Rombo. Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, amewataka walimu wilayani humo kuacha tabia ya kusemana na kufitiniana kazini, badala yake waimarishe umoja na mshikamano ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema migogoro na fitina kazini huchangia kudhoofisha morali ya kazi miongoni mwa walimu, jambo linaloweza kuathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu.
Mwangwala alitoa kauli hiyo leo Oktoba 13, 2025 wakati akizungumza na walimu ambao ni wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani humo, katika maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani yaliyofanyika katika Tarafa ya Mashati.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala akizungumza na walimu ambao ni wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani humo(hawapo pichani) katika maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani yaliyofanyika katika Tarafa ya Mashati.
“Niwapongeze CWT kwa kuonyesha kuwa ninyi ni chama mama cha walimu kinachobeba masilahi yenu. Najua walimu tupo wengi, lakini kinachotupoteza mara nyingi ni maneno mengi,” amesema DC Mwangwala.
Ameongeza kuwa walimu wanapaswa kujenga upendo na kusema mazuri juu ya wenzao badala ya majungu.
“Tupendane, majungu hayajawahi kumfikisha mtu mahali popote, walimu sisi ndiyo tunaongoza kwa kusemana na kufitiniana, tuache tabia hiyo, tuzungumze mazuri ya wenzetu, kwa sababu huwezi jua nani atakusemea kesho,” amesisitiza.
Aidha, aliwaonya baadhi ya wakuu wa shule wanaoongoza wenzao kwa amri badala ya mashauriano, akisema mtindo huo haujengi mafanikio ya kitaaluma.
“Mmesema baadhi ya viongozi wa shule hawana ushirikiano na wenzao na badala yake kuongoza kwa mtindo wa amri, hili nalikataza, mwalimu aheshimiwe,” amesema
Mwangwala amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na maslahi ya walimu, ili kuinua ubora wa elimu nchini.
Kwa upande wake, Katibu wa CWT Wilaya ya Rombo, Nazama Tarimo, amesema baadhi ya viongozi wa shule bado hawatilii mkazo ushirikiano kazini, jambo linalosababisha changamoto katika utekelezaji wa majukumu.
“Tunahitaji kujenga mazingira rafiki ya ushirikiano baina yetu na viongozi wetu ili kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma,” amesema Tarimo.