Canada. Leo tunachambua suala nyeti na tata yaani umalaya ndani ya ndoa.
Kwa tafsiri rahisi, umalaya ni tendo la mtu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na watu mbalimbali kwa wakati mmoja kinyume na matarajio ya uaminifu wa ndoa. Hili, hata hivyo, halihusishi ndoa za mitala zinazokubalika kidini au kitamaduni.
Makala haya yanalenga kuonyesha jinsi ndoa kama taasisi inayotarajiwa kuwa ya heshima na uaminifu, inavyoweza kuwa pazia linaloficha tabia ya uasherati au umalaya.
Tuchukue kisa cha X ambaye ni mama wa familia, mke wa ndoa, na mfanyabiashara. Anaonekana kuwa wa heshima mbele za watu, lakini anashiriki uhusiano wa pembeni (mchepuko).
Licha ya kuwa na mume mwenye kipato, bado X anatumia fedha zake kumtunza mpenzi wake wa siri. Kuna hisia kuwa X alishawahi kupata ujauzito kupitia uhusiano huo na kisha kutoa mimba. Haijulikani kama kuna watoto wengine wa nje wa ndoa.
Kwa sura ya nje, huwezi kudhani kuwa X anaishi maisha ya aina hiyo. Lakini migogoro ya mara kwa mara kwenye ndoa yake huenda ni dalili ya madhara ya anachokifanya.
Sababu za tabia hiyo haziko wazi; je, ni kisasi dhidi ya mume? Kukosa kutoshelezwa au ni hulka tu ya tamaa isiyozuilika? Hatuna majibu ya uhakika.
Ifuatayo ni hadithi ya Y, mwanamke mwingine aliyeolewa lakini mwenye tamaa ya kingono isiyo na mipaka. Yeye hajali anayeshiriki naye, alimradi haja yake imetimia.
Haoni tofauti kati ya ndugu, rafiki au mgeni; yeyote akipata nafasi, anampa. Wapo wanaodhani anafanya hivyo kwa sababu ya mkataba fulani wa kifamilia au hali ya ndoa inayomruhusu kuwa na uhuru huo. Hata hivyo, hilo ni fumbo linalosubiri jibu.
Z pia ni mke wa mtu, lakini tofauti na wengine, yeye anajiuza waziwazi, akionekana kufanya hivyo ili kuongeza kipato, au pengine kwa sababu ya tabia ya uchangudoa.
Cha kushangaza, wanawake hawa wote wana waume na wanaishi nao kama familia za kawaida. Ndiyo maana makala haya inaibua hoja nzito: Je, ndoa hizi ni kificho cha tabia zisizofaa na kwa nini wanawake hawa hufanya wanayoyafanya?
Tunaweza kutafakari mambo manne muhimu:
Mosi, wote ni wake za watu, lakini wanajihusisha na tabia zisizolingana na ndoa.
Pili, wote ni malaya kwa maana ya kimaadili, japokuwa tofauti za mazingira na sababu zinatofautiana.
Tatu, wanayoyafanya hayaendani na misingi ya ndoa ya uaminifu na heshima.
Nne, ndoa inaweza kuwa kichaka kinachoficha tabia chafu za mtu.
Maswali magumu yanaibuka:
Je, hawa wanawake walikuwa na tabia hizi kabla ya ndoa au zimejitokeza ndani ya ndoa?
Je, ni tatizo la mtu binafsi, ndoa zenyewe, au jamii kwa ujumla?
Je, jamii ina mchango gani katika kuzalisha mazingira ya aina hii?
Makala haya haimaanishi kuwa wanaume hawafanyi umalaya. Tofauti ni kuwa katika mfumo dume wa kijamii, wanaume wengi huonekana kama “wenye haki” ya kufanya hivyo, hali inayowafanya madhara yao kuonekana madogo.
Lakini ukweli ni kuwa umalaya ni tatizo lisilo na jinsi linapofanywa na yeyote, lina madhara makubwa kwa ndoa, watoto, na jamii kwa ujumla.
Somo kuu hapa ni kwamba ndoa, licha ya kuwa taasisi ya heshima, inaweza pia kuwa pazia linaloficha maovu ya ndani.
Hili halimaanishi ndoa zote zina tatizo hili, lakini ni ukweli usiopingika kuwa baadhi zinaoana tu kwa jina huku undani wake ukiwa ni mseto wa usaliti, uongo na uasherati.
Tunatoa rai wanaofanya haya waache mara moja, kwa sababu si tu wanaathiri maisha yao, bali pia familia na jamii nzima.
Jamii isinyamaze inapogundua vitendo hivi, ingawa ni vya faragha, madhara yake ni ya kijamii.
Na kwa yeyote anayejua kuwa hana uwezo wa kudhibiti tamaa zake, je, ndoa ni sahihi kwake?
Kumbuka kuwa binadamu hatosheki kwa kupokea kila kitu, bali kwa kuridhika na kile alichonacho. Kama huwezi kuridhika, ndoa si suluhisho bali ni mzigo kwa mwingine.