Shinyanga. Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo ameahidi kuwa endapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza Taifa, atapitia upya mikataba ya uwekezaji katika sekta ya madini nchini ili kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na uwepo wa rasilimali za madini.
Amesema mchakato huo utafanyika ndani ya miaka mitano ya uendeshaji wa nchi kwani ni mchakato unaohusisha masuala ya sheria, ukilenga kuondoa changamoto ya ajira kwa kutanua fursa ambazo hazipo kwa ajili ya watu kupata cha kufanya.
Doyo ametoa ahadi hiyo leo Oktoba 13, 2025 katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya kituo cha mabasi CDT.
Ametolea mfano wa nchi za Falme za Kiarabu wanaotegemea uchimbaji wa dhahabu na gesi lakini maisha ya wananchi wao yanaonekana kuwa bora tofauti na wanashinyanga kuwa na madini lakini bado wanakabiliwa na umasikini mkali.
Amesema endapo atagundua mikataba hiyo haina maslahi kwa Watanzania ataivunja na kuwaondoa wawekezaji wote kwenye migodi husika na kuanza upya ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote.
Amesema: “Tunataka kutumia rasilimali za madini kwa ajili ya maisha yenu wanakahama na Shinyanga kwa ujumla, tuna dhahabu hapa Kahama na almasi kule Shinyanga, lakini madini haya pamoja na kuchimbwa, hayaonyeshi ni namna gani yanawanufaisha Watanzania waliopo katika hayo maeneo.”
Amesema: “Endapo tutashinda tutahakikisha kwamba asilimia 40 ya maduhuli yanayokusanywa yanarudi kwenye Halmashauri husika kwa ajili ya kuwapa wananchi mikopo isiyo na riba ili waendeshe maisha yao.”
Katika kuendelea kutatua changamoto ya ajira, amesema katika kipindi cha miezi sita ya kwanza baada ya kuchaguliwa, atahakikisha Wilaya ya Kahama inakuwa na soko la kisasa la bidhaa kutokana na lililopo kutokidhi mahitaji ya wananchi.
Amesema: “Nitakaposhinda ndani ya kipindi cha miezi sita nitahakikisha na jenga soko la kisasa hapa Kahama ili wananchi walitumie kuuza na kununua bidhaa kuondoa adha ya ajira na vijana kuzurura ovyo mtaani.”
Kuhusu suala la afya kwa wananchi, Doyo amesema ataajiri madaktari wa kibingwa na wataalamu wa kada ya kati 15,000 kuhakikisha anamaliza changamoto ya madaktari na wataalamu wa kada ya afya kwenye vituo vyote vya kutolea huduma nchini.
Amesema: “Tutaboresha vifaa tiba pamoja na kuajiri madaktari bingwa na wataalamu wa kada ya kati 15,000 kuhakikisha tunamaliza kabisa ukame wa madaktari pamoja na wataalamu wa afya.”
“Tutasimamia kupata madaktari bingwa katika hospitali zetu na zahanati na vituo vya afya, tutapata wataalamu, vifaa tiba na dawa. Na kwa magonjwa ya kawaida yasiyokuwa na gharama kubwa yatatolewa bila malipo kwa kila Mtanzania,” ameongeza.
Kwa upande wa sekta ya elimu, Doyo amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwaongoza, atasimamia suala la utolewaji wa elimu ya vitendo itakayomuwezesha mtoto kuingia kwenye ushindani wa soko la ajira.
“Sisi tumekubaliana kwamba endapo tutachaguliwa, tutawawezesha Watanzania kupata elimu kwa vitendo ambayo itawasaidia kuingia kwenye ushindani wa soko la ajira popote anapokwenda.”
Kuhusu miundombinu, Doyo amesema atajenga barabara zote za vijijini kwa kiwango cha zege ili zidumu kwa muda mrefu zaidi na kumrahisishia mkulima kupitisha mazao yake kwenda sokoni.
Amesema barabara zote zinazounganisha wilaya na mikoa zitajengwa kwa kiwango cha lami kuchechemua uchumi wa maeneo husika hasa makao makuu ya wilaya na mikoa.
“Tutajenga barabara zote za vijijini kwa kiwango cha zege ili wananchi waweze kusafirisha mazao yao ya kilimo kwenda sokoni, lakini barabara zote zinazounganisha wilaya na mikoa yote nchini kwa kiwango cha lami kukuza uchumi wa maeneo husika,” amesema.
Mkazi mmoja wa Kahama, Mariana John amesema: “Kampeni ni suala moja na utekelezaji ni suala jingine, sasa hivi wananchi tumeamka, tunaelewa kila kitu kwa hawa wanasiasa. Niwaombe haya wanayoyatamka tukiwachagua wakayatekeleze, hata wabunge na madiwani wakatekeleze wanachoahidi majukwaani, waache siasa za danganya toto.”
Naye Salum Shaibu amewaomba wanasiasa wanaopita kufanya mikutano ya kampeni kuhubiri amani kwenye maeneo wanayoyafikia ili Taifa liendelee kuwa salama.
“Nawashauri hawa wagombea wanaopata nafasi ya kufika kila eneo, wazungumzie sana amani na mshikamano, maana tunayasikia mengi, wasiache mambo yakaharibika, wayasemee haya kila mahali kila mara itatusaidia hata sisi tusiopenda vurugu vurugu,” amesema.