TUJITOKEZE KUPIGA KURA, TUACHE PROPAGANDA ZISIZO NA MAANA

Na Emmanuel Mbatilo, Michuzi Tv- 0673956262

TUKIWA katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, kumekuwa na hali tofauti kutokana na kuibuka kwa makundi madogo ya watu ambao kwa kawaida hutumia nafasi za kisiasa kuchochea machafuko na kutisha amani ya nchi yetu.

Tanzania, nchi huru na yenye haki kwa raia wake, haiwezi kuruhusu hali kama hiyo kuathiri mshikamano na utulivu tuliozoea.

Watanzania, kama tulivyozoea kuishi kwa amani na mshikamano, tunatakiwa kuendelea na utulivu huu na kupuuza maneno yenye viashiria vya uvunjifu wa amani.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kushirikiana katika kudumisha amani, bila kujali itikadi za kisiasa au kabila.

Serikali, pamoja na baadhi ya viongozi wa dini, wamekuwa wakihimiza amani na utulivu kwa kila raia.

Aidha, vyombo vya usalama vya taifa vikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), na vyombo vingine vya ulinzi viko mstari wa mbele kuhakikisha usalama wa wananchi wote, mali zao, na utulivu wa mchakato mzima wa uchaguzi.

Nimpongeze Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ambaye amekuwa mstari wa mbele kukemea viashria vyovyote vya uvunjifu wa amani kwa nchi yetu hasa pale anapotoa taarifa juu ya tukio fulani.

Uwajibikaji wa vyombo hivi ni msingi wa kuimarisha imani ya wananchi kuwa taifa letu litaendelea kuwa huru, salama, na lenye sheria.

Ni lazima kila Mtanzania atambue kuwa uchaguzi ni nafasi ya kidemokrasia ya kutoa maoni, si chanzo cha migogoro.

Kwa kushirikiana, tukizingatia mwongozo wa vyombo vya usalama, tunaweza kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 unakuwa wa amani, huru, na unaothibitisha mshikamano wetu wa kitaifa. Kwa kufanya hivyo, tunajenga taifa thabiti, lenye maendeleo, na linalohimiza haki na ustawi wa kila raia.

USHIRIKI WA VYAMA VINGI KWENYE UCHAGUZI

Tanzania katika vipindi vyote vya Uchaguzi tokea tumeruhusu mfumo wa vyama vingi, vyama vimekuwa vikishiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ambao ni wa huru na haki huku wananchi wakipewa nafasi kuchagua viongozi wao ambao wanaona wanafaa.

Kipindi hiki cha uchaguzi karibu vyama vyote vimeonesha nia ya kushiriki Uchaguzi Mkuu, licha ya Chama kimoja kujiondoa kushiriki kikidai Tume ya uchaguzi iliyopo si Tume Huru kama tunavyoelezwa.

Wananchi tujitokeze kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu, tuweze kuchagua viongozi bora watakaotimiza maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla. Tuachane na propaganda za baadhi ya watu wenye nia ovu na nchi yetu.

ELIMU KWA MPIGA KURA

Elimu ya Mpiga Kura ni elimu ambayo hutolewa kwa wananchi wotekwa lengo la kuwawezesha kuelewa kuhusu Sheria, Kanuni, Taratibu za mchakato mzima wa Uchaguzi, wajibu wao na umuhimu wa kushiriki katika Uchaguzi. Vilevile ni elimu isiyokuwa na hisia, ubaguzi wala itikadi za kisiasa, kidini au kikabila.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetimiza wajibu wake kwa kukutana na makundi mbalimbali kuwapatia elimu na umuhimu wa kujitokeza kupiga kura, ambapo imewafikia makundi kama vyama vya siasa, waandishi wa habari, makundi maalumu wakiwemo walemavu na mashirika yasiyo ya kiserikali. hayo yote ni katika kuhakikisha wananchi wanajitokeza kikamilifu kupiga kura.