“UCHAGUZI NI MSINGI WA MAENDELEO, TUSIFANYE MAJARIBIO KWA MUSTAKABALI WA TAIFA”_JENISTA MHAGAMA

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Peramiho kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Jenista Mhagama, amewataka wananchi wa Kijiji cha Nakahegwa kutambua uzito wa maamuzi yao wakati wa uchaguzi kwa kuzingatia kuwa kuchagua viongozi sahihi ni msingi imara wa maendeleo endelevu.

Akihutubia wakazi wa kijiji hicho kilichopo Kata ya Mbinga-Mhalule, Mhagama amesema wananchi wanapoitumia haki yao ya kidemokrasia kwa busara, huwa wanajenga misingi bora ya maendeleo kwao na vizazi vijavyo, ameonya kuwa kufanya majaribio kwa kuchagua viongozi wasiokuwa na sera madhubuti za maendeleo ni sawa na kuichelewesha jamii kufikia mafanikio yanayostahili.

Akiwa kwenye kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuendelea kulitumikia jimbo hilo, Mhagama alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 katika eneo hilo, ikiwemo ujenzi wa zahanati kubwa katika kijiji cha Nakahegwa pamoja na nyumba ya Mganga, licha ya kuwa na idadi ndogo ya wakazi  jambo linalothibitisha dhamira ya serikali ya kuboresha huduma za afya hata katika maeneo ya vijijini.

Alibainisha kuwa katika kipindi kijacho cha Ilani ya 2025-2030, CCM imejipanga kuendeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa zahanati katika vijiji vya Matomondo na Mbinga-Mhalule, pamoja na kituo kikubwa cha afya kitakachotoa huduma za upasuaji kwa kina mama wajawazito.

Kwa upande wa miundombinu, alisema Ilani mpya itaendeleza ujenzi wa barabara ya lami, usambazaji wa umeme kwenye Kitongoji cha Misri, pamoja na ujenzi wa madarasa bila kuwatoza wananchi michango kama ilivyokuwa zamani.

Katika nyanja ya uchumi, Mhagama alisema mafanikio ya CCM yameonekana kwa kuimarika kwa hali za maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa pembejeo za kilimo kama mbolea na mbegu za ruzuku, hatua iliyochochea ongezeko la uzalishaji na kipato.

Pia alimwelezea mgombea urais wa CCM kuwa ni mtu mwenye maono, uchapakazi na moyo wa kizalendo, akisema amefanya kazi nae kwa karibu katika sekta mbalimbali na kumtaja kuwa ni kiongozi anayefaa kuaminiwa na Watanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini Thomas Masolo, aliwahimiza wananchi kuchagua wagombea wa CCM ambao alieleza kuwa ni watu safi, waadilifu na wenye uwezo wa kuwaletea maendeleo ya kweli kwa kipindi kijacho cha miaka mitano.

Ujumbe wa kampeni hiyo ulikuwa wazi, kwa wananchi kutumia busara na kumbukumbu ya utekelezaji uliopita kuhakikisha wanafanya maamuzi sahihi Oktoba 29, kwa kuchagua CCM kuendeleza maendeleo.