Lissu alivyoibua malumbano kuhoji kiwango cha elimu ya shahidi

‎‎Dar es Salaam.  Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameibua malumbano ya hoja za kisheria kati yake na waendesha mashtaka katika kesi ya uhaini inayomkabili, baada ya kuuliza maswali yanayohusu kiwango cha elimu cha shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri.

Malumbano hayo yalijitokeza wakati Lissu akiendelea kumhoji shahidi huyo kwa mtindo wa maswali ya dodoso, akichambua maelezo yaliyomo kwenye ushahidi wa maandishi pamoja na ule wa mdomo alioutoa kizimbani chini ya kiapo.

Katika mchakato huo, Lissu alimuuliza shahidi huyo maswali mbalimbali kuhusu elimu yake, yakiwamo ya kiwango cha ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne.

Swali hilo lilipingwa na upande wa mashtaka, hatua iliyosababisha mabishano ya hoja za kisheria baina ya pande hizo mbili.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Mahakama iliingilia kati na kutoa uamuzi uliokubaliana na pingamizi lililotolewa na upande wa Jamhuri, hivyo kuzuia swali hilo kuendelea.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, akidaiwa kutoa maneno yenye lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Inadaiwa kuwa, Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri, Lissu alitoa maneno yaliyodaiwa kuwa na nia ya kuhamasisha uasi na kuvuruga uchaguzi kwa kuchapisha ujumbe katika mitandao ya kijamii akisema:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli… kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko… kwa hiyo tunaenda kukinukisha… sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kweli kweli… tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, wakisaidiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Shahidi wa pili wa Jamhuri ni Mkaguzi wa Polisi, John Kaaya kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni (Dawati la Doria Mtandaoni), Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Makao Makuu Dar es Salaam.

Leo, mshtakiwa Lissu ameendelea kumhoji shahidi huyo kwa maswali ya dodoso, hali iliyosababisha malumbano hayo ya hoja za kisheria kuibuka ndani ya ukumbi wa Mahakama.

Lissu:  Shahidi, waeleze waheshimiwa majaji kama umewahi kuhudhuria mafunzo ya shule ya msingi.

Shahidi: Mwaka 1989 mpaka 1995

Shahidi: Nilisoma shule mbili, kwanza Shule ya Msingi Nganyeni Marangu kisha  Lyakirimu Primary School, Marangu Moshi Kilimanjaro.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama  umewahi kuhudhuria mafunzo ya elimu ya sekondari.

Shahidi: Ndiyo, 1996 mpaka 1999 Shule ya Sekondari Lyakirimu.

Lissu: Ulipata divisheni ngapi kidato cha nne Lyakirimu Secondary School?

Kabla ya shahidi hajajibu swali hilo mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Ajuaye Zegeli amesimama na kupinga swali hilo, akidai kuwa halihusiani na ushahidi wake.

“Waheshimiwa majaji  kwa mujibu wa kifungu cha 167 cha Sheria ya Ushahidi (Tanzania Evidence Act – TEA),  tunapinga kuhusu ufaulu wake kwa sababu hilo swali halihusiani,” amesema Wakili Zegeli na kusisitiza kuwa, suala la msingi ni kwamba alihitimu elimu kiwango hicho.

Hoja hiyo imeungwa mkono na Wakili wa Serikali  Mkuu, Nassoro Katuga  ambaye pamoja na mambo mengine amesema, maswali ya namna hiyo yakiruhusiwa shahidi anayeweza kuulizwa Masjala ya kifamilia kama idadi ya wake na watoto.

Wakili Katuga amesema kimsimgi swali hilo halina msingi maana shahidi hajazungumzia hata elimu ya sekondari ina athari gani kwenye ushahidi wake na hata hajaizungumzia .

Pia, Wakili Katuga amesema kuna Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, inayolinda taarifa Binafsi kama hizo.

“Tunaomba mshtakiwa ajikite kwenye mambo yatakayoisadia Mahakama kufikia uamuzi,” amesema Wakili Katuga.

Akijibu pingamizi hilo, Lissu amesema yeye haulizi swali bila sababu ya msingi na kwamba suala la elimu ya shahidi huyo  limejitokeza sana kwenye ushahidi kwa kuwa, ameulizwa sana elimu yake alikopita.

“Wasingetaka wasingelizungumzia suala la elimu yake, lakini kwa kulianzisha wamefungua milango, hivyo wavumilie,” amesema Lissu.

Pia, Lissu amesema  suala la elimu linahusika sana kwenye ajira ya polisi kwa kuwa, Mwongozo wa Utendaji Kazi wa Jeshi la Polisi (Police General Order – PGO )  54(1) unasema anapaswa kuwa na elimu ya sekondari kidato cha nne.

Vilevile Lissu amedai kuwa, kwa mujibu wa PGO 53(10) suala la elimu linahusika katika kupandishwa daraja.

Lissu amesisitiza kuwa, suala la elimu ni muhimu sana kujua kama shahidi huyo anafaa kuwa polisi, maana kama amepata daraja sifuri hafai.

Pia, amesema shahidi aliulizwa sana katika ushahidi wake wa  msingi kuhusu ujuzi wake lakini pengine ana divisheni sifuri..

“Hivyo hawawezi kusema kuwa ushahidi huu ni irrelevant (hauna uhusiano) wasingelileta. Na ili kuwa askari na ili kupanda cheo lazima awe na kisomo,” amesema Lissu.

 “Kwa hiyo, huu ushahidi unahusiana, maana nataka kujua kwenye kesi kubwa ya uhaini Jamhuri imeleta mashahidi wa aina gani wa elimu na ujuzi gani.”

Akijibu hoja hizo za Lissu, Wakili Katuga amedai kuwa mshtakiwa hakuelewa na wao hawakupinga kuhusu elimu, bali wamepinga ufaulu kuwa amepata daraja gani kwa kuwa,  hiyo ni taarifa binafsina suala la daraja la ufaulu halihusiani kwenye kesi.

Wakili Katuga amedai kuwa, mshtakiwa amesema wazi kuwa ili mtu aajiriwe kuwa polisi lazima awe na elimu ya kidato cha nne na si ufaulu na kwamba ndio maana alipomuuliza kuhusu elimu ya  sekondari, kama amesoma, hawakupinga.

Wakili Katuga amedai kuwa, PGO zote alizozitaja mshtakiwa zinazungumzia elimu kwa jumla na si kiwango cha ufaulu.

Mahakama katika uamuzi wake imekubaliana na pingamizi la Serikali ikieleza swali la mshtakiwa kwa shahidi liishie kwenye kiwango cha elimu yake tu.

 “Hata PGO imezungumzia tu kiwango cha elimu na si zaidi ya hapo,” amesema Jaji Ndunguru katika uamuzi huo na Lissu akaendelea kumhoji shahidi maswali mbalimbali.