Pingamizi La Jamhuri Latupiliwa Mbali Kesi Ya Tundu Lissu – Global Publishers



Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Dar es Salaam, imeridhia ombi la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kupokea maelezo ya maandishi ya shahidi wa pili wa Jamhuri kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wake katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Mahakama hiyo imekubali kupokea maelezo hayo katika uamuzi wake uliotolewa leo, Jumatatu, Oktoba 13, 2025, baada ya kutupilia mbali pingamizi la Jamhuri.

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, inaendelea kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri.
Ijumaa Oktoba 10, 2025, wakati akimhoji maswali ya dodoso shahidi huyo wa pili wa Jamhuri katika kesi hiyo, aliiomba Mahakama hiyo ipokee maelezo ya maandishi ya shahidi huyo yawe kielelezo cha upande wake.

Lissu aliomba Mahakama hiyo iyapokee maelezo hayo ili ayatumie kuhoji kuaminika kwake kwa kuonesha kukinzana kwa maelezo hayo ya maandishi na ushahidi alioutoa kwa mdomo kizimbani chini ya kiapo.

Hata hivyo, aliwekewa pingamizi na waendesha mashtaka katika kesi hiyo wakidai kuwa, mshtakiwa huyo hakufuata utaratibu uliowekwa na sheria kwa mujibu wa kifungu cha 163 cha Sheria ya Ushahidi (TEA) na katika mashauri mbalimbali yaliyoamuliwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.