Arusha. Aliyekuwa Mbunge wa Simanjiro kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, amewataka Watanzania kuwapuuza watu wanaoeneza propaganda dhidi ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, akidai kuwa wengi wao ni wafanyabiashara waliokosa zabuni za Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili, Oktoba 12, 2025 jijini Arusha, Sendeka amesema baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakipata zabuni za kuendesha miradi ya Serikali kwa muda mrefu, hivi karibuni wamezikosa kulingana na sheria za manunuzi wamekuwa wakifadhili makundi ya vijana, vyombo vya habari visivyojiheshimu na wanaharakati wa nje ya nchi ili kuharibu taswira ya Serikali na ya chama tawala.
Amesema tabia hiyo imekuwa ikienezwa pia na baadhi ya wanachama wa CCM waliokosa uteuzi wa kugombea nafasi mbalimbali, ambao sasa wamegeuka kuendesha kampeni za kuwachafua walioteuliwa kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya habari.
Sendeka ameongeza kuwa baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu wamekuwa wakitumiwa na makundi hayo kuvuja nyaraka za Serikali kwa lengo la kuonesha picha potofu ya ufisadi. “Watu wamekosa uzalendo. Wanachukua nyaraka za Serikali na kuziwasilisha vibaya ili kuchafua Serikali na viongozi wake,” amesema.
Akizungumzia hoja ya baadhi ya vyama vya siasa vinavyotaka uchaguzi mkuu uahirishwe kwa madai ya No reform, No election, Sendeka amesema: “Kwa hiyo tuahirishe uchaguzi kwa sababu chama kimoja kimeshindwa kujipanga? Hiyo si hoja. Wangoje miaka mitano ijayo, nafasi ipo.”
“Watu wanasema Rais Samia anagombea na nani hawajui anayegombea naye, wote walipeleka majina yameteuliwa na tume na ndiyo anaogombea nao. Mwaka 2020 mgombea urais wa CCM aligombea na nani si aligombea na wapinzani na aliwapiga vizuri tu.”
“Nasema mimi ni kiongozi ninatembea huko mikoani nakuambia mama Samia atashinda na atapata kura za heshima ambazo zitapeleka ujumbe kwa wale wanapojaribu kutuchafua.