Dar es Salaam. Dira ya Taifa 2050 imeibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa elimu nchini, baada ya wadau wa maendeleo, wasomi na viongozi wa Serikali kujadili hilo katika mkutano uliofanyika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU) mjini Iringa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wadau hao wamejadili nafasi ya ubia katika utekelezaji wa dira hiyo.
Mkutano huo uliobeba ujumbe wa kutafakari ‘Nafasi ya Ubia katika Utekelezaji wa Dira 2050,’ hoja kuu iliyoibuka ni umuhimu wa mageuzi ya kina katika mfumo wa elimu ili Taifa lizalishe rasilimali watu itakayowezesha kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.
Awali, akifafanua kuhusu dira hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia wa Serikali na Sekta Binafsi (PPT), David Kafulila amesema uchumi wa Tanzania unategemea nguzo kuu nne ambazo ndizo msingi wa kufanikisha dira hiyo ya muda mrefu.
Amezitaja nguzo hizo kuwa ni jiografia ya nchi, rasilimali asilia, kilimo na mifugo na diplomasia ya kiuchumi.
Amesema Tanzania ni nchi yenye nafasi ya kipekee kijiografia kwa kuwa na bandari kubwa inayozungukwa na nchi zisizo na bandari, hali inayoiwezesha kuwa kitovu cha biashara za kikanda.
“Bandari zetu, hasa Dar es Salaam, zinachangia takribani asilimia 40 ya pato la taifa,” amesema Kafulila.
Ameongeza kuwa, sekta ya madini na utalii imeendelea kukua kwa kasi kubwa.
Mchango wa wachimbaji wadogo, kwa mujibu wa Kafulila, umeongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2021 hadi asilimia 40 mwaka 2025.
Vivyo hivyo, mapato ya sekta ya utalii yameongezeka kutoka Sh1.3 bilioni mwaka 2021 hadi Sh4 bilioni, mwaka 2025, yakizalisha zaidi ya ajira milioni 1.5.
Kwa upande wa kilimo na mifugo, Kafulila amesema Serikali imeongeza maeneo ya kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 500,000 mwaka 2021 hadi hekta 980,000 mwaka 2025, lengo likiwa kupunguza utegemezi wa mvua.
Idadi ya viwanda vya nyama imeongezeka kutoka vitatu hadi tisa, na viwanda vya kuchakata madini vimeongezeka kutoka viwili hadi tisa.
Ameeleza kuwa, diplomasia ya kiuchumi imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza pato la Taifa huku biashara za kimataifa zikipanda kutoka Dola 12 bilioni mwaka 2021 (takribani Sh31.2 trilioni) hadi Dola 32 bilioni mwaka 2024 (takribani Sh83.2 trilioni), jambo linaloonesha mafanikio ya juhudi za Serikali katika kukuza uhusiano wa kimataifa.
Akizungumzia kuhusu mwenendo wa uchumi, Kafulila amesema Tanzania inaendelea kufanya vizuri kimataifa, ripoti ya Global Credit Ranking inaonesha nchi ipo katika uwiano wa deni kwa uchumi wa asilimia 46, ikilinganishwa na baadhi ya nchi za Afrika ambazo zimefikia hadi asilimia 80.
“Hii inaonesha kuwa Tanzania ipo kwenye nafasi nzuri ya kunufaika na mikopo ya kimataifa,” amesema.
Kafulila amesema Dira ya Taifa 2050 inalenga kuijenga Tanzania yenye uchumi wa trilioni moja za dola, kiwango ambacho kwa sasa kinamilikiwa na takribani nchi 19 pekee duniani.
Amesema, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN), Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 140 ifikapo mwaka 2050, ongezeko la asilimia tatu kwa mwaka, zaidi ya wastani wa Afrika wa asilimia mbili.
Amesisitiza kuwa, ukuaji huo wa idadi ya watu unahitaji kuandaliwa kwa kuzalisha rasilimali watu wenye elimu na ujuzi sahihi, akitahadharisha kwamba bila mageuzi ya elimu, dira hiyo inaweza kubaki kwenye karatasi.
‘Mageuzi ya elimu ndiyo injini ya Dira ya Taifa 2050’
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU), Profesa Sister Christina Lekule, amesema Taifa linapaswa kujiuliza maswali matatu ya msingi, tupo wapi, tumetoka wapi na tunakwenda wapi?
