KIPA wa Mbeya City, Beno Kakolanya amesema katika mechi tatu walizocheza zimewapa picha ya ushindani mkali watakaokabiliana nao msimu huu, hivyo wanajipanga kuhakikisha hawatoki katika mstari wa malengo yao.
Kakolanya katika mechi hizo tatu amepata klinshiti mbili. Mbeya City ilianza na ushindi wa bao 0-1 ugenini dhidi ya Fountain Gate, kisha ikafungwa ugenini mabao 2-0 na Azam FC na kutoka suluhu nyumbani dhidi ya Yanga.
“Tumeanza na mechi ngumu, mfano dhidi ya Azam na Yanga ambazo zina wachezaji wenye viwango vya juu wanaozichezea timu zao za taifa, hilo limetupa picha ya namna gani tuendelee kukaza buti,” amesema Kakolanya aliyewahi kuzichezea Simba, Yanga, Singida Black Stars, Namungo, Tanzania Prisons na timu ya taifa ya Tanzania.
Amesema ugumu wa hizo mechi anaamini timu inayojipanga vizuri inakuwa na uwezo wa kupata matokeo ya ushindi iwe nyumbani ama ugenini.

“Timu zimejipanga na zimesajili vizuri, msimu huu unahitaji kujitoa zaidi na kuwa fiti muda wote kuhakikisha unaipambania timu kupata matokeo ya ushindi, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya msimamo wa Ligi Kuu Bara,” amesema Kakolanya na kuongeza;
“Kinachonifurahisha ligi inakwenda kuonyesha viwango bora vya wachezaji kupambana zaidi hivyo mashabiki watakuwa na mvuto wa kuzifuatilia mechi.” Mbeya City imerejea Ligi Kuu Bara baada ya kukosekana kwa misimu miwili ambayo ni 2023-2024 na 2024-2025. Timu hiyo ilishuka daraja msimu wa 2022-2023 baada ya kuwepo ndani ya Ligi Kuu Bara kwa takribani misimu kumi tangu msimu wa 2013-2014.