KOCHA Mkuu wa Mashujaa ya Kigoma, Salum Mayanga amefunguka namna timu yake imeyatumia mapumziko mafupi ya Ligi Kuu Bara kujipanga na mambo mawili kwenye kikosi chake.
Akizungumza na Mwanaspoti Mayanga amesema wakati huu wa mapumziko ya ligi kupisha mechi za Kimataifa za Kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), timu yake imeyatumia kujipanga na kuboresha safu yake ya ushambuliaji.
Mayanga ambaye ni kocha mkongwe, amesema licha ya timu yake kufunga mabao mawili kwenye mechi tatu tofauti, bado anataka kuona wanatengeneza na kutumia nafasi nyingi.

“Tulikuwa na mambo tunayarekebisha kwenye mapumziko haya, kwanza tulikuwa na kazi ya kufanya kuongeza uwezo wa kutengeneza nafasi, lakini pia kuzitumia,” amesema Mayanga.
“Tumekuwa tunafunga ni mchezo mmoja tu hatujapata bao kati ya mitatu, lakini huwezi kuridhika. Ili uwe na uhakika unatakiwa uwe na uwezo wa kutumia nafasi kuanzia mbili au zaidi.
Aidha, Mayanga aliongeza kuwa eneo jingine ni kwenye umakini katika safu yake ya ulinzi ambayo imeruhusu mabao mawili kwenye mechi zake tatu.
“Nataka pia kuwa imara kwenye ulinzi, kuna mechi hatukuruhusu bao na tulishinda lakini tunataka kuwa bora zaidi kwenye mechi zitakazoendelea.
Kocha huyo ameongeza kuwa baada ya mazoezi hayo watapima ubora wao kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Tanzania iliyotakiwa kuchezwa juzi.

Mashujaa kwenye mechi tatu imeshinda moja dhidi ya Mtibwa Sugar, kisha ikatoa sare ya 1-1 dhidi ya JKT Tanzania na kupoteza mbele ya Singida Black Stars.
Wanajeshi hao baada ya mchezo huo wa kirafiki dhidi ya JKT Tanzania watasafiri kuifuata Pamba Jiji kwa mchezo wao wa nne wa ligi utakaopigwa Oktoba 17 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.