Cheche alia na mambo mawili Chama la Wana

KOCHA Mkuu wa Stand United ‘Chama la Wana’ ya Shinyanga, Idd Cheche amesema kukosa umakini eneo la ulinzi na utumiaji sahihi wa nafasi za kufunga kimewaangusha katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Championship msimu huu.

Stand United ilianza vibaya msimu huu kwa kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Songea United kwenye Uwanja wa Majimaji.

Baada ya mechi hiyo, Stand United inayosaka nafasi ya kurejea Ligi Kuu Bara, itasafiri kwenda jijini Mbeya kucheza na KenGold Oktoba 19, 2025 kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Sokoine.

Akizungumza baada ya kichapo hicho, Cheche amesema licha ya vijana wake kucheza vizuri na kupambana lakini walipoteza umakini na kuruhusu mabao mawili ambayo yalitokana na makosa binafsi ya wachezaji.

CHE 01

“Tulijaribu kucheza vizuri na kupata nafasi zaidi ya mbili za kufunga mabao lakini tumezipoteza na kuwafanya wenzetu warudi kipindi cha pili wamechangamka zaidi yetu, japokuwa hawakuwa vizuri kutuzidi lakini ule uchangamfu wao umewapa ushindi,” amesema.

Aliongeza kuwa: “Tuna makosa pale nyuma ambayo tumefanya na kuruhusu bao la pili na ukitazama mabao yote mawili tuliyofungwa tungekuwa makini tusingepoteza.”

CHE 02

Kocha huyo wa zamani wa Azam FC, amesema eneo la ushambuliaji bado lina shida ya matumizi ya nafasi, hivyo wanakwenda kufanya maboresho ili matatizo hayo mawili yasijirudie katika michezo inayofuata.

Stand United tangu ishuke Ligi Kuu Bara 2018-2019 ilipomaliza nafasi ya 19, imekuwa ikipambana kurejea, lakini haijafanikiwa.