Wanafunzi Rombo watengeneza mfumo wa upigaji kura kidijitali

Rombo. Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mashati iliyopo wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, wametengeneza mfumo wa upigaji kura kwa njia ya kidijitali unaolenga kurahisisha mchakato wa upigaji kura kwa wananchi katika kipindi cha uchaguzi.
Wanafunzi hao wa kidato cha tano na cha sita wamebuni mfumo huo kupitia maarifa wanayopata katika somo la kompyuta sayansi, kama sehemu ya kuonyesha ubunifu na uelewa wao katika matumizi ya teknolojia.

Akionyesha mfumo huo unavyofanya kazi wakati wa mahafali ya 16 ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo Oktoba 11, 2025, mwanafunzi wa kidato cha sita, Eliabu Japhet, amesema wazo hilo lilitokana na hamasa ya kutaka kuchangia katika maendeleo ya Taifa kupitia teknolojia.

“Tulitumia maarifa tuliyojifunza darasani kuunda tovuti na mfumo wa upigaji kura mtandaoni kama mfano wa jinsi teknolojia inavyoweza kurahisisha mchakato wa uchaguzi, tuliangalia kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu, tukabuni mfano wa mfumo unaoweza kutumika kupiga kura kwa njia ya kidijitali,” amesema Japhet.

Amesema kuwa, mfumo huo umeundwa kwa kufuata kanuni zinazofanana na zile za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ukiwa na sehemu za kuonyesha wagombea wa urais na kumwezesha mpiga kura kuchagua mgombea anayemtaka.
“Mfumo huu unahifadhi kura na kila mpigakura hupokea risiti ya kidijitali kama uthibitisho wa ushiriki wake, ambayo hubaki kuwa siri yake binafsi,” amesema mwanafunzi huyo.
Akizungumza baada ya kuonyeshwa ubunifu huo, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, amewapongeza wanafunzi hao kwa ubunifu na uthubutu waliouonyesha katika kutumia elimu wanayoipata shuleni hapo.
“Hongereni sana kwa ubunifu huu mkubwa, mmeonyesha mfano mzuri wa jinsi elimu ya Tehama inavyoweza kuleta suluhisho katika jamii, endeleeni kuboresha wazo hili kwani linaweza kuwapatia manufaa makubwa hapo baadaye,” amesema Profesa Silayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Emmanuel Mrosso amesema ubunifu huo ni ushahidi kuwa elimu ya Tehama shuleni hapo ina mchango mkubwa katika kutatua changamoto za kijamii kupitia suluhisho bunifu za vijana.

“Wanafunzi wetu wameonyesha kuwa elimu si nadharia tu, bali inaweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii, tunajivunia kuona vijana wetu wakiwa wabunifu na wanaotumia teknolojia kwa manufaa ya umma,” amesema Mwalimu Mrosso.