Geita. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kwamba endapo atapata ridhaa ya kuongoza kwa kipindi cha pili, Serikali yake itatoa mitaji kwa wachimbaji wadogo ili kuwakuza wawe wakubwa sambamba na kupima maeneo ya wafugaji kutoka ekari milioni 3.4 ya sasa, hadi milioni sita na kuzimilikisha kwa wafugaji kote nchini.
Samia amesema kitaifa pia, Serikali yake imejipanga kukuza sekta ya viwanda kutoka ukuaji wa asilimia 4.8 kwa sasa, hadi asilimia tisa ifikapo mwaka 2030.
Katika Mkoa wa Geita, mgombea huyo ameahidi ujenzi wa Uwanja wa Ndege Geita Mjini pamoja na maboresho ya uwanja wa ndege wa Chato na ujenzi wa machinjio matatu ya kisasa.

Ahadi nyingine kwa Geita ni ujenzi wa tawi la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), maabara ya kisasa kwa ajili ya wachimbaji madini, viwanda vya kuchakata mbegu za alizeti pamoja na viwanda vya kusindika matunda.
Samia ametoa ahadi hizo leo Jumatatu Oktoba 13, 2025 katika maeneo ya Nyawilimilwa na Geita Mjini, akinadi sera na ilani ya CCM ya 2025/2030 katika mwendelezo wa kampeni zake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kuhusu matumizi endelevu ya ardhi nchini, amesema wanakwenda kuangalia changamoto zinazokabili kwenye sekta hiyo kwa maeneo mbalimbali ikiwemo wakulima, wafugaji, hifadhi na watumiaji wengine wa ardhi lengo likiwa ni kumilikisha ardhi.
“Ilani ya 2025/30 inatutaka kupima kitaifa maeneo ya wafugaji pia kutoka hekari milioni 3.4 ya sasa hadi kufikia milioni sita na tutazimilikisha kwa wafugaji. Tunakwenda kupima maeneo ya miji, makazi na matumizi mengine kwa ajili ya uwekezaji,” amesema.
Akizungumzia Mkoa wa Geita, Samia amesema umezidi kuimarika kiuchumi kