Usaliti unatosha kuvunja ndoa yako?

Mwanza. “Nilianza kuona tabia za mume wangu zinabadilika. Alianza kuchelewa kurudi nyumbani, akikataa chakula mezani kwa madai kuwa ameshiba… wakati mwingine hata hakutafuna kajiwe kamoja. Si unajua sisi wa kipato cha chini, mchele wetu ni wa bei rahisi,” anasema Ziada Juma (jina si halisi), mama wa watoto watano kutoka Buhongwa, Mwanza, akisimulia jinsi alivyodumu katika ndoa licha ya kusalitiwa.

Ziada anasema mabadiliko ya tabia ya mume wake yalimtia wasiwasi, hivyo akaanza kuchunguza. Hatimaye aligundua kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine ambaye alikuwa anaishi mtaa wa jirani.

Anaendelea kusimulia: “Alianza kuwa mkali ghafla. Ukiuliza jambo lolote, anakurukia kama moto. Nilipogundua chanzo ni mwanamke mwingine, niliumia sana. Nikamkusanyia nguo zake na kumwambia aende akaishi na huyo mwanamke. Aniache na watoto wangu.”

“Baada ya kuondoka, mwanaume huyo alikaa kwa mwanamke wake mpya kwa wiki kadhaa kisha akarudi.

“Nakumbuka nilitoka kibaruani kufulia wanafunzi wa Chuo cha St Agostino. Niliporudi saa 12 jioni nikamkuta barazani. Alinisalimia na kuulizia hali yangu na watoto. Aliniomba alale pale nyumbani kwa ajili ya kuwaona watoto wake, nikamruhusu kulala kwenye kochi,” anasema.

Kesho yake, anasema aliamka na kuacha pesa ya matumizi, jambo ambalo hakuwa akilifanya tangu ahamie kwa mpenzi wake. Jioni alirudi akiwa mchangamfu, akaleta zawadi na kuanza kuomba msamaha, akidai alipitiwa na shetani.

“Baada ya kuondoka kwake, nilimweleza mama mkwe na kaka yangu. Aliporudi, niliwashirikisha. Kaka aliniambia atanisaidia kwa uamuzi yangu, mama mkwe akaniomba nimpe nafasi ya mwisho kwa ajili ya watoto.”

Ziada anasema  alikagua simu ya mumewe na kuona ujumbe wa mwisho kutoka kwa yule mwanamke, ukiashiria kuwa walikuwa wamegombana na mumewe  na kwamba alishamwambia hataki tena uhusiano huo.

“Nikajiridhisha kuwa ameachana naye kweli, nikamsamehe. Tukaendelea na maisha ya ndoa,” anaeleza.

Rafiki yake Ziada, Mariam Abassi, anakiri kuwa alihisi wasiwasi mkubwa wakati shemeji yake alipoondoka.

“Nashukuru Mungu sikumshauri vibaya. La sivyo, ningeumbuka. Sikutarajia kama wangerudiana tena,” anasema.

Samweli Adam (si jina halisi) alikuwa mume wa familia kwa zaidi ya miaka saba. Anasema alimpenda mkewe, kwa moyo wake wote na hakuwahi kufikiria kuwa siku moja angekuwa chanzo cha maumivu makubwa maishani mwake.

Walibarikiwa na watoto wawili na maisha yao yalionekana kuwa ya kawaida kama ya wanandoa wengine, yakijawa na changamoto ndogo ndogo, lakini wakizitatua kwa mazungumzo na uvumilivu.

Hata hivyo, mambo yalianza kubadilika pale mkewe alipoanza kuwa na misimamo mikali, kupunguza mawasiliano, na kuwa na simu iliyolindwa sana na nywila.

Juma alihisi kuna jambo linaendelea, lakini alijipa moyo kwamba labda ni msongo wa kazi au changamoto nyingine za kawaida. Hakuamini kuwa mkewe angeweza kumsaliti.

Baada ya muda, alipopata ushahidi wa ujumbe wa mapenzi kati ya mkewe na mwanaume mwingine, moyo wake ulivunjika vipande. Aliamua kukabiliana naye kwa utulivu, lakini alikanusha kila kitu. Ilipobainika kuwa uhusiano huo wa ulikuwa umedumu kwa miezi kadhaa, na hata wakati mwingine mwanaume huyo alifika nyumbani kwao, Samwel alihisi heshima yake kama mume, baba na mwanaume imedhalilishwa vibaya.

Alijaribu kusamehe mara ya kwanza, lakini tabia ya mkewe haikubadilika. Aligundua kuwa upendo hauwezi kustawi penye usaliti wa mara kwa mara na ukosefu wa toba ya kweli. Hatimaye, kwa uchungu lakini kwa uamuzi wa kiutu uzima, aliamua kuvunja ndoa hiyo ili kulinda afya yake ya kiakili na heshima yake binafsi.

Wataalamu wa uhusiano wanaeleza sababu kadhaa zinazochangia usaliti katika ndoa, ikiwemo ukosefu wa mawasiliano.

Wenza wanaposhindwa kuzungumza kwa uwazi kuhusu hisia, matatizo au matarajio yao, hutengeneza umbali wa kihisia.

Sababu nyingine ni, upungufu wa mapenzi. Kukosa ukaribu wa kimwili au hisia huweza kusababisha upweke unaosukuma mtu kutafuta uhusiano wa nje.

Nyingine ni kutojisikia kuthaminiwa. Kukosa sifa, heshima au pongezi kutoka kwa mwenza kunaweza kuchochea kutafuta faraja nje.

