Dar es Salaam. Baada ya siku kadhaa za hekaheka za maandamano ya wananchi dhidi ya serikali ya Madagascar inaoongozwa na Rais Andry Rajoelina, ofisi ya Rais huyo imelaani kile ilichokiita jaribio la mapinduzi kinyume na sheria.
Katika maandamano hayo ambayo yanazidi kuongezeka kwa sasa, makundi ya wanajeshi yamejiunga tangu mwishoni mwa wiki katika mitaa ya Antananarivo, na kikosi cha jeshi la Madagascar kilitoa wito wa kukataliwa kwa amri ya kuwapiga risasi waandamanaji.
Maelfu ya raia wa Madagascar wamekuwa wakiandamana katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa zaidi ya wiki moja sasa, katika kile kinachoelezwa kuwa wimbi kubwa zaidi la maandamano kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa zaidi ya miaka 15.
Kilichoanza kama malalamiko dhidi ya upungufu wa bidhaa za msingi kimekuwa kwa kasi na kuwa changamoto kubwa kwa Rais Rajoelina ambaye yuko madarakani kwa mara ya pili tangu mwaka 2018.
Katika kuonyesha uwajibikaji, Rajoelina alivunja serikali yake kama njia ya kujibu hasira ya vijana wa Gen Z, lakini hatua hiyo haikuweza kuwatuliza wanaoshutumu serikali kushindwa kutimiza majukumu yake ya msingi ikiwemo umeme.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu wasiopungua 22 wamepoteza maisha na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika machafuko hayo, ingawa serikali ya Madagascar imekanusha idadi hiyo.
Kwa mujibu wa RFI Kiswahili na Al Jazeera, taarifa ya Ikulu ilipo Ofisi ya Rais Rajoelina, imekanusha taarifa ikishutumu vikali “jaribio la kunyakua mamlaka kinyume cha sheria na kwa nguvu” na kutoa wito kwa vikosi vya taifa kuungana kulinda utaratibu wa kikatiba.
Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku mbili tangu wanajeshi kutoka kikosi maalumu cha kijeshi cha CAPSAT kujiunga na waandamanaji vijana huku wakitoa ujumbe wa video wakidai kuwa wametwaa udhibiti wa vikosi vyote vya jeshi la Madagascar (nchi kavu, anga na baharini).
Ikumbukwe kwamba kikosi cha CAPSAT ndiyo kitengo cha kijeshi ambacho kiliwahi kumweka Rajoelina madarakani mwaka 2009.
Hata hivyo, haijabainika wazi ni kwa kiasi gani vitengo vingine vya jeshi vimefuata amri ya CAPSAT na haijathibitishwa rasmi kama kilichotokea ni mapinduzi ya kijeshi.
Nani anaandamana, kwa nini?
Maandamano hayo yalianza kama kampeni dhidi ya kukosekana kwa huduma za msingi na baadaye yakageuka kuwa wito wa kumwondoa Rais Rajoelina madarakani.
Maandamano yalianzishwa Septemba na kundi linalojiita Gen Z Madagascar kupinga uhaba wa umeme, maji, na kupanda kwa gharama za maisha.
Gen Z wanataka kwanza Rais Rajoelina ajiuzulu, mfumo wa Seneti uvunjwe, kukomesha upendeleo kwa wafanyabiashara wanaodhaniwa kuwa karibu na rais, kupinga ufisadi wa kimfumo, ubadhirifu wa fedha za umma na upendeleo wa kifamilia.
Rajoelina, mwenye umri wa miaka 51, alipata umaarufu mwaka 2009 kama meya wa Antananarivo baada ya kuongoza maandamano yaliyosababisha kupinduliwa kwa Rais Marc Ravalomanana kwa msaada wa jeshi.
Historia ya siasa: Madagascar, taifa la kisiwa lenye watu zaidi ya milioni 31 ambapo asilimia 80 wanaathiriwa na umaskini uliokithiri, lina historia ya matukio ya kisiasa ambapo viongozi wamelazimishwa kuondoka madarakani tangu ilipopata uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960.