Ukosefu elimu ya tahadhari watajwa kuongeza athari za majanga

Dar es Salaam. Wakati kesho Oktoba 13 ni Siku ya Kupunguza Hatari ya Majanga Duniani, Tanzania inaungana na mataifa mengine kuiadhimisha huku wataalamu wakisema bado kuna hatari kubwa katika jamii kutokana na ukosefu wa maandalizi, elimu duni ya tahadhari na uharibifu wa mazingira unaochangia kuongezeka kwa maafa nchini.

Siku hiyo huadhimishwa tarehe hiyo kila mwaka kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu namna ya kujiandaa kukabiliana na majanga pamoja na kutambua hatua zilizopigwa kuyapunguza.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Tanzania imeshuhudia majanga yakitokea katika maeneo mbalimbali, yakiwamo maporomoko ya ardhi, mafuriko, moto wa msituni na ukame, yaliyosababisha vifo, uharibifu wa mali na wengine kukosa makazi.

Miongoni mwa majanga yaliyotikisa Taifa ni maporomoko ya ardhi yaliyotokea Desemba 2023 katika Wilaya ya Hanang mkoani Manyara huku zaidi ya watu 70 wakipoteza maisha, mamia wakijeruhiwa na wengine kukosa makazi baada ya nyumba zao kufunikwa na matope.

Tukio hilo lilikuwa moja ya maafa makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Aprili 14, 2024, tukio lingine la maporomoko ya udongo lilitokea Kata ya Itezi jijini Mbeya baada ya safu ya Mlima Kawetere kumeguka na kusababisha kaya 20 ikiwamo Shule ya Msingi Generation kufunikwa kwa matope.

Mwaka huohuo, katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, watu watatu walifariki dunia kutokana na maporomoko ya udongo.

Wakati hayo yakijiri, kila msimu wa mvua nchini umekuwa ukiacha maafa katika maeneo kama Jangwani, Msimbazi, Mikocheni, Morogoro, Handeni na Kilosa ambako makazi ya mabondeni na kando ya mito, yamekuwa yakijaa maji, hali inayoongeza uwezekano wa kuathiriwa na mafuriko.

Akizungumza na Mwananchi jana, Ofisa Miradi GreenFaith Africa, Baraka Machumu amesema matukio  ya mara kwa mara ya mafuriko, maporomoko ya ardhi na matetemeko ya ardhi, Tanzania bado haina mfumo madhubuti wa kutoa tahadhari mapema kabla ya majanga kutokea, jambo linalosababisha madhara kwa wananchi na mali zao.

Amesema mfumo uliopo sasa unafanya kazi zaidi baada ya majanga kutokea badala ya kabla, jambo linaloonesha udhaifu mkubwa katika maandalizi na uratibu.

“Kwa Tanzania mara nyingi sisi huchukua hatua baada ya janga kutokea. Tunachangishana, tunasaidiana, tunapeleka misaada lakini mfumo wa tahadhari kabla ya majanga bado upo nyuma,” amesema Machumu.

Amesema nchi inahitaji kuwekeza katika mifumo ya tahadhari ya mapema (early warning) na inaweza kutoa taarifa mapema kuhusu uwezekano wa kutokea kwa majanga kama mafuriko, maporomoko au ukame, badala ya kusubiri maafa yatokee.

Ofisa huyo amesema zamani wazee walikuwa na mbinu za kienyeji za kutambua dalili za majanga, kama mabadiliko ya upepo, sauti za wanyama au mienendo ya nyota, lakini maarifa hayo yameanza kupotea kutokana na kutotumika tena katika mifumo rasmi.

“Ukienda maeneo kama Manyara au Nyanda za Juu Kusini, wazee wanaweza kukwambia wakisikia ndege au upepo fulani, wanajua kuna tukio linakuja. Hiyo ni mifumo ya jadi ya onyo, sasa hivi hatuithamini wala hatuijumlishi kwenye mipango yetu ya kisasa,” amesema Machumu.

Pia, amesema licha ya uwepo wa teknolojia za kisasa kama mitambo ya hali ya hewa na rada, bado kuna pengo kubwa katika kufikisha taarifa hizo kwa wananchi wa vijijini na maeneo ya pembezoni.

Machumu ametoa wito kwa Serikali na taasisi husika kuhakikisha kuwa, mifumo ya tahadhari inaimarishwa na kuhusu jamii katika ngazi zote, badala ya kusubiri majanga yatokee.

