Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Geita.
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameeleza hatua mbalimbali ambazo Serikali katika miaka mitano iliyopita imezichukua katika kuboresha maisha ya wananchi wa Mkoa wa Geita.
Aidha amesema nguzo za kuu za uchumi katika mkoa huo wa Geita ni madini, kilimo na ufugaji hivyo katika miaka mitano jitihada za Serikali zilielekezwa kwenye huduma za jamii, ujenzi wa miundombinu na mipango ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Akizungumza leo Oktoba 12,2025 alipokuwa akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Jimbo la Geita Mjini mkoani Geita Mgombea Urais Dk.Samia amebainisha hatua hizo ambazo zimechukuliwa kuboresha maisha ya wananchi yanalenga kuwafanya wananchi washiriki kikamilifu shughuli za uzalishaji katika sekta hizo.
“Matokeo ya jitihada hizo za pamoja baina ya Serikali na wananchi yanaonekana wazi kwani Geita kuna ustawi mkubwa wa kiuchumi.Geita ninayoijua mimi ya miaka 10 nyuma siyo ile ninayoiona leo,maendeleo ni makubwa,”amesema Dk.Samia.
Akieleza mbele ya wananchi hao Dk. Samia amefafanua Ilani ya uchaguzi (2025 – 2030) imeelekeza masuala mbalimbali ikiweml sekta za uzalishaji zenye kuleta mageuzi ya kiuchumi.
Ameongeza katika sekta hizo,katika sekta ya kilimo lengo la serikali ifikapo 2030 ukuaji wake ufikie asilimia 10.
Pia, amesema kwamba kuwa Ilani ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2025-2030 imeelekeza katika ufugaji serikali itaendelea kutoa chanjo kwa mifugo, ujenzi wa majosho na machinjio.
“Ilani pia ina inaelekeza kwenye ujenzi uchumi wa viwanda, kuimarisha biashara na fursa za ajira kwa vijana.Serikali itajenga viwanda vya kuchakata alizeti maeneo ya Nyaluanzaga, Bukoli na Busanda huku viwanda vya kusindika matunda vitajengwa eneo la Igate.
“Kitaifa tunataka kuikuza sekta ya viwanda kutoka ukuaji wa asilimia nne ya sasa mpaka asilimia tisa mwaka 2030,” amesema Dk.Samia.
Kuhusu sekta ya madini Dk.Samia Suluhu Hassan amesema mkakati wa serikali katika miaka mitano ijayo itajenga maabara ya kisasa katika Mkoa huo wa Geita ambayo itarahisisha kazi za wachimbaji badala ya kufuata huduma hiyo maeneo ya mbali.
Pia amesema Serikali inajiandaa kutoa mitaji kwa wachimbaji wadogo kuwakuza wawe wachimbaji wakubwa kisha kupima maeneo mapya ya uchimbaji.
“Tunakwenda kupima zaidi maeneo ya nchi yetu kujua madini yapo wapi ili uchimbaji ukiwe zaidi hasa kwa wachimbaji wadogo.
“Uwanja wa maonyesho wa madini kwenda kuujenga kuwa uwanja wa kimataifa, kuwa uwanja wa mikutano wa sekta ya madini na uwanja wa maonyesho,” amesisitiza.
Akizungumza sekta ya usafiri na usafirishaji, amesema Ilani imeagiza uendelezaji ujenzi wa barabara ambapo kifungu cha 41 A kifungu kidogo G katika ilani ya mkoa huo kimeeleza barabara zitakazojengwa.
Ameongeza pia Ilani inaelekeza kujenga viwanja vya ndege ambapo katika mkoa huo kitajengwa kiwanja cha ndege Geita na kukiendeleza kiwanja cha ndege Chato.
Kwa upande wa usafiri majini, amesema kwamba maeneo yote yenye kuhitaji vivuko serikali itajenga miundombinu ya vivuko kuwezesha usafirishaji wananchi.
Wakati katika nishati amesema Serikali amesema mpango wa Serikali ni kujenga kituo cha kupoza umeme ambacho kitahakikisha umeme ndani ya mkoa huo unapatikana muda wote.
“Nishati hiyo itawezesha wananchi kufanya shughuli zao viwandani na katika makazi yao.Tutamalizia ile ngwe yetu ya umeme kwenye vijiji vilivyobakia na vitongoji lakini pia umeme kwenye visiwa.”