Liwale. Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalim, amewataka wananchi wa Liwale, mkoani Lindi, kutokubali korosho yao ichezewe, akisisitiza kuwa ni zao lenye thamani kubwa si tu nchini bali pia duniani.
Mwalim ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Oktoba 13, 2025, katika mkutano wa kampeni wa chama hicho uliofanyika katika stendi ya Liwale mkoani Lindi.
Amesema kutokana na thamani ya korosho, ni dhahiri kuwa ni zao la gharama kubwa jambo linaloonesha kwamba watu wa Kusini walipaswa kuwa miongoni mwa matajiri hapa nchini endapo wangefaidika ipasavyo na kilimo hicho.
“Tujiulize, umeona wapi korosho zinauzwa Sh200? Ni zao lenye thamani kubwa, linaweza kuliwa kama tiba, kama mboga au kama kiburudisho, lakini haliliwi na masikini. Nikiwaangalia wananchi wa Kusini na hali zao, nawaonea huruma,” amesema Mwalim.
Amefafanua kuwa korosho ni zao linalothaminiwa hadi kwenye maeneo ya kifahari duniani, akitoa mfano kuwa hata kwenye ndege na katika mikutano mikubwa ya viongozi, hutolewa korosho badala ya karanga.
“Nenda Ikulu, hutapewa karanga bali korosho. Ukienda kwenye mataifa yenye maendeleo, utakutana na korosho ambazo ni za Liwale na Nchingwea, lakini cha kusikitisha ni kwamba wanaozilima wenyewe ni masikini wa kutupwa. Hii si sawa,” amesema.
Mwalimu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chaumma, amesema zao hilo linauzwa kwa bei ya juu zaidi duniani mara mbili au tatu ya mazao mengine, hivyo ni muhimu wananchi kuacha kuruhusu watu wachache kunufaika nalo.
Aidha, amewataka wananchi wa Liwale kutouza korosho zao kwa sasa hadi pale atakapoapishwa kuwa rais, akiahidi kuchukua hatua za kuongeza thamani ya zao hilo na kuhakikisha wakulima wananufaika ipasavyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chaumma, John Mrema amesema mbali na changamoto ya bei ya korosho, wananchi wa Liwale pia wanakabiliwa na tatizo la tembo wanaovamia makazi na kuharibu mazao yao.
Amesema chama hicho kina mpango wa kufunga nyaya za umeme zenye kengele mita 100 kutoka makazi ya watu ili kutoa tahadhari pindi tembo wanapokaribia vijiji, mfumo ambao alisema tayari umefanikiwa kutumika nchini Kenya.
“Suala hili halihitaji gharama kubwa, bali nia ya dhati ya kuwasaidia wananchi. Walioko madarakani wamekosa utashi wa kisiasa wa kulitatua tatizo hili,” amesema Mrema.
Ameongeza kuwa serikali yao itaunda mfumo wa tahadhari wa mapema kwa kushirikiana na askari wanyamapori ili kuzuia wananchi kuingilia maeneo ya ikolojia ya wanyama, pamoja na kuanzisha mfuko maalum wa fidia kwa wale wanaoharibiwa mashamba au kupoteza maisha kutokana na wanyama hao.
“Kilio cha tembo si cha Liwale pekee, kiko pia Kanda ya Ziwa na Kaskazini. Wote wanalia fidia. Chaumma tukiingia madarakani, tutahakikisha kila mkulima anayeharibiwa mazao analipwa stahiki zake kwa uwazi,” amesisitiza Mrema.
Awali, mgombea ubunge wa Liwale kupitia Chaumma, Mikidadi Abdallah alisema akichaguliwa atashughulikia changamoto za miundombinu, hasa barabara, ambazo zimekuwa kikwazo kwa maendeleo ya wananchi.
“Tuliahidiwa barabara bora, lakini mpaka leo hazipitiki. Wakati wa mvua, hali inakuwa mbaya zaidi. Watu wa Liwale hawawezi kupanda ndege, na bidhaa za Sh15,000 tunanunua Sh52,000 kwa sababu ya ubovu wa barabara. Hili halikubaliki,” amesema Abdallah.
Aidha, amegusia changamoto ya wananchi wanaoishi jirani na Hifadhi ya Selous, ambao wamekuwa wakikumbwa na mashambulizi ya tembo na kuharibiwa mazao yao, akisema kilimo kwao kimekuwa “kinachoumia mgongo badala ya kuwa uti wa mgongo.”