Budeba aeleza sababu Mbuni kuwaka Championship

KOCHA wa Mbuni FC, Leonard Budeba, amesema maandalizi makini na umakini wa wachezaji wake katika kufuata maelekezo ndiyo siri ya ushindi mnono wa mabao 4-0 walioupata dhidi ya Mbeya Kwanza kwenye mechi ya kwanza ya Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026.

Budeba amesema ushindi huo ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanyika mazoezini, akibainisha kuwa kikosi chake kilijikita zaidi katika mazoezi ya kutumia nafasi na kushambulia kwa kasi kwa vipindi vyote, jambo ambalo liliwawezesha kuvunja ngome ya wapinzani.

Amesema mechi hiyo uliyopigwa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, ilikuwa na ushindani mkubwa kutokana na uzoefu wa wapinzani wao ambao wamewahi kucheza Ligi Kuu Bara, lakini kikosi chake kilijibu kwa nidhamu, utulivu na umakini katika dakika zote 90.

Aidha alibainisha kuwa kila mchezaji kutekeleza majukumu na kufuata maelekezo kwa usahihi ndio iliwawezesha kupata matokeo hayo ambayo imeongeza morali na ari ya kupambana zaidi kutafuta nafasi ya kupanda daraja.

Licha ya ushindi huo mkubwa, lakini bado kocha huyo ambaye amedumu kwa muda mrefu na maafande hao kutoka wilayani Monduli tangu timu hiyo ikiwa Ligi ya Mkoa wa Arusha, anasema wako kwenye hatua ya kujenga kujenga kikosi kutokana na uwepo wa wachezaji wapya wanaoendelea kuzoeana.

“Bado tunaunda timu, tuna vijana wapya, lakini najivunia kasi yao ya kujifunza, tunarudi katika uwanja wa mazoefu nitaenda kufanyia kazi mapungufu yote ambayo yalijitokeza”, amesema Budeba.

Budeba aliweka wazi sasa wanageukia maandalizi ya mechi ya pili dhidi ya Bigman itakayopigwa Oktoba 18, 2025 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, akisema mechi hiyo itakuwa kipimo kingine cha ubora wa timu yake.

“Tunajua Bigman ni wapinzani wazuri, lakini wachezaji wangu wamepata nafasi ya kuwaona wakicheza na TMA Stars, tutatumia udhaifu wao, tukiendelea kuboresha ubora wetu,” amesema.

Kocha huyo amewataka mashabiki wa soka Arusha kuendelea kuiunga mkono timu yao, akisema nguvu ya wananchi ndiyo silaha ya Mbuni katika safari ya kupanda Ligi Kuu Bara.

Akizungumzia kichapo hicho, kocha wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi amesema kimempa somo muhimu kuhusu maeneo yanayohitajika maboresho ndani ya kikosi chake, ili kuendelea kupigania nafasi ya kupanda daraja.

Mwalwisi amesema matokeo hayo hayamaanishi wao ni dhaifu, bali ni sehemu ya mchakato wa kujenga kikosi kipya kinachoanza kupata uzoefu wa ligi ngumu kama Championship, ambacho kinahitaji muda ili kuimarika.

Amesema licha ya kipigo hicho, wachezaji wake walionyesha uhai mkubwa, wakipambana hadi dakika za mwisho licha ya changamoto za kiufundi na kisaikolojia zilizojitokeza kutokana na wingi wa vijana wapya ndani ya kikosi.

Kocha huyo alibainisha kuwa mechi hiyo ilikuwa fundisho muhimu kwao kuelekea mechi zinazofuata, hasa wakilenga kurekebisha mapungufu yaliyosababisha kufungwa mabao kirahisi kipindi cha kwanza. “Tumemaliza mchezo wa kwanza na mchezo mgumu, tumepoteza ni sehemu ya mchezo, yale mapungufu yaliyoonekana tunaenda kuyafanyia kazi kuhakikisha tunakuwa bora zaidi,” amesema kocha huyo.