MAWAZIRI WAIMWAGIA PONGEZI BENKI YA NMB KWA UTENDAJI WAKE

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera na Uratibu) Zanzibar, Hamza Hassan Juma, wameimwagia pongezi Benki ya NMB kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali kwa kutoa elimu ya kifedha kwa vijana ili kujikwamua kiuchumi.

Wameyasema hayo walipotembelea banda la NMB kwenye maadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea katika viwanja vya Soko la Uhindini jijini Mbeya.

“Mmekuwa na sapoti kubwa kwa Serikali kusaidia elimu ya kifedha kwa vijana. Vijana wengi kwa sasa wamejikwamua kiuchumi kutokana na elimu mnayotoa,” alisema Waziri Katambi.

Kwa upande wake, Waziri Hamza Hassan Juma amesema vijana wengi wa Kizanzibari wamejikita katika ujasiriamali kutokana na elimu ya kifedha inayotolewa na Benki ya NMB.

Akizungumza wakati akiwakaribisha mawaziri hao, Meneja Mahusiano Mwandamizi wa NMB, Josephine Kulwa, alisema benki hiyo imetumia fursa ya Wiki ya Vijana kutoa elimu ya kifedha, ambapo kwa sasa kuna akaunti maalumu inayowagusa wanafunzi wa vyuo vikuu, iitwayo Mwanachuo Account.

Amesema akaunti hii ni rafiki kwa vijana na wanachuo, ambapo wakifanya muamala kwa kutumia Mshiko Fasta, wanarudishiwa asilimia 30.