Bado Watatu – 56 | Mwanaspoti

“KWANI wewe ulishaonana na wakili wake?”
“Nilishaonana naye mara nyingi.”
“Amekwambia nini?”
“Ameniambia ameshaieleza kila kitu mahakamani. Kwa hiyo tusubiri hukumu.”
“Ni sawa. Tusubiri hukumu. Si vizuri hukumu tutoe sisi.”
“Kama atanyongwa au atafungwa, mahakama ndiyo inajua.”
Sikumjibu kitu. Nikajifanya ninawaza.
Mwanamke huyo akanipa mkono na kuniambia, “Kwaheri. Tunaweza kuonana siku nitakaporudi.”
Baada ya kuagana na mama yake Faustin, mwanamke huyo aliondoka ofisini kwangu na kuniacha nikimfikiria Hamisa.
Nilikuwa nikifikiria kwamba siku za ndoa yetu zilikuwa zikikaribia kwa haraka.
Nilipoitafakari safari ya mapenzi yetu na Hamisa, pamoja na misukosuko tuliyokutana nayo, niliona kama safari iliyokuwa na mabonde, milima, mito na tambarare.
Baada ya misukosuko na kukata tamaa, hatimaye tulibakisha siku chache tu tufunge ndoa yetu ambayo kila mmoja wetu alikuwa akiisubiri kwa hamu.
Kwa vile kesi ya Faustin, ambayo ilikuwa ikinipotezea muda wangu mwingi, ilikuwa inamalizika, niliamini kuwa nitakuwa na pumziko la kutosha baada ya hukumu ya Faustin kutolewa.
Kulikuwa na mambo mawili ambayo nilikuwa nikiyatarajia kwa Faustin. La kwanza ni kuhukumiwa kunyongwa na la pili kupata kifungo cha maisha.
Mahakama ingeweza kumhukumu anyongwe kwa sababu aliua kwa kukusudia. Alipanga njama za mauaji na akazitekeleza. Na angeweza kufungwa kifungo cha maisha baada ya mahakama kutafakari kwamba aliowaua tayari walishahukumiwa kunyongwa.
Kosa la kujitwalia mamlaka kinyemela kinyume cha sheria linaweza kuonekana dogo lisilostahili adhabu ya kifungo cha maisha, lakini kama mahakama itaamua kutoa adhabu hiyo, itakuwa imetafakari athari iliyotokana na kosa hilo.
Siku ya hukumu ikawadia. Faustin aliletwa mahakamani. Wakati ninaingia mahakamani kusikiliza hukumu hiyo nilimuona mama yake Faustin, lakini nilimkwepa. Sikutaka kukutana naye. Lolote litakalomtokea Faustin katika hukumu yake, yule mwanamke angenilaani mimi, nilijiambia.
Angenilaani mimi kwa sababu ndiye niliyemkamata baada ya Faustin kujitokeza polisi, na mimi ndiye niliyeshughulika na uchunguzi wa kesi yake mwanzo hadi mwisho.
Isitoshe, nilipanda kizimbani na kutoa ushahidi wangu dhidi yake. Hivyo kama atahukumiwa kunyongwa, mama yake hatamlaumu mtu mwingine zaidi yangu.
Bado, hata kama atafungwa kifungo cha maisha, lawama zitakuwa upande wangu kwa sababu ndiye anayenifahamu. Hivyo siku ile ambayo ilikuwa ya hukumu sikutaka kuwa karibu naye.
Wakati Faustin anapandishwa kizimbani, nilimuona mama yake amekaa katika safu za mbele ili aweze kumuona vizuri mwanawe na pengine kuagana naye baada ya hukumu.
Mwanamke huyo alipomtazama mwanawe, ambaye siku ile alionekana amekonda na kupwaya pengine kwa sababu ya mawazo ya hukumu yake, alitoa kitambaa na kuanza kujifuta machozi.
Hakuuinua uso wake tena hadi jaji alipoanza kusoma hukumu yake.
Jaji alianza kutaja kosa lililomkabili Faustin. Alitaja kosa lile lile aliloshitakiwa – la kuua kwa kukusudia.
Akataja kipengele cha sheria ambacho Faustin alidaiwa kukikiuka kwa kutenda kosa hilo. Akataja tarehe ambazo matukio yalitokea.
Baada ya hapo akafafanua kwamba mshitakiwa alikiri mwenyewe kosa lake.
Alisema hata hivyo, mahakama ilitaka kupata ushahidi ili kujiridhisha kwamba mshitakiwa aliyekiri kosa ametenda kweli kosa hilo kwa mujibu wa sheria au la.
Jaji alitoa mfano wa kesi moja ambayo mshitakiwa alikiri kosa la kuua kwa kukusudia na kuhukumiwa kunyongwa, lakini baada ya hukumu kutolewa iligundulika kwamba mshitakiwa alikiri kwa makosa kosa hilo. Ilibainika kwamba mshitakiwa aliua kwa kujihami kwani aliyemuua alikuwa mtu aliyetaka kumdhuru.
