Dhamana ya Sh2.4 trilioni yachochea uwekezaji sekta ya kilimo nchini

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa nchini ndani ya kipindi cha miaka mitano, Taasisi Pass Trust, imetoa dhamana ya Sh2.4 trilioni kwa wakulima, kupitia mikopo kutoka taasisi za kifedha.

Leo Oktoba 13, 2025, wakati wa maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo Mkurugenzi wa Biashara wa Pass Trust, Adam Kamanda, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa mpango huo, taasisi imefanikiwa kutoa dhamana ya Sh2.4 trilioni kwa wakulima kwa kipindi cha miaka 25.

“Mpaka sasa tumeweza kutoa dhamana ya Sh2.4 trilioni kwa wakulima wetu, tunaishukuru sana Serikali kwa kutambua umuhimu wa kilimo na kuongeza bajeti ya sekta hiyo hadi kufikia Sh1.2 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026, huku tukiangazia kilimo cha umwagiliaji na uboreshaji wa mazingira ya kilimo,” amesema Kamanda.

Kamanda amefafanua kuwa, Pass Trust inaendelea kujizatiti kuweka mbele masilahi ya wakulima kwa kutoa dhamana hadi asilimia 80 kwa kila mkopo wa kilimo unaotolewa.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amesema kuwa ongezeko la bajeti kwa sekta ya kilimo ni ishara ya umuhimu mkubwa wanaopewa wakulima nchini.

“Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa hili. Serikali inaendelea kuwekeza kwa kuongeza bajeti ya kilimo kwa miaka minne mfululizo. Mkulima anapaswa kuthamini kile anachokifanya kwa kiwango cha juu, kwani wao ndiyo wanaochangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa vyakula na bidhaa nyingine muhimu,” amesema Mapunda.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtuis Mapunda akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa taasisi inayojiusisha na masuala ya kilimo nchini Pass Trust leo Octoba 13, 2025 kwenye kituo cha mikutano cha Jlius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mapunda pia ameongeza kuwa, ili Tanzania ifikie maendeleo ya kiuchumi, ni muhimu sekta ya kilimo ihusishwe na teknolojia, elimu, na uwezeshaji kutoka serikali na wadau wengine.

Meneja wa Mahusiano wa Benki ya Ushirika, Hadija Seif, amesema kuwa kilimo cha Tanzania kinakabiliwa na changamoto nyingi, lakini msaada wa taasisi za kifedha kama Pass Trust unachangia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta hiyo.

“Kwa ushirikiano wetu na Pass Trust, tumekwishatoa mikopo ya Sh8 bilioni kwa wakulima wadogo. Huu ni mwanzo mzuri, lakini tunahitaji msaada zaidi kutoka taasisi zingine ili kilimo kije kuwa sekta inayoendeshwa kwa ufanisi,” amesema Hadija.