Amesema kufikia Dira ya 2050 kunahitajika Taifa lenye watu wenye elimu bora, maadili na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira.
“Mfumo wetu wa elimu bado unazalisha wasomi ambao hawana maono na uhusiano wa moja kwa moja na mahitaji ya Taifa. Elimu bora ni injini ya mabadiliko; ni silaha ya kujenga uchumi imara tunaoutaka,” amesema.
Ameongeza kuwa, mageuzi ya elimu siyo hiyari bali ni sharti la kimaendeleo, akibainisha kuwa dira 2050 si ndoto, bali ni ramani ya Taifa kuelekea Tanzania yenye uchumi shindani na watu waliokomaa kielimu.
Mwenyekiti wa Daima Association, Profesa Samwel Wangwe, ambaye alishiriki katika kuandaa rasimu ya Dira ya Taifa 2050, amerejea maneno ya Mwalimu Julius Nyerere aliyewahi kusema kuwa vyuo vikuu ni mahali pa kuzalisha mawazo mapya yanayoweza kutatua changamoto za jamii.
Amesema vyuo vikuu nchini vinapaswa kuwekeza katika ubunifu na tafiti zenye tija, badala ya kurudia maudhui yasiyoendana na wakati.
“Tunahitaji elimu inayomwandaa kijana kwa soko la dunia, siyo darasani pekee,” amesema.
Akinukuu tena maneno ya Nyerere, Profesa Wangwe amesema: “Soko kubwa ni sawa na gari lenye nguvu kubwa, lakini unahitaji dereva anayejwa anataka kwenda wapi.”
Ameongeza kuwa, Dira ya 2050 itafanikiwa endapo mipango ya Taifa itaacha kuwa ya mazoea na badala yake iwe na utekelezaji wa vitendo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, ameunga mkono hoja ya mageuzi ya elimu akisema Taifa limepoteza mwelekeo katika kujenga maarifa ya vitendo na kusisitiza elimu ya ujuzi ili kuandaa rasilimali watu itakayolifikisha Taifa katika Dira yake ya maendeleo ya 2050.
“Zamani vijana waliweza kushona nguo zao au kutengeneza vitu vidogo, lakini leo hata kifungo cha shati kikikatika, kijana anakimbilia kwa fundi,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa elimu ya ujuzi badala ya nadharia pekee, akionya kuwa bila kuwekeza katika elimu ya vitendo, Taifa litakosa nguvu kazi bunifu inayohitajika katika uchumi wa kisasa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Isdori Minoni amesema dira ya Taifa haiwezi kufikiwa kama kuna makundi ya watu yataachwa nyuma.
Amehimiza jamii za vijijini zifikiwe na kupewa elimu ya dira hiyo ili ziwe sehemu ya safari ya maendeleo.
“Dira hii ni ya Taifa zima, si ya viongozi pekee hivyo tunahitaji ushirikishwaji wa watu wote wanawake, vijana, sekta binafsi na mashirika ya kiraia,” amesema.
Katika kujenga utamaduni na maadili ya kitaifa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria, Dk Nasra Habib amesisitiza umuhimu wa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia na kuwasiliana katika elimu, ili kukuza maadili na utamaduni wa Taifa.
“Kiswahili ni nguzo ya umoja wetu, ni urithi unaoweza kujenga jamii yenye kujitambua na kujitegemea,” amesema.
Akifunga kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Heri James amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha dira ya Taifa 2050 inatekelezwa kwa vitendo kupitia ubia, ubunifu na uwekezaji katika elimu na teknolojia.
“Hatufikii dira kwa maneno, bali kwa vitendo, kupitia utendaji kazi na uadilifu katika yale tuliyojipangia,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
“Mkoa wetu wa Iringa unafursa nyingi sana, watu wa Iringa ni wachapa kazi, tunayo hifadhi kubwa ya Ruaha, vipo vyuo vikuu hapa na biashara mbalimbali watu wanachapa kazi,” amesema.
Amesisitiza wadau kuweka mikakati ya pamoja kupigania maadili ya jamii ili kuwa na jamii bora itakayowezesha kufikia dira 2050.