Dar es Salaam. Alikuwapo jamaa mmoja, tumuite Samsoni. Samsoni alikuwa na mwili wa miraba minne kama anaishi gym. Alikuwa na maguvu sio kawaida.
Samsoni alikuwa anaweza kuvuta mzigo wa tani moja peke yake. Samsoni alikuwa na maguvu kiasi kwamba vitani alikuwa na uwezo wa kupambana na jeshi zima la maadui na kuliangusha.
Samsoni aliogopeka na kila mtu hasa viongozi. Waliogopa kwa sababu walifikiria siku Samsoni akiamua kuzitaka nafasi zao hakutakuwa na wa kumzuia.
Basi viongozi wa juu wakaanza kupanga mipango ya kumuangusha. Wakaanza kwa kumtumia watu wengine wenye maguvu kama yeye lakini Samsoni alipambana nao na kuwashinda. Kila mpango wa kumwangusha Samsoni ulifeli na mwishowe viongozi wakakataa tamaa.
Sasa tutafanyaje? Wakawa wanajiuliza. Na ndipo alipokuja mwanamke mmoja, tumuite Delila. Delila akawaambia viongozi, nipeni mimi hiyo kazi, baada ya mwezi tu, Samsoni atakuwa historia.
Kweli, viongozi wakamkubalia lakini wakiwa na matumaini ya chini sana. Delila akaingia kazini, akaanza kwa kujenga ukaribu na Samsoni, Samsoni akaingia kwenye kumi na nane. Delila akahamia kwenye kumfanya Samsoni kuwa mpenzi, Samsoni akiwa hana hili wala lile akakubali na akawa mpenzi wa Delila.
Wakiwa kwenye penzi, Delila akaanza kumdadisi na kumpeleleza, na mbinu yake ilikuwa ni kutumia uanamke wake; urembo, sauti nzuri, kuzungumza kwa upole, kumjali Samsoni, kwa kifupi, Delila alikuwa na haiba ya kike.
Mwishowe, mwanaume wa shoka Samsoni akapagawa na upendo alionyeshwa na Delila na kujikuta anamwaga siri zake. Akamuelezea Delila kuwa siri ya yeye kuwa na manguvu kiasi kile ni kwa sababu alikuwa hanyoi nywele zake.
Basi, Delila akavizia Samsoni akiwa amelala, akamnyoa nywele zote, kisha akatoa taarifa kwa viongozi ambao walituma wanajeshi wao na wakammaliza Samsoni.
Najua umewahi kuisikia hadithi ya kufanana na hii. Lakini lengo la kuirudia leo ni kukumbusha kwamba siku ambayo wanawake watajua namna ya kutushinda ndio utakuwa mwisho wetu wa kujiona miamba.
Historia inaonyesha, wanaume wengi waliowahi kuanguka kutoka nafasi za juu walizokuwa nazo waliangushwa na mwanamke. Na sio kwa maana mbaya, bali ukweli ni kwamba wanawake wanajua jinsi ya kuwashinda wanaume kwenye mapambano.
Ubaya ni kwamba, wanawake wengi wa siku hizi hawaijui hii mbinu. Wanataka kushindana na wanaume kwa njia za kivita. Mfano, unakuta mwanamke ana mwanaume anayevaa nguo za kishamba ambazo yeye hazifurahii.
Lakini utakuta mwanamke anatumia nguvu kutaka kumbadilisha mwanaume, utasikia; “Mimi manguo yako siyapendi, manguo yako yananitia aibu, manguo ya kishamba kama mzee.” Ngumu mwanaume kubadilishwa kwa mtindo huo.
Lakini tufanye badala ya kuchapwa na maneno makali kiasi hicho, mwanamke akamnunulie nguo anazopenda aone mwanaume wake anavaa, kisha ampe kama zawadi, mwanaume atazivaa na mwishowe atakuta mwanaume amebadilika kabisa na kuwa kama anavyopenda.
Siku wanawake wa kisasa wakigundua jinsi ya kuwa kama Delila, wanaume tutaangamia vibaya sana.