Jaji aliendelea kueleza kuwa katika ushahidi uliotolewa aligundua kuwa mshitakiwa aliua kwa kukusudia.
Jaji alipofika hapo nikajua Faustin ananyongwa! Nilimtupia macho mama yake, nikaona alikuwa amemtolea macho jaji. Macho yake yalikuwa mekundu yaliyoonyesha wazi kuwa alikuwa akilia kimya kimya.
Jaji akaendelea kueleza kuwa kosa la kuua kwa kukusudia linatakiwa lizingatie vipengele kadhaa vya sheria.
Akataja baadhi ya vipengele hivyo kwamba: kuwepo dhamira ya mauaji kwa mshitakiwa, kuwepo kitendo kilichosababisha mauaji, na aliyeuawa awe na haki ya kuishi kwa mujibu wa sheria.
Akitoa mfano wa mtu kuwa na haki ya kuishi, jaji alisema ni mtu yeyote isipokuwa yule ambaye mamlaka maalum iliyopewa kwa mujibu wa katiba imesema kwamba maisha ya mtu huyo yanatakiwa kukomeshwa kutokana na kosa alilotenda.
Jaji akaendelea kueleza kwamba wakati anaandika hukumu, alirejea katika vipengele hivyo vya sheria vinavyopaswa kuzingatiwa katika kosa la mauaji ya kukusudia.
Akaeleza kuwa katika kurejea vipengele hivyo aligundua kuwa mshitakiwa alikuwa na dhamira ya kuua. Alitekeleza zoezi hilo la mauaji kwa kuwanyonga wahusika wote kama walivyoelezwa katika ushahidi.
Jaji akaeleza kuwa amekuja kugundua kuwa kipengele cha tatu hakikuwepo. Alikitaja kipengele hicho kwamba ni kile kinachomtazama aliyeuawa kama alikuwa na haki ya kuishi.
Akasema watu wote wanne walionyongwa na mshitakiwa hawakuwa na haki ya kuishi baada ya mahakama kuwahukumu kifo na Rais kuidhinisha kunyongwa kwao.
“Kama walionyongwa hawakuwa na haki ya kuishi,” jaji akaendelea, “kosa la kuua kwa kukusudia haliwezi kuthibiti kwa kuuliwa kwao, hata kama aliyewanyonga alijitwalia mamlaka asiyohusika nayo.”
“Kwa sababu hiyo,” jaji akaendelea, “ninakubaliana na upande wa utetezi kwamba kosa aliloshitakiwa mshitakiwa halikuwa sahihi. Mshitakiwa alitakiwa kushitakiwa kwa kosa la kujitwalia mamlaka ya kunyonga ambayo hakupewa kisheria.”
Jaji akaendelea, “Kwa vile mshitakiwa alijitokeza mwenyewe polisi, kwa vile alikiri kosa yeye mwenyewe, na kwa vile ni kosa lake la kwanza, na kwa vile kosa lake lilitokana na makosa ya mkuu wa gereza aliyewatorosha wafungwa hao, ninamhukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja.”
Watu wote waliokuwepo hapo mahakamani walipigwa na mshangao kutokana na adhabu hiyo.
Jaji aliendelea, “Katika kifungo hicho cha nje, mshitakiwa anatakiwa aonyeshe tabia njema na asitende kosa lolote jingine katika muda huo.”
Alipofika hapo, jaji alifunga faili lake akamtazama Faustin.
“Nenda ukatumikie kifungo hicho ukiwa uraiani, na usitende kosa jingine lolote katika muda huo. Maafisa wa magereza watakueleza jinsi ya kutekeleza adhabu yako.”
Jaji akainuka.
“Kooorti!” sauti ikavuma. Jaji akaondoka.
Nilimuona wakili wa Faustin akiinuka kwenda kumpongeza Faustin. Nikamuona mama yake naye akiinuka. Sasa uso wake ulikuwa umejaa tabasamu la furaha.

Wote walikwenda kumkumbatia kizimbani kabla ya Faustin kudakwa na polisi.
“Usije ukaondoka hapa,” polisi mmoja akamwambia.
Baadaye Faustin alichukuliwa na askari wa magereza wakaondoka naye huku mama yake na wakili wake wakiwafuata nyuma.
Kwa vile hukumu ilikuwa imeshatolewa, nilitoka kwa mlango wa nyuma, nikajipakia katika gari na kuondoka. Kazi yangu ilikuwa imekwisha.
“Yule kijana ana bahati sana,” nikajiwazia huku nikiendesha.
Nilimuona alikuwa na bahati kutokana na jaji kukubaliana na hoja ya wakili wake kwamba Faustin hakustahili kushitakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia.
Mimi nilitarajia Faustin asingesalimika. Nilijua angenyongwa au angefungwa kifungo cha maisha. Na hilo ni wazo lililokuwa nalo kila polisi aliyekuwa akifuatilia kesi yake.
