Kigoma. Mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameahidi utekelezaji wa miradi mbalimbali katika wilaya za Kigoma ikiwemo kuimarisha ushirikiano na nchi jirani ili kuchochea shughuli za kibiashara.
Aidha, ameahidi kuboresha huduma za afya, ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, nishati ya umeme, shule, miundombinu ya barabara, kuimarisha shughuli za kilimo na ufugaji pamoja na ujenzi wa masoko.
Dk Nchimbi ametoa ahadi hizo wakati wa mikutano yake ya kampeni ya siku mbili mkoani Kigoma katika wilaya za Kakonko, Kibondo jana na kumalizia leo Jumatatu, Oktoba 13, 2025, Kigoma kwenye Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Amesema ahadi hizo na zingine, zitatekelezwa iwapo tu, chama hicho na mgombea wake wa urais, Samia Suluhu Hassan kitaibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Katika siku ya mwisho mkoani humo, Dk Nchimbi amesema miaka mitano ijayo, Serikali itaimarisha diplomasia ya uchumi na nchi jirani ili mazao yapate masoko kwenye nchi hizo.
“Tutaimarisha mahusiano na nchi jirani zetu kama Burundi, DRC na Zambia ili kuwa na uhakika wa mazao yetu,” amesema Dk Nchimbi.
Ili kuboresha sekta ya kilimo, Dk Nchimbi amesema wanakwenda kuongeza skimu za umwagiliaji, utoaji wa ruzuku, mbegu na madawa.
Amesema miaka minne na nusu ya Rais Samia madarakani, ameonesha kwa vitendo kuwajali wakulima kwani alikuta bajeti ya kilimo ya maendeleo ikiwa Sh294 bilioni na sasa imefikia Sh1.24 trilioni.
“Miradi mikubwa ya umwagiliaji alikuta ikiwa 13 lakini sasa iko 780.
Ruzuku ya mbolea ilikuwa tani 163,000 leo ni tani 848,000, maofisa ugani wamepata vitendea kazi nchi nzima,” amesema Dk Nchimbi.
Katika miaka mitano ijayo, watajenga soko jipya kwa ajili ya mafuta ya mawese na miongoni litajengwa Mwandinga.

Amesema miaka minne iliyopita chakula kilichozalishwa kilikuwa tani milimo 17, leo ni tani milioni 22:”Tumeweza kwa mara ya kwanza kuondokana na changamoto kabisa ya chakula.”
Eneo la afya kwa Kigoma Kaskazini amesema wanakwenda kusogeza huduma kwa wananchi kwa kujenga
vituo vipya vinne vya afya, zahanati mpya saba na nyumba za watumishi sekta ya afya 12.
Amesema wa wanakwenda kujenga shule mpya za msingi tano, za sekondari tatu, madarasa mapya 75, nyumba za walimu 15 na mabweni 11.
Amewaomba wananchi kujitokeza kumpigia kura Rais Samia kwani ameonesha kwa vitendo kwamba anaweza.
“Kila aliyekuwa na mashaka na Rais Samia, kwa sasa amefuta mashaka hayo na amewaheshimisha wanawake na sasa kila aliyekuwa na shaka na uwezo wa mwanamke yeye ameubadilisha kwani ameonesha kwa vitendo kuwa wanaweza,” amesema Dk Nchimbi.
Akiwa kwenye mkutano wa Kakonko, alisema sekta ya ufugaji, Serikali imefanikisha ongezeko kubwa la mauzo ya nyama nje ya nchi, kutoka tani 692 hadi tani 14,701, jambo lililoongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kuboresha maisha ya wafugaji.
“Wafugaji wamejitambua kuwa shughuli wanayofanya ina tija. Katika miaka mitano ijayo, Serikali ya CCM imepanga kufanya kampeni kubwa kuhakikisha kila mfugaji anapata huduma za chanjo, dawa na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa maofisa ugani,” alisema.
Sekta ya maji, Dk Nchimbi alisema wananchi wa Kakonko zaidi ya asilimia 81 wanapata maji safi na salama, kutoka asilimia 61 awali. Hii ni kutokana na kukamilika kwa miradi minne ya maji na upanuzi wa skimu ya maji Mboli.
“Serikali itachimba visima virefu katika vijiji sita, kuboresha skimu za maji katika maeneo matano na kuongeza kasi ya usambazaji wa mtandao wa maji ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hiyo muhimu,” alisema.

Aliongeza kuwa barabara kadhaa zitajengwa kwa kiwango cha lami na changarawe, na madaraja matano ili kuboresha usafiri na biashara katika wilaya hiyo.
Katika mkutano wa leo, Dk Nchimbi amekumbushia historia yake na mkoa huo akisema, “wazee wa zamani walioko hapa wanajua baba yangu alikuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kigoma.
“Na mimi nimesoma shule ya Kihesa. Na uchaguzi wangu wa kwanza katika maisha yangu wa kupigiwa kura, nilipigiwa kura shule ya msingi nikiwa darasa la tatu wakati wanachagua viranja wa shule,” amesema.
Amesema kura zile zilikuwa za wazi zaidi kwa sababu kila bodi ya walimu inapendekeza wanafunzi na ufikiri wanafaa kuwa viongozi, kama nafasi ziko 10 unaleta majina 20 halafu mnapanga mnatazama ukuta, nyie wagombea halafu wanafunzi wanasimama nyuma yenu.
“Kila mtu anaenda kwa anayemtaka awe kiongozi. Angalau ninachokumbuka ni kwamba kura yangu ya kwanza kabisa katika maisha ya kupigiwa kura ilikuwa ya kaka yangu anayefuatia ambaye alikuwa amenitangulia darasa moja, anaitwa Wilfred Nchimbi,” amesema.
Amesema Wilfred alisimama na kumweleza yupo nyuma yake na kukweleza niko hapa nyuma yako, usiogope kura nyingi tu.
“Ninapokuwa Kigoma, nakuwa kama niko nyumbani, hata bibi yangu kizaa baba amezikwa Kigoma. Mjue mimi ni ndugu yenu,” amesema Dk Nchimbi.
Mgombea ubunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba amesema, Rais Samia alifanya uamuzi sahihi kumteua Dk Nchimbi kuwa mgombea wake mwenza wa urais.
Serukamba amesema Dk Nchimbi atakuwa msaidizi sahihi wa Rais Samia mara baada ya uchaguzi mkuu kwani ni mzalendo na mtu makini.
Amesema Ilani ya uchaguzi ya chama hicho kwa mwaka 2025/2030 imebainisha jinsi inavyokwenda kutatua changamoto za maji, afya, barabara na hana shaka chama chake kinakwenda kutekeleza kwa vitendo.
Naye mgombea ubunge wa Kakonko (CCM), Allan Mvano alishukuru maendeleo makubwa katika wilaya hiyo ndani ya miaka minne, akibainisha zaidi ya Sh128.9 bilioni zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali.
“Kuna hospitali mpya ya wilaya yenye thamani ya Sh4.9 bilioni, vituo viwili vya afya na zahanati katika vijiji sita. Sekta ya elimu imepata shule nane mpya za sekondari kwa gharama ya Sh3.8 bilioni, shule mbili za msingi na ujenzi wa Chuo cha Veta chenye thamani ya zaidi ya Sh800 milioni,” alisema Mvano.
Alisema stendi mpya ya kisasa yenye thamani ya Sh3.5 bilioni imekamilika na imeanza kutumika, vibanda 34 vya biashara vimejengwa katika soko jipya na huduma za maji na umeme zimeenea katika maeneo yote ya wilaya hiyo.