Unaongezaje ladha kwenye uhusiano wako?

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa uhusiano wa kimapenzi, kuna msemo wa Kiingereza usemao: “It takes two to tango” ukimaanisha kuwa mafanikio ya uhusiano wowote yanahitaji juhudi kutoka kwa pande zote mbili.

Penzi halidumu kwa sababu ya mtu mmoja tu kujitahidi, bali kwa ushirikiano wa kweli kutoka kwa wapenzi wote. Kila mmoja anao wajibu wa kuhakikisha penzi linasitawi na kuwa na ladha ya kuvutia kila siku.

Mara nyingi, si mambo makubwa au matatizo makubwa yanayoua uhusiano, bali ni mambo madogo madogo ambayo hupuuziwa. Swali la msingi kwa mpenzi yeyote ni je, unaongeza au unapunguza ladha kwenye penzi lako?

Kuna njia rahisi, lakini zenye nguvu kubwa, ambazo zikitumika vyema huongeza thamani ya uhusiano na kuimarisha uhusiano wa kimapenzi.

Moja ya nguzo muhimu inayochangia ladha ya mapenzi ni mawasiliano. Mawasiliano ya kweli ni zaidi ya kuzungumza;  ni sanaa ya kuwasilisha hisia, mawazo na mitazamo kwa namna inayoonyesha heshima, upendo na kujali kwa mpenzi wako.

Mawasiliano duni husababisha migogoro, sintofahamu na hatimaye kuvunjika kwa uhusiano. Watalaam wengi wa uhusiano wanaeleza kuwa mawasiliano mabovu ni sababu kubwa ya ndoa nyingi kuvunjika au penzi kufifia.

Ili uhusiano wako upate nguvu na ladha mpya kila siku, jifunze kuwasiliana kwa upendo, kusikiliza kwa makini na kueleza unachohisi bila kumkashifu mpenzi wako.

Mbali na mawasiliano, muda wa faragha ni silaha nyingine ya kuongeza ladha katika uhusiano. Hili ni eneo linalopuuzwa na wengi kwa kisingizio cha majukumu, kazi au shughuli za kila siku.

Lakini ukweli ni kwamba, muda unaotumia pamoja na mpenzi wako kwa mazungumzo, vicheko na hata ukimya wa pamoja huimarisha uhusiano wenu kwa kiwango kikubwa.

Ni katika muda wa faragha ndipo wapenzi hufahamiana zaidi, huzungumza kuhusu hisia na matarajio yao, na kujenga urafiki wa kweli unaozidi tu mapenzi ya kawaida.

Hakikisha unatenga muda wa kipekee wa kuwa na mpenzi wako, muda ambao hauhusu kazi, watoto au majukumu mengine ya kila siku.

Katika kuongeza ladha ya mapenzi, namna unavyoshughulika na ndugu wa mpenzi wako ni jambo lisilopaswa kupuuzwa. Kuna methali ya Kiswahili isemayo: “Ukipenda boga, penda na ua lake.”

Katika muktadha wa uhusiano, methali hii inasisitiza kuwa unapompenda mpenzi wako ni lazima pia uwe na mtazamo chanya kwa watu wake wa karibu, hasa ndugu na wakwe. Heshima na upendo unayowapa ndugu wa mpenzi wako hujenga taswira chanya kwako na huongeza upendo kutoka kwa mpenzi wako. Ingawa si kila ndugu atakuwa mpole au mkarimu, mnapaswa kama wapenzi kuzungumza kwa uwazi namna bora ya kushughulika na ndugu wa aina hiyo bila kuharibu ladha ya penzi lenu.

Zawadi na vishangazo navyo vina nafasi ya kipekee katika kutia sukari kwenye penzi. Kinyume na imani potofu kwamba zawadi ni jambo la watu wenye fedha nyingi, ukweli ni kwamba zawadi huonyesha fikra na moyo wa kujali.

Usemi usemao “kutoa ni moyo si utajiri” unadhihirisha kuwa thamani ya zawadi haipimwi kwa bei bali kwa maana yake ya kihisia. Zawadi inaweza kuwa kitu kidogo tu lakini kikagusa moyo wa mpenzi wako kwa kina.

Wataalamu wa saikolojia wanasema kuwa wanawake, kwa mfano, hupokea kwa furaha kubwa zawadi ndogo ndogo, ilimradi zinatoka moyoni. Usisubiri sherehe kubwa au tukio maalumu kutoa zawadi;  unaweza kutoa ishara ya upendo hata kwa chokoleti, ua au hata ujumbe mfupi wa simu.

 Hii inaongeza mvuto na uhusiano hukua katika msingi wa kushangaza na kufurahishana.

Ladha ya mapenzi haiji yenyewe kama bahati, bali hujengwa kwa juhudi za makusudi kutoka kwa wahusika wote wawili. Ikiwa uko kwenye uhusiano, chukua hatua leo.

Jifunze kuwasiliana kwa ufasaha, tenga muda wa faragha, heshimu na thamini ndugu wa mpenzi wako, na usisahau zawadi  hata ndogo  ambazo zina nguvu ya kuamsha upendo uliolala.

Penzi bora si la kupatikana tu, bali la kujengwa kila siku. Na kwa kutumia mbinu hizi, unaweza kuongeza ladha na thamani ya uhusiano wako bila kusubiri mabadiliko kutoka kwa mpenzi wako pekee. Anza leo.