Sababu Kanisa Katoliki Kenya kubadilisha divai

Nairobi. Kanisa Katoliki nchini Kenya limebadilisha aina ya divai iliyokuwa ikitumika katika Misa Takatifu baada ya kubainika kuwa divai hiyo imekuwa ikipatikana kwa wingi kwenye maeneo ya burudani ikiwemo baa, hoteli na maduka makubwa.

Hatua hiyo imetangazwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB) likieleza kuwa divai mpya Mass Wine itatumika pekee katika ibada na haitauzwa katika maeneo ya biashara.

Kwa mujibu wa taarifa ya KCCB, divai hiyo mpya imetengenezwa maalumu kwa ajili ya matumizi ya kidini na ina lebo rasmi ya Baraza hilo, kama ishara ya uthibitisho wa ubora na matumizi sahihi ya kidini pekee.

Askofu wa Jimbo Kuu la Nyeri, Anthony Muheria, amesema kanisa lililazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kugundua baadhi ya waumini na watu wasio wa Kanisa kutumia divai hiyo kama kinywaji cha kawaida cha burudani.

“Ni jambo la kusikitisha kuona divai takatifu inayotumika kwenye misa ikitumiwa kwenye maeneo ya pombe. Hii ni kinyume na heshima ya sakramenti,” amesema Askofu Muheria.

Kwa sasa, divai mpya itasambazwa kupitia parokia na majimbo pekee, na haitawekwa sokoni wala kuuzwa katika maduka au hoteli.

Hatua hiyo inalenga kulinda utakatifu wa sakramenti ya ekaristi na kudhibiti matumizi yasiyofaa ya divai hiyo, ambayo awali ilipendwa na watu wengi kutokana na ladha yake.

Endelea kufuatilia Mwananchi