Pia mitandao ya kijamii imekuwa kichocheo kikubwa cha usaliti wa kihisia kupitia mawasiliano ya siri.

Lakini pia wapo wanaochepuka kama njia ya kulipiza kisasi baada ya kugundua mwenza naye alisaliti, au kutokana na majeraha ya kihisia kutoka maisha ya awali.

 Usaliti unatosha kuvunja ndoa?

Mshauri wa ndoa, Dk Jacobo Mutashi, anasema:

“Usaliti peke yake hautoshi kuvunja ndoa. Kuna nafasi ya msamaha kwa aliyeomba msamaha kwa dhati. Hakuna binadamu mkamilifu. Biblia imejaa mafundisho ya kusameheana. Yesu mwenyewe alihukumu kesi ya mwanamke aliyefumaniwa na kusema asiye na dhambi awe wa kwanza kumpiga jiwe.”

‘’Yesu akasema kama kuna mmoja kati yenu hana dhambi awe wa kwanza kuokota jiwe kumpiga huyu mwanamke. Yesu akaendelea kuandika alipoinua uso wake akakuta yupo na mwanamke wale wazee wote wakakimbia. Kwahiyo hakuna kosa wala dhambi isiyo sameheka sisi binadamu hakuna mkamilifu hata mmoja.’’

Dk Mutashi anasisitiza kuwa ndoa inahitaji msamaha, uvumilivu na kuchukuliana, kwa kuwa vikwazo haviepukiki katika maisha ya pamoja.

Ustadhi Twaha Bakari, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), Mkoa wa Mwanza, anasema:

 “Katika Uislamu, talaka haiji moja kwa moja kwa sababu ya usaliti isipokuwa kama kuna ushahidi wa wazi  wa mashahidi wanne walioona tendo. Siyo tu kupokea meseji au kusikia tetesi.”

“Pale ofisini kwetu tuna ofisi maalum inayoshughulikia masuala ya ndoa na talaka. Kwahiyo ndoa nyingi zinazovunjika pale ni watu waliofumaniana.

Na sasa hivi watu wanachukulia kufumaniana mtu anaweza kukuta meseji tu siyo kufumaniana kama dini inavyotaka yaani ushuhudie kabisa lile tendo siyo umewakuta watu wawili wapo chumbani unasema nimewafumania,”anafafanua.

Naye Sheikh Hassan Kabeke, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, naye anasema:

“Uamuzi wa talaka ni wa aliyeumizwa. Anaweza kusamehe au kuachana, lakini kitendo cha kuchepuka peke yake si talaka moja kwa moja.”

Anaongeza: ‘’ Katika Uislamu ndoa haivunjwi kwa utashi wala kwa maasi. Ukifanya kosa fulani ndoa haivunjiki moja kwa moja. Mwenye haki ya kuvunja ndoa ni mwanaume. Akiona huyu amesaliti basi anampa talaka anamwacha. Lakini siyo kwamba kitendo cha kusaliti chenyewe ndicho sababu ya moja kwa moja ya kuachana.’’

Kwa upande wake, Mchungaji Godwin Mathayo wa Kanisa la EAGT anasema:

“Ndoa ni hadi kifo kiwatenganishe. Hata kama mwenza anakusaliti, ni muhimu kutafuta suluhu, kuomba msaada wa kiroho na kuliweka jambo hilo mbele za Mungu.”

“Kuna wanawake wengine hata wafumanie waume wake mara 20 bado wataendelea kwenye ndoa, watajua hapa kuna changamoto fulani waume walizipitia. Hivyo ni muhimu wanandoa kukabidhi ndoa na familia zao kwenye maombi…wamtangulize mbele Mungu,”anaeleza.

Katika nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Tanzania, sheria inatambua usaliti kama moja ya sababu zinazoweza kutumiwa na mmoja wa wanandoa kuomba talaka. Mahakama huangalia ushahidi wa usaliti na athari zake katika ndoa kabla ya kutoa uamuzi wa kuivunja.

Kwa mujibu wa kifungu cha 72 cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 (marekebisho ya 2019),  mwanandoa aliyeumizwa na usaliti anaweza kudai fidia dhidi ya mtu aliyehusika na mwenza wake.

Lengo la fidia si adhabu bali ni kifuta machozi na kulipia madhara yaliyotokea. Hata hivyo, fidia haiwezi kudaiwa kama mhusika alishakubali au kuridhia usaliti huo.

Kifungu cha 74 kinaeleza kuwa mahakama itaamua kiwango cha fidia kulingana na mazingira ya kesi husika, bila kuweka lengo la kumwadhibu mtuhumiwa, bali kutoa haki kwa aliyeumizwa.

Simulizi ya Ziada na maoni ya wataalamu yanaonyesha kuwa usaliti, japo ni jeraha kubwa katika ndoa, hauwezi kuwa sababu ya moja kwa moja ya kuivunja bila tafakari, mawasiliano na msaada wa kijamii, kidini au kisheria.

Katika ulimwengu wa sasa ambapo ndoa nyingi hukumbwa na changamoto za mawasiliano, tamaa, na shinikizo la maisha, uamuzi wa kusamehe au kuachana unahitaji busara, uvumilivu, na maarifa ya kina.

Kwa mtazamo wa kijamii na kitamaduni, katika baadhi ya jamii, usaliti huonekana kama jambo linaloweza kusamehewa na kusuluhishwa kupitia mazungumzo au ushauri wa kifamilia au wa kidini.

Katika jamii nyingine, hasa zile zinazosisitiza uaminifu na heshima ya familia, usaliti unaweza kuwa fedheha kubwa inayoweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa mara moja.