Siku ya pili yake nikakutana na Faustin na mama yake wakati ninatoka kwenye mkahawa mmoja ambako nilikwenda kupata chakula.
Walikuwa wanapita. Waliponiona walisimama wakanisalimia.
Tulipeana mikono huku Faustin akionekana mwenye furaha.
Na mimi, kwa mara ya kwanza, nilimtolea tabasamu la uongo Faustin nikamsifu.
“Wewe kijana hatari!” nilimwambia huku nikimnyooshea kidole.
“Kwanini?” Faustin akaniuliza.
“Unajua mwenyewe, lakini umetusaidia kazi. Wale watu uliowanyonga wangetusumbua. Mimi nilikuweka ndani tu kwa sababu mimi ni polisi ninatekeleza kazi yangu, lakini nilitaka nikuachie, na nilijua ungeshinda ile kesi,” nikamwaga uongo wangu ili kujikosha.
“Lakini tunashukuru. Kifungo cha nje cha mwaka mmoja ni afadhali kuliko kufungwa jela au kunyongwa,” mama yake Faustin akaniambia huku naye akionekana mwenye furaha.
“Kifungo cha mwaka mmoja ni sawa na kuachiwa huru, ila mwanao azingatie asitende kosa jingine, hata kama ni kwa bahati mbaya.”
“Nimemuonya sana, hatatenda kosa.”
“Kwa hiyo utaondoka lini kurudi Lindi?”
“Bado nipo nipo.”
“Sawa. Basi mimi nawaaga. Ninarudi ofisini.”
Tukaagana. Nilijipakia kwenye gari na kuondoka.

Kwa upande mwingine, nilishukuru ile kesi kutolewa hukumu. Ingawa ilikuwa hukumu iliyotufadhaisha polisi, tuliikubali kwa vile ulikuwa uamuzi wa mahakama.
Sasa nikaielekeza akili yangu moja kwa moja kwenye ndoa yangu na Hamisa. Wiki moja kabla ya ndoa niliomba likizo ya wiki tatu ili nikamilishe matayarisho ya harusi yetu.
Nilipopata likizo hiyo ndogo ndipo nikajikita katika kushughulikia hatua za mwisho za maandalizi. Baadhi ya ndugu zangu pamoja na wazazi wangu walishafika kutoka kwetu Bagamoyo.
Baada ya wiki hiyo sherehe zikaanza. Nataka nimalizie kwa kusema ilikuwa harusi ya kukata na shoka. Baada ya ndoa yetu iliyofungwa katika msikiti wa Ijumaa maarufu – Msikiti wa Riyadh – msururu wa magari ulielekea Barabara ya Nane alikokuwa Bi Harusi.
Bi Harusi alikuwa amehamishiwa Barabara ya Nane kwenye nyumba ya mama yake mdogo.
Tulipofika, niliingizwa katika chumba alichowekwa nikampa mkono mke wangu. Sheikh aliyetufungisha ndoa akatuombea dua na kututakia maisha marefu, maisha ya heri na fanaka.
Wiki moja tu baada ya kuishi na Hamisa, alikuja kuniambia kitu ambacho sikuwa nikikifahamu.
“Unajua ule ugomvi wetu wa siku ile ulitengezwa na Helena,” akaniambia.
Kwanza nilishituka kwa kuona Hamisa anataka kurudisha mambo ya Helena. Nikamuuliza,
“Helena aliutengeneza vipi ule ugomvi?”
“Aliandaa yeye ile video niliyorushiwa. Maana yake ni kwamba alitaka nione jinsi ulivyokuwa unacheza naye ili tugombane.”
“Na ni kwanini alifanya hivyo?”
“Alifanya vile kwa sababu alikuwa hataki uwe na mimi. Alitaka uwe naye yeye.”
Nikanyamaza kidogo kufikiri, kisha nikamuuliza,
“Wewe ulijuaje?”
“Yule aliyenirushia ile video ndiye aliyekuja kuniambia. Si unajua sisi wasichana kwa umbeya.”
Nilikuwa nimeduwaa nikijiuliza kama Helena aliweza kufanya kitendo kama hicho.
“Ndiyo maana nilirudisha moyo wangu kwako. Sikutaka Helena aendelee kufurahi,” akaendelea kusema Hamisa.
Nikatingisha kichwa changu kuonyesha kukubaliana na Hamisa.
“Mchunge sana Helena, alitaka kukuvunjia uchumba, asije akakuvunjia ndoa yako!”
“Nimeshamjua. Nitajichunga naye.”
“Kama aliweza kuvunja uchumba, hawezi kushindwa kuvunja ndoa!”
“Ni kweli.”
Mpaka hapa ninaposimulia mkasa huu, Hamisa ameshanizalia watoto watatu, na kwa mawazo yangu watoto hao wanatosha kabisa. Nataka tuwasomeshe wapate elimu bora, nikiamini kuwa mmojawapo anaweza kuja kurithi kazi yangu, akawa kachero bora kuliko mimi.