Kigoma. Mgombea ubunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka wananchi wa Kigoma kuamka na kuchagua viongozi wanaotekeleza ahadi zao badala ya wale wanaotoa maneno matupu.
Akizungumza leo Jumapili, Oktoba 12, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Mwanga Community Center mjini Kigoma, Zitto amesema yeye ni miongoni mwa viongozi waliothibitisha kwa vitendo utendaji wao, akisisitiza kuwa endapo ataaminiwa tena, atamalizia miradi aliyoianzisha wakati wa kipindi chake cha awali.
“Kipindi chetu cha uongozi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma-Ujiji kati ya mwaka 2015 hadi 2020, kilikuwa cha kipekee, tuliacha alama za kudumu kwa kujenga miundombinu ya kisasa ikiwemo barabara za lami,” amesema Zitto.

Ameongeza kuwa katika kipindi hicho waliweza kupunguza makorongo kwa kujenga mifereji ya maji ya mvua, kuanzisha miradi ya masoko kama vile Soko la Jioni lililopo Mtaa wa Mzee Menge (Soko la Marungu), kuboresha Stendi mpya ya Gungu, kujenga mialo ya wavuvi katika maeneo ya Kibirizi na Katonga, pamoja na kuimarisha huduma za elimu na afya.
“Tulijenga shule mpya za msingi na sekondari, tukaanzisha shule za upili katika mji wetu, tuliboresha zahanati na vituo vya afya, tulijenga bandari mbili Ujiji na Kibirizi, na tukasababisha kuanza kwa mradi wa Bandari Kavu ya Katosho, tuliahidi na kutekeleza,” amesema Zitto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo amesema uchaguzi si jaribio bali ni fursa ya wananchi kuchagua hatma yao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Amesema Zitto ni kiongozi aliyejitoa kwa dhati kupigania maendeleo ya Kigoma, ikiwemo kusukuma mradi wa reli ya kisasa (SGR) kufika Kigoma na kuhimiza uboreshaji wa barabara kuu za mikoa.
“Ndugu zangu, Oktoba 29 ni siku muhimu ya kufanya maamuzi kwa hatma zenu na watoto wenu. Msifanye makosa kuchagua chama kingine, tuchague ACT-Wazalendo kwa maendeleo ya Kigoma Mjini,” amesema Nondo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Esther Thomas amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kumpigia kura Zitto Kabwe, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda kura ili kuhakikisha ushindi wa chama hicho unapatikana kwa kishindo.