Aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Viktoria,Ezekiel Wenje
………….
CHATO
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya ziwa Viktoria, Ezekiel Wenje, ametangaza kukihama Chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai ya kuvutiwa na misingi imara iliyowekwa kwaajili ya kulinda amani na utulivu wa nchi.
Mbali na hilo, amedai kuwa maendeleo ni mchakato na kwamba hakuna nchi yoyote duniani iliyokwisha kukamilisha maendeleo kwa wananchi wake ikiwemo ajira kwa kila raia.
Kutokana na hali hiyo, amekipongeza CCM kwa kuhakikisha kinapambana kuwaletea maendeleo wananchi wake na kwamba ni wakati sahihi kwake kuungana na Chama hicho ili kupata nafasi ya kutoa ushauri kwaanufaa ya nchi.
Ametoa kauli hiyo wilayani Chato mkoani Geita baada ya kupokelewa na Katibu mkuu wa CCM, Balozi Asha Rose Migilo, kwenye mkutano wa kampeni za Urais,Wabunge na Madiwani nchini zilizofanyika kwenye stendi ya zamani ya mabasi ya Muungano, maarufu mataa.
Akiwa mbele ya mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wenje amewaonya wanachama wa Chadema wanaojiandaa kufanya maandano ya kupinga Uchaguzi mkuu Oktoba29, mwaka huu kujiepusha na kitendo hicho kwa sababu hakina afya kwa taifa.
Amesema viongozi wanaohamasisha wananchi kuandamana familia zao zipo nje ya nchi, na kwamba iwapo yatatokea machafuko nchini, familia zao hazitaweza kudhurika badala yake waliopo nchini ndiyo watakubwa na mateso na majuto.
Kutokana na hali hiyo, amewataka kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi kwa kuhakikisha wanakipigia kura nyingi ili kiendelee kuongoza nchi na kusimamia maendeleo, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Kwa upande wake Mgombea Urais kupitia CCM na mwenyekiti wa Chama hicho, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amedai kufurahishwa na ujio wa kiongozi huyo wa Chadema, huku akimpokea kwa mikono miwili na kumkaribisha kuwa mwanachama mpya wa Chama hicho.
Kadhalika amewataka wananchi waliojitokeza kumsikiliza kukichagua CCM kwa kura nyingi kwa kuwapigia kura mgombea Urais,Wabunge na Madiwani ili wakaendelee kupeleka maendeleo kwa jamii.
Amesema licha ya kuachiwa miradi mikubwa na ya kimkakati na mtangulizi wake aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ameendelea kusimama imara na sasa miradi mingi imekamilika na imeanza kazi.
Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na Bwawa la kufua umeme la mwalimu Nyerere, Reli ya kisasa, daraja la Kigongo Busisi, serikali kuhamishia makao makuu ya nchi, bomba la mafuta kutoka Uganda pamoja na ujenzi wa eneo maarufu kwa jina la mji wa Magufuli jijini Dodoma.
Hata hivyo ameitaka baadhi ya miradi iliyotekelezwa wilayani Chato kuwa ni pamoja na ukamilishaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ambayo inakusudiwa kutoa huduma za kibingwa na ubobevu ili kuwapunguzia wananchi gharama za kwenda hospitali ya Jakaya Kikwete Dar es Salaam.
Mingine ni ujenzi wa nyumba za kitalii ndani ya hifadhi taifa ya Burigi-Chato,hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo,Chuo cha usimamizi wa fedha (IFM), Stendi ya mabasi, Veta, pamoja na ujenzi wa jengo la nyota tano kwaajili ya shughuli za utalii.
Vilevile amemzungumzia Hayati Magufuli kama Mzalendo,shupavu na mpenda maendeleo wa kweli na kwamba anajivunia kufanya naye kazi kwa madai alimfundisha kufanya kazi kwa bidii na kwamba ndiyo siri ya kufanikiwa kwake.
Mwisho.