“Tunapaswa kuwa na mfumo wa kitaifa wa tahadhari mapema unaounganisha teknolojia, elimu ya jadi na ushiriki wa wananchi. Tukisubiri hadi janga litokee, tunakuwa tunapoteza maisha na rasilimali,” amesema.

Pia, amesema jamii inapaswa kupewa elimu ya mapema juu ya ishara za hatari, ikiwamo nyufa zinazojitokeza ardhini, ongezeko la kasi la maji au mabadiliko ya hali ya hewa, kwa kuwa, mambo hayo mara nyingi huwa ni viashiria vya majanga makubwa.

Pia, ametoa mfano wa miundombinu mikubwa kama madaraja na majengo ambayo hubaki bila ukaguzi wa mara kwa mara, hali inayoweza kusababisha ajali pindi linapotokea janga kama mafuriko au mtikisiko wa ardhi.

“Kwa mfano, Kariakoo au maeneo mengine ya mijini, tungekuwa na mfumo wa ukaguzi wa kudumu wa majengo na madaraja. Tukiona dalili ya udhaifu, tungechukua hatua mapema, lakini kwa sasa hatua hizo ni kama jambo jipya,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Usimamizi wa Maafa, Suleiman Kova amesema majanga mengi yanayoendelea kujitokeza nchini yanasababisha athari kubwa kutokana na maandalizi hafifu.

Amesema endapo wananchi wakijengewa uwezo juu ya namna ya kujikinga na kujiokoa yanaweza yasiwe na athari kubwa pindi yanapojitokeza.

Kova amesema pamoja na kuwapo kwa dosari ndogondogo kwenye uokozi bado watu wengi hawana uelewa wa namna ya kujikinga pindi yanapotokea.

Naye, Mtaalamu wa Mazingira, Dk George Msuya alisema Tanzania bado haina mfumo madhubuti wa kupunguza hatari za majanga kabla hayajatokea.

Amesema kuwa, tatizo kubwa ni wananchi na hata taasisi za umma kutozingatia ramani za hatari (hazard maps) katika upangaji wa makazi na miradi ya maendeleo.

“Tunaishi kwa mazoea watu wanaendelea kujenga kwenye mabonde, kando ya mito na kwenye milima yenye mteremko mkali bila kujua madhara yake. Mara nyingi hatua huchukuliwa baada ya janga kutokea,” amesema Dk Msuya.

Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Makao Makuu, John Nyanda amesema moja ya changamoto kubwa wanazokutana nazo ni wananchi kukimbilia eneo la tukio bila kufuata utaratibu wa usalama, hali inayosababisha majeruhi na wakati mwingine vifo.

“Mara nyingi linapotokea janga lolote watu hukimbilia eneo la tukio badala ya kukimbilia usalama. Unakuta mtu anajaribu kuokoa mtu tukio linapotokea bila kuwa na taahdhari au elimu ya uokoaji linaloongeza hatari zaidi,” amesema Nyanda.

Mbali na hilo, vifaa vya uokoaji pia ni changamoto kwao kwa kuwa, vipo lakini kuna maeneo mengine havina faida hususani kwenye majanga ya maji, kuna wakati hali ya hewa hairuhusu kufika katika maeneo hayo.

Pia, amesema jeshi hilo limekuwa likifanya jitihada za kutoa elimu kupitia shule, taasisi na jamii kwa jumla, lakini changamoto kubwa ni ushirikiano mdogo kutoka kwa baadhi ya wananchi na viongozi wa mitaa.

“Tunapotoa mafunzo, tunahitaji viongozi washiriki kikamilifu. Wao ndiyo wanaweza kusaidia kufikisha elimu hii kwa jamii kwa urahisi zaidi. Wakati mwingine tukio linapotokea, wananchi wanakuwa mbali na huduma za zimamoto, hivyo ni muhimu kila eneo kuwa na mpango wa dharura,” amesema Nyanda.

Baadhi ya wananchi wamesema linapotokea tatizo wanaotangulia kufika ni viongozi kabla ya wataalamu ambao hawawezi kusaidia kwa wakati huo.

“Kutokuwepo kwa elimu na tahadhari ya moja kwa moja mfano maeneo ya maporomoko inachangia athari kubwa pia wananchi hawaoni faida hiyo kwa sababu majanga mengi yanaongozwa kisiasa na si kitaalamu,” amesema Hancy Mwakalinga, mkazi wa Mbeya.