NI JKT Queens inabeba taji la Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuifunga Simba Queens mabao 2-1, kwenye Uwanja wa KMC.
Bao la Winfrida Gerald dakika ya 12 na lile la Simba walilojifunga la winga Asha Omary dakika ya 17 liliipa timu hiyo taji la pili la mashindano hayo na lile la kufutia machozi la Wanamsimbazi likifungwa na Zawadi Usanase.
Kwa ubingwa huo unaifanya JKT kuwa timu ya kwanza kunyakua taji hilo mara nyingi ikichukua mara mbili mfululizo mwaka jana na huu.
Tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2023 na Simba iliibuka mabingwa wa kwanza ikiwatoa wanajeshi hao kwa mikwaju ya penati 5-4 baada ya sare ya 1-1, JKT inakuwa timu pekee iliyocheza fainali zote tatu
Winga wa JKT Winifrida amekuwa msumari wa moto kwa vigogo Simba Queens na Yanga Princess akiwafunga wote wawili kuanzia nusu fainali na leo fainali.
Katika mechi hiyo Winifrida alionyesha kiwango bora akiwapita mabeki wa Simba na kumchezea faulo nyingi ambazo zilikuwa na faida kwa Wanajeshi hao.

JKT ilionekana kucheza kwa kuelewana hasa eneo la kiungo wakianza kutengeneza mashambulizi kutokea chini hadi kwa mawinga wake.
Hata hivyo Simba ambayo takribani wachezaji watano kati ya 11 walioanza walikuwa wapya hivyo hakukuwa na muunganiko wa timu kama timu.
Katika mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu, Yanga Princess iliichapa Mashujaa Queens mabao 3-0 kwenye uwanja huo huo, mchezo ulioanza saa 7:00 mchana.
Yanga chini ya Kocha Edna Lema ‘Mourinho’ ilicheza mechi hiyo baada ya kutolewa hatua ya nusu fainali na JKT Queens kwa penalti 6-5 baada ya sare ya 1-1.
Timu hiyo ilionyesha kiwango bora tangu dakika za mwanzo, ikimiliki mpira na kushambulia kwa kasi kupitia viungo wake wa pembeni.
Bao la kwanza lilifungwa dakika ya 16 na Jeanine Mukandayisenga aliyemalizia krosi ya Precious Christopher baada ya ukuta wa Mashujaa Queens kujichanganya.

Dakika ya 48 Precious aliiongezea la pili akimalizia pasi ya Mukandayisenga na dakika 18 baadaye Aregash Kalsa akaweka kambani bao la tatu kwa asisti ya Adebis Ameerat.
Katika mchezo wa jana, Edna alifanya mabadiliko kwenye maeneo matatu, eneo la golikipa akianza na Ester Emily aliyechukua nafasi ya Zubeda Mgunda aliyeanza mechi ya nusu fainali, kiungo akianza Adebis Ameerat aliyempisha Agnes Pallangyo aliyeanzia benchini.
Eneo jingine la beki wa kushoto alianza Protasia Mbunda baada ya Wincate Kaari kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi iliyotangulia na upande wa kulia alicheza Diana Mnally akichukua nafasi ya Wema Maile ambaye hakuwapo kabisa kwenye benchi.
Yanga pia ilikosa penalti kipindi cha kwanza.
Kwa matokeo hayo, timu zote nne zimemaliza michuano ya Ngao ya Jamii ya Wanawake, kwa kushika nafasi zilezile zilizoshika katika Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL) msimu uliopita.
JKT ilimaliza kinara, ikifuatiwa na Simba, Yanga ikiwa ya tatu na Mashujaa ya nne.