Mwili mgombea ubunge CUF kuzikwa kesho Siha

Siha. Mwili wa aliyekuwa mgombea ubunge wa Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro, Daudi Ntuyehabi (34) umeshindwa kusafirishwa kwenda kuzikwa kijijini kwao Kumlungwe, wilayani Kakonko, mkoani Kigoma, kutokana na ukosefu wa fedha katika familia hiyo.

Kutokana na hali hiyo, familia ya marehemu imeamua kumzika kesho Jumatatu Oktoba 13, 2025, nyumbani kwake Kijiji cha Kilingi, wilayani Siha, baada ya baadhi ya wadau walioahidi kusaidia gharama za usafiri kushindwa kutimiza ahadi zao, licha ya shughuli za kuaga mwili kufanyika jana Oktoba 11 nyumbani kwa marehemu.

Baada ya kushindikana kwa safari hiyo, mwili wa Ntuyehabi ulirudishwa na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Kibong’oto, Siha hali iliyosababisha taharuki kwa wakazi wa kijiji hicho.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Oktoba 12, baba wa marehemu, Wilbard Ntuyehabi amesema mtoto wake alitarajiwa kuzikwa Kigoma, lakini familia imeshindwa kutekeleza mpango huo baada ya watu waliotoa ahadi ya kusaidia usafiri kuingia mitini.

“Mazishi tunafanya kesho hapa nyumbani. Tumekosa usafiri, ahadi zimegeuka maneno matupu. Tuliahidiwa msaada lakini ‘wakubwa’ wamezima simu. Tumeamua tusipoteze muda zaidi, tutazika kesho ili tuendelee na mambo mengine,” amesema Wilbard.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kikuyuni, Ruben Mgeni amesema maandalizi yote ya mazishi yamekamilika na wanachosubiri kwa sasa ni kibali cha mazishi kutoka mamlaka husika.

“Tunasubiri kibali cha kuzika kesho. Taratibu zote zimekamilika na tumeafikiana kama jamii kufanya mazishi hapa nyumbani,” amesema Mgeni.

Ntuyehabi alifariki dunia Oktoba 7, 2025, baada ya kushambuliwa na kundi la watu takribani wanane waliomtuhumu kuhusika na tukio la kumjeruhi kijana mmoja wakati alipokwenda kusuluhisha ugomvi uliotokana na madai ya fedha katika ‘grocery’ya vinywaji baridi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononina kumsababishia kifo mgombea huyo wa CUF.