Bukombe. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kuendelea kuboresha na kuinua sekta ya maziwa wilayani Bukombe Mkoa wa Geita ili kuinyanyua biashara ya maziwa na kuinua uchumi wa wafugaji.
Kimeahidi kujenga na viwanda vitakavyochakata maziwa hayo ili kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji nchini wakiwamo wadogo.
Ahadi hizo zimetolewa leo Jumapili Oktoba 12,2025 na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, akinadi sera za chama hicho kwa wananchi wa wilayani Bukombe Mkoa wa Geita.

Samia amesema iwapo atachaguliwa kuendelea kipindi cha pili, Serikali yake itawekeza na kuinua sekta ya maziwa ili kukuza uchumi wa wafugaji.
Amesema Serikali yake kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo imejipanga kuongeza nguvu kwenye sekta ya mifugo kwa ujumla kwa kutoa ruzuku ya chanjo, kujenga majosho, kukarabati minada na kujenga minada mipya pamoja na machinjio.
“Tumeamua sasa tuingie kwenye ng’ombe wa maziwa tuinyanyue sekta ya biashara ya maziwa ambapo Bukombe ni wazalishaji wa maziwa wazuri aana tunakwenda kunyanyua sekta ya maziwa lakini pia kuweka viwanda vitakavyochakata maziwa ili wafugaji wauze bidhaa, fedha iingie mfukoni maisha yaendelee,”

Kuhusu madini amesema kipindi cha nyuma baadhi ya vijana walikuwa wakienda eneo la Pori la Kigosi na kuiba madini ila kwa kutambua utu wa vijana alimtaka Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko na viongozi wengine serikalini kukaa na kuangalia jinsi watakavyofanya ili vijana hao wa Bukombe waweze kunufaika na rasilimali hiyo.
“Unapokuwa na mtoto ambaye ana tabia mbaya kidogo mama anapopika na kufunika nyama jikoni mtoto anakwenda kudokoa dokoa ile nyama na kula, sasa wazazi wengine atamchapa yule mtoto mpaka aseme hapa nimezaliwa,”amesema na kuongeza.
“Lakini wazazi wengine nikiwemo mimi kama mtoto ana tabia hiyo kwenye zizi kuna ng’ombe, kuna mbuzi, kuna kondoo nitachinja wanyama nipike ndani watoto wale mpaka wakinai nitawalea namna hiyo.”

“Na ndivyo nilivyofanya kwa upande wa madini, vijana wangu wa Bukombe hawa walikuwa wanakwenda kuniibia madini kule Kigosi lakini rasilimali ile Mungu ameishusha hapa Bukombe, sasa kuliko wakaibe wakamatwe wapigwe na askari wa hifadhi wapelekwe mahakamani nikasema hapana,” amesema Samia.
Amesema kwa sasa vijana hao wanachimba kwa mujibu wa sheria, wanauza na masoko yamejengwa na kuwa huo ndiyo kujenga utu wa Mtanzania, utu wa vijana na ndiyo maana waliamua kuwawezesha ili waendelee na maisha yao.
Kuhusu wakulima Bukombe, mgombea huyo amesema Serikali itaendelea kuwapa ruzuku ya mbolea, dawa zingine za kilimo na kuwajengea skimu za umwagiliaji maji ili wakulima waweze kulima na kuzalisha kwa wingi na kuweza kuendesha maisha yao.
“Maisha ya mwanadamu yanahitaji afya nzuri, elimu nzuri, maji na umeme na tumefanya kazi nzuri miaka mitano iliyopita kuleta huduma hizo,”amesema.
Awali Dk Biteko amemnadi Samia akimsifu kama kiongozi anayejali utu na kazi kama msingi wa maendeleo na kuwa amefanya kazi kubwa nchini ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa sekta mbalimbali, kuimarisha uchumi huku akielezea hata suala la katiba mpya limejumuishwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2025/30.