Mahakama yakubali Lissu kutumia  maelezo ya shahidi wa Jamhuri

‎‎Dar es Salaam.  Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Dar es Salaam, imeridhia ombi la Mwenyekiti wa Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kupokea maelezo ya maandishi ya shahidi wa pili wa Jamhuri kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wake katika kesi ya uhaini inayomkabili.

Mahakama hiyo imekubali kupokea maelezo hayo katika uamuzi wake uliotolewa leo, Jumatatu, Oktoba 13, 2025, baada ya kutupilia mbali pingamizi la Jamhuri.

Kesi  hiyo ya  inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, inaendelea kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri.

Ijumaa Oktoba 10, 2025, wakati akimhoji maswali ya dodoso shahidi huyo wa pili wa Jamhuri katika kesi hiyo, aliiomba Mahakama hiyo ipokee maelezo ya maandishi ya shahidi huyo yawe kielelezo cha upande wake.

Lissu aliomba Mahakama hiyo iyapokee maelezo hayo  ili ayatumie kuhoji kuaminika kwake kwa kuonesha kukinzana kwa maelezo hayo ya maandishi na ushahidi alioutoa kwa mdomo kizimbani chini ya kiapo.

Hata hivyo, aliwekewa pingamizi na waendesha mashtaka katika kesi hiyo wakidai kuwa, mshtakiwa huyo hakufuata utaratibu uliowekwa na sheria kwa mujibu wa kifungu cha 163 cha Sheria ya Ushahidi (TEA) na katika mashauri mbalimbali yaliyoamuliwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Kwa nyakati tofauti waendesha mashtaka, Mawakili wa Serikali Wakuu, Ajuaye Zegeli na Ignas Mwinuka wakidai kuwa zipo hatua tatu za kufuatwa.

Walibainisha kuwa, kwanza lazima shahidi asomewe maelezo hayo, pili lazima maeneo yanayokusudiwa kuhojiwa katika maelezo hayo yabainishwe kumfahamisha shahidi na tatu maelezo hayo lazima yapokewe mahakamani kama kielelezo.

Hivyo walidai kuwa, mshtakiwa alizingatia hatua ya kwanza na ya tatu tu na kwamba hakufuata hatua ya pili.

Lissu alipinga hoja za pingamizi hilo la Serikali akisisitiza kuwa, amefuata hatua zote kama zilivyoainishwa kwenye sheria na katika uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika shauri la Rufaa ya Lilian Jesus Fotes dhidi ya Jamhuri.

Mahakama katika uamuzi wake uliosomwa na Jaji Ndunguru imelikataa pingamizi hilo la Jamhuri ikisema kuwa, imejiridhisha kuwa mshtakiwa alifuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria na kesi rejea zilizorejewa na pande zote.

Jaji Ndunguru amesema kuwa, Mahakama imeangalia na kuzingatiwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa kifungu cha 163 cha TEA na  uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika mashauri ya Lilian Jesus Fotes, Shadrack Sospeter dhidi ya Jamhuri na shauri la Elias Leonard dhidi ya Jamhuri la mwaka 2023 lililoamriwa Mei 2025.

Amesema kuwa Mahakama pia imeangalia kile kilichofanywa na mshtakiwa Lissu  imebaini kuwa maelezo ya shahidi yalisomwa na mshtakiwa aliainisha maeneo 43 anayokusudia kumhoji shahidi kisha aliiomba Mahakama shahidi aweze kuyatoa mahakamani yapokewe kuwa kielelezo.

“Kwa kuzingatia nilichosema na kile kilichofanyika, Mahakama hii inaridhika kuwa taratibu zilifuatwa na hivyo pingamizi linakataliwa,” amesema Jaji Ndunguru.

Hivyo Mahakama hiyo imeyapokea maelezo hayo na kusajiliwa kama kielelezo cha kwanza cha upande wa utetezi, yaani upande wa Lissu (DE1).

Baada ya maelezo hayo kupokewa Lissu ameendelea kumhoji shahidi huyo wa pili wa Jamhuri akilinganisha maelezo yake hayo ya maandishi na maelezo aliyoyatoa kwa mdomo, kuonesha kuwa baadhi ya maneno aliyoyasema kwa mdomo kizimbani hayamo katika maelezo yake ya maandishi.

Katika maswali mengi shahidi huyo amekiri kuwa maneno aliyoyasema kwa mdomo kizimbani hayamo katika maelezo yake ya maandishi huku akijaribu kutoa ufafanuzi kuwa asingeweza kuandika kila jambo.

Hata hivyo  Lissu ameukataa ufafanuzi wake huo kuwa yeye hautaki na kwamba huo ufafanuzi atautoa atakapoulizwa na waendesha mashtaka maswali ya kusawazisha.

Shahidhi wa pili wa Jamhuri katika kesi hiyo ni Mkaguzi wa Polisi John Kaaya, kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni,  Dawati la Doria Mtandaoni, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Makao Makuu, Dar es Salaam.

Kwa uamuzi huo, leo Lissu ameshinda pingamizi hilo dhidi ya Jamhuri baada ya kushindwa katika pingamizi la aina hiyo awali.

Oktoba 7, 2025, wakati akimhoji maswali ya dodoso shahidi wa kwanza wa Jamhuri katika kesi hiyo, Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumm Dar es Salaam (DZCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) George  Bagyemu, Lissu aliwasilisha ombi kama hilo.

Lissu baada ya kumhoji shahidi huyo maswali machache kuhusiana na maelezo yake ya maandishi, alimuuliza  kama anakubali kuyatoa mahakamani ili yapokewe na kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wake (Lissu) na shahidi akakubali kisha Lissu akaiomba mahakama hiyo iyapokee.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulimuwekea pingamizi ukiiomba Mahakama isiyapokee kwa maelezo kuwa mshtakiwa huyo hakufuata utaratibu wa kisheria katika kuwasilisha maelezo ya shahidi kwa kusudi la kuyatumia kuhoji kuaminika kwake.

Mawakili wa Serikali Wakuu Ignas Mwinuka na Nassoro Katuga, waliirejesha Mahakama katika kifungu cha 163 na 173 vya TEA pamoja uamuzi wa mashauri ya Lilian Jesus Fotes, Shadrack Sospeter yote dhidi ya Jamhuri na  Jamhuri dhidi ya Mnawale Hamis Nyanda na wenzake tisa.

Lissu baada ya kusikiliza hoja za pingamizi alikubali pingamizi hilo kuwa kweli alikosea utaratibu.

Hivyo, aliiomba Mahakama aruhusiwe kurekebisha kasoro hiyo kwa kuanza upya kwa kufuata utaratibu huo lakini pia alipinga na waendesha mashtaka kuwa katika mazingira hayo kwa mujibu wa kifungu 131 cha TEA hana nafasi hiyo kwa kuwa, ni kifungu hicho kinamzuia kurekebisha makosa hayo.

Mahakama katika uamuzi wake ilikubaliana na hoja za pingamizi la Jamhuri  kuwa upande mmoja unapokiri kukosea, kuruhusu  kufanya marekebisho ni kukinzana na utaratibu ambao ulishawekwa  na Mahakama ya Rufani .

“Kwa hiyo  Mahakama inakubaliana na pingamizi hili, hivyo inaikataa nyaraka hii,” amesema Jaji Ndunguru, kisha Lissu akaendelea na maswali ya dodoso kwa shahidi huyo.

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali  kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,

Anadaiwa kuwa,  Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha maneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko… kwa hiyo tunaenda kukinukisha… sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”