuliaji.

Mbeya Kwanza iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship msimu wa 2021-2022, msimu wa 2024-2025, ilimaliza ikiwa nafasi ya saba na pointi 50, baada ya kikosi hicho kushinda mechi 14, kikitoka sare minane na kupoteza pia minane.