Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo Othman Masoud Othman amesema akiingia madarakani atahakikisha anaondoa jeuri na kiburi cha baadhi ya watendaji wa Serikali wanaojifanya miungu watu.
Amedai kuwa kiburi na jeuri hizo za baadhi ya watendaji hao, zinasababisha Wazanzibari kukosa haki zao za msingi ikiwemo kupata maisha bora na ajira kwa vijana.
Othman ameeleza hayo leo Jumatatu Oktoba 13, 2025 akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Gombani ya Kale, Jimbo la Wawi kisiwani Pemba.
Mgombea huyo ameanza ziara ya kampeni Pemba ikiwa ni awamu ya tatu baada ya jana Jumapili Oktoba 12, 2025 kuhitimisha Unguja katika mwendelezo wa kusaka kura za kujihakikishia ushindi Oktoba 29, 2025.

“Chini ya urais wangu, ahadi yangu au ahadi yetu ACT ni kuondoa kiburi cha mtu kushika nafasi za Serikali na kujifanya yeye ndio kila kitu. Hii nchi sio ya mama au baba yake mtu, bali ni wananchi.
“Tutakwenda kukomesha hali kwa kuirudisha Zanzibar mikononi mwenu kupitia Katiba mpya mtakayoipitisha wananchi kupitia kura ya maoni,” amesema Othman.
Mbali na hilo, Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, amerejea ahadi ya kurejesha mali za Wazanzibari zilizochukuliwa kinyume cha utaratibu ikiwemo walioporwa ardhi zao.
“Waliokwapua mali za wananchi watazitapika, waliobeba fedha za umma kupitia miradi ya maendeleo, tutakwenda kufukua makaburi ili wazirejeshe,”
“Kura yako safari hii, huendi kuipigia ACT Wazalendo tu, bali kujiondoa katika dhuluma hizi. Mpeni Othman Masoud na wagombea wote wa ACT kuanzia madiwani, wawakilishi na wabunge,” amesema Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo (Bara), Omari Ali Shehe amesema kampeni za uchaguzi za chama hicho zinakwenda vizuri katika kisiwa hicho.
Shehe amesema kati ya mikutano ya hadhara ya kampeni 37 aliopangiwa kuifanya Othman, tayari amefanya 26, akisema kati ya majimbo 18 ya Pemba aliyopanga kuyafikia 11 ameshayafikia.
“Kwa Unguja kati ya majimbo 50, Othman ameshafikia 37, safari yetu inaendelea vizuri sana…Wazanzibari wametuitikia. Pia Wazanzibari wametuahidi kuwa Othman ndiye watakaomchagua Oktoba 29,” amesema Shehe.