Zanzibar. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kufufua michezo yote visiwani humo na kuhakikisha Zanzibar inapata heshima kimataifa kupitia mafanikio ya wanamichezo wake.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Viwanja vya Kivumbi, Jimbo la Shauri Moyo, Othman alisema michezo ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan kwa vijana.
“Tutarejesha michezo yote kuanzia soka, kuogelea, mpira wa mikono, netiboli hadi riadha. Michezo si burudani pekee — ni ajira, ni afya, na ni njia ya kuitangaza nchi yetu duniani,” alisema Othman.
Aliongeza kuwa serikali ya ACT Wazalendo itatoa kipaumbele katika kuimarisha miundombinu ya michezo, ikiwemo ujenzi wa viwanja vya kisasa, kutoa mafunzo kwa makocha, na kuweka mikakati ya kuwawezesha vijana kushiriki mashindano ya kimataifa.
Othman alibainisha kuwa Zanzibar imejaa vipaji ambavyo havijapewa fursa ya kuonekana, na akasema serikali yake itahakikisha vipaji hivyo vinaibuliwa na kuendelezwa.
“Kila kijana mwenye kipaji atapata nafasi. Tunataka kuona Zanzibar iking’ara kwenye michuano ya kimataifa kupitia wachezaji wetu,” alisisitiza.
Mkutano huo ulihudhuriwa na mamia ya wafuasi wa ACT Wazalendo waliomshangilia mgombea huyo huku wakiahidi kumuunga mkono katika uchaguzi ujao.