Dar es Salaam: Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo Oktoba 13, 2025 inaendelea kuunguruma Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, baada ya mapumziko ya mwisho wa Juma.
Katika mwendelezo huo wa usikilizwaji kesi hiyo leo Mahakama hiyo itatoa uamuzi wa pingamizi la Jamhuri dhidi ya maombi ya Lissu, aliyeiomba Mahakama hiyo iyapokee maelezo ya maandishi ya shahidi wa pili yawe kielelezo cha upande wake.
Lissu aliomba maelezo hayo yawe kielelezo cha upande wake katika kesi hiyo ili ayatumie katika kuhoji kuaminika kwa shahidi huyo, kuonesha mkinzano kati ya ushahidi wake wa maandishi na ule alioutoa kwa mdomo kizimbani chini ya kiapo.
Waendesha mashtaka wa kesi hiyo walimwekea pingamizi kuwa mshtakiwa huyo hajafuata masharti yaliyowekwa na sheria pamoja na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake wa mashauri mbalimbali namna ya kupokea maelezo kama hayo.
Baada ya uamuzi huo Mahakama hiyo itaendelea kupokea ushahidi wa ziada wa shahidi huyo, wakati akihojiwa na mshtakiwa Lissu maswali ya dodoso, kuhusiana na ushahidi wake wa msingi alioutoa wakati akiongozwa na mwendesha mashtaka.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kwa lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchapisha maneno yafuatayo:-
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndungiru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Shahidi wa pili wa Jamhuri katika kesi hiyo ni Mkaguzi wa Polisi, John Kaaya, kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni, Dawati la Doria Mtandaoni, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Makao Makuu, Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake wa msingi akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu Job Mrema, pamoja na mambo mengine shahidi huyo alieleza kuwa Aprili 4, 2025 wakati akifanya doria mtandaoni Youtune, kwenye Jambo TV aliona picha mjongeo (video clip ) inayomuonesha Lissu.
Alieleza kuwa baada ya kuisikiliza alibaini baadhi ya matamshi yenye viashiria vya jinai, ya kuitishia Serikali.
Kutokana na ushahidi wake huo Lissu alianza kumuhoji maswali mbalimbali na sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo:
Lissu: Shahidi, ulisema maneno ” Nitaenda kuzuia uchaguzi, nitahamasisha uasi nitaenda kuvuruga sana sana na mahakamani hakuendeki ndio yalikufanya uamini kuwa ni kuitisha Serikali, ni kweli?
Shahidi: Ni kweli, uchaguzi unaandaliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu na unasimamiwa na Serikali .
Lissu: Ieleze mahakama kama unafahamu kwa zaidi ya miaka 30 , viongozi wa vyama vya upinzani wameweza kutumia mahakama kudai katiba na uchaguzi huru bila mafanikio?.
Katika mfululizo wa maswali hayo Lissu alirejea jitihada za wanasiasa kupinga na kupigania sheria zinazowezesha uchaguzi huru na wa haki na haki nyingine za kisiasa, zikiwemo kesi zilizofunguliwa mahakamani, kama anafahamu.
Miongoni mwazo ni zile zilizofunguliwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Democratic Party (DP) Mchungaji Christopher Mtikila, mwaka 1993 na mwaka 1995 Mahakama Kuu na Mahakama Haki ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
Miongoni mwa kesi hizo aliitaja kesi kuruhusiwa mgombea binafsi ambayo Mahakama Kuu ilikubaliana naye, lakini Mahakama ya Rufani ikatengua hukumu ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu na Watu mwaka 2011 iliiamuru Serikali ya Tanzania kurekebisha sheria.
Shahidi huyo alijibu kuwa hafahamu na kwamba miaka hiyo yeye alikuwa shuleni.
Nyingine ni iliyofunguliwa na viongozi wa vyama vya siasa wakiwamo Freeman Mbowe, Zitto Kabwe, Hashimu Rungwe, Seif Sharif Hamad, Salum Mwalimu na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania ( THRDC) dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, 2019, wakipinga vifungu vya Sheria ya Vyama vya Siasa?
Kesi ambayo Lissu Lissu alimuuliza shahidi kama anafahamu kuwa katika kesi hiyo Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, 2022 iliitaka Tanzania irekebishe hivyo vifungu vya sheria vinavyokandamiza misingi ya katiba.
Pia Lissu alirejea kesi ya kikatiba kupinga wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na manispaa kusimamia uchaguzi iliyofunguliwa mwaka 2021 na Bob Chacha Wangwe ambayo Mahakama Kuu ilikubaliana naye, lakini Mahakama ya Rufani ikaitengua, akamuuliza shahidi kama anafahamu naye akajibu kuwa hafahamu, kisha Lissu akamuhoji:
Lissu: Unafahamu maana ya kauli yangu kuwa ” Mahakamani hakuendeki” si ulisema hivyo kwenye ushahidi wako jana?
Shahidi: Inategemea na maana unayotaka.
Lissu: Narudia kama anafahamu kauli yangu niliyoitoa kuwa ‘Mahakamani hakuendeki’
Lissu : Hayo maeneo yalikuwa na maana gani?
Shahidi: Ulitamka majaji ni watu wa maraisi na kwamba ni maccm.
Lissu: Nilikueleza kuwa mahakamani hakuendeki nilikuwa na maanisha kuwa tumejaribu kwenda mahakamani kwa zaidi ya miaka 30 na bado mahakamani hakuendeki utasemaje?
Lissu : Jibu kwa sauti shahidi , maana mkiwa huko mtaani mnatukoromea, mkija hapa mnanywea. Unafahamu licha ya jitihada za kudai mabadiliko ndani ya mahakama.
Pia Lissu alimuuliza shahidi huyo kuwa kumekuwa na jitihada za kudai mabadiliko ya sheria na kikatiba nje ya mahakama zaidi ya miaka 30 na shahidi akajibu kuwa hauwepo katika jitihada hizo.
Lissu alirejea hatua mbalimbali nje ya Mahakama zikiwemo Tume zilizoundwa na marais wa awamu tofautitofauti ikiwemo Tume ya Jaji Mkuu, Francis Nyalali ya mwaka 1991 kuangalia mifumo ya vyama vingi, ambayo pamoja na mambo mengine ilipendekeza kuwe na Katiba Mpya na Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi alilikataa.
Tume nyingine ni ya Jaji Robert Kisanga iliyoundwa na Rais Benjamini Mkapa mwaka 1998 kuchunguza matatizo yanayotokana na Katiba ya nchi, na nyingine aliyoiunda mwaka 2003 iliyoongozwa na Jaji Mark Boman.
Vilevile alirejea Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba iliyoundwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete mwaka 2011 na kwamba Serikali ya Kikwete ilikataa mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba.
Lissu pia alirejea mazungumzo ya maridhiano baina ya Chadema na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2022 na kwamba Mei 31, 2023 CCM ilikataa mapendekezo ya Chadema na mambo yote yaliishia hapo.
Lissu alipomuuliza shahidi huyo kama anafahamu jitihada hizo, alijibu kuwa hafahamu , mengine aliwahi kusikia mengine hakuwepo, kisha Lissu akauliza:
Lissu: Sasa kwa juhudi zote tulizofanya kuanzia mwaka 2004 hadi sasa, utakubaliana na mimi kuwa hatukufanikiwa mahakamani na kwa mazungumzo.
Lissu: Kwani tuna Katiba mpya mpaka sasa?
Shahidi: Tuna tumia ileile ya zamani.