Rais wa Madagascar atimkia Ufaransa maandamano yakipamba moto

Dar es Salaam. Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina ameripotiwa kukimbilia Ufaransa baada ya mfululizo wa maandamano ya wananchi wake yaliyodumu kwa takribani wiki mbili sasa, yakiongozwa na vijana wa kizazi cha Gen Z nchini humo.

Kwa mujibu wa duru za kimataifa, maandamano hayo yamekuwa yakilalamikia ufisadi, umasikini na huduma duni za kijamii ambapo taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa hali ya maandamano imekuwa ya kutisha zaidi leo kufuatia shinikizo la wanajeshi walioungana na waandamanaji katika mji mkuu wa Antananarivo, kuongeza shinikizo kwa serikali.

Rais Rajoelina leo Jumatatu Oktoba 13, 2025, ameondoka kwa ndege ya kijeshi ya Ufaransa baada ya kufikia makubaliano ya kisiasa na Rais Emmanuel Macron.

Hata hivyo, hakuna tamko rasmi lililotolewa na ikulu ya nchi hiyo kufuatia kuondoka kwa Rais huyo huku vyombo vya habari nchini humo vikiripoti kuwa huenda kuondoka kwake ni kwa muda, huku mazungumzo ya kupata uongozi wa mpito yakiendelea.

Maelfu ya raia wa Madagascar wamekuwa wakiandamana katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa zaidi ya wiki moja sasa kwa kile kinachoelezwa kuwa wimbi kubwa zaidi la maandamano kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa zaidi ya miaka 15.

Kilichoanza kama malalamiko dhidi ya upungufu wa bidhaa za msingi kimekua kwa kasi na kuwa changamoto kubwa kwa Rais Rajoelina ambaye yuko madarakani kwa mara ya pili tangu mwaka 2018.

Shinikizo lilianza kuongezeka kufuatia kukamatwa kwa wanasiasa wawili mashuhuri wa Antananarivo Septemba 19, 2025, waliokuwa wamepanga kufanya maandamano ya amani kupinga matatizo sugu ya ukosefu wa umeme na maji.

Mashirika ya kiraia yalijiunga na harakati hizo na kundi la vijana mtandaoni lijulikanalo kama Gen Z Mada likaibuka kuwa mstari wa mbele.

Katika juhudi za kurejesha amani nchini humo, wiki iliyopita, Rajoelina alivunja serikali yake kama njia ya kujibu hasira za Gen Z hao, hata hivyo hatua hiyo haikufanikiwa kuwatuliza waandamanaji hao.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu wasiopungua 22 wamepoteza maisha na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika machafuko hayo huku serikali ya Madagascar ikikanusha takwimu hizo na kuzitaja kuwa ni uvumi na kuripoti kuwa ni vifo 12 tu vilivyothibitishwa, na wote waliouawa walikuwa wahalifu waliotumia mwanya wa maandamano hayo.

Kuhusu madai ya maandamano hayo, inadaiwa yamebadili sura kutoka kuwa malalamiko ya huduma duni hadi kuwa wito wa mabadiliko ya kisiasa ambapo vijana wengi wanaokumbwa na ukosefu wa ajira za kudumu na mishahara midogo, wakitaka Rais Rajoelina ajiuzulu, wakimlaumu kwa matatizo yanayowakabili.

Madagascar ni moja ya nchi maskini zaidi duniani, ambapo asilimia 75 ya watu wanaishi chini ya mstari wa umaskini, kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB).

Msemaji wa Rais, Lova Ranoromaro, ameandika kwenye mitandao ya kijamii: “Hatutaki mapinduzi ya kijeshi, kwa sababu mapinduzi huharibu taifa letu, na huharibu maisha ya watoto wetu.”

Madagascar imeshuhudia maasi kadhaa tangu ilipopata uhuru mwaka 1960, ikiwemo maandamano ya mwaka 2009 yaliyomlazimu Rais wa zamani, Marc Ravalomanana kujiuzulu na kumuingiza madarakani Rajoelina kwa mara ya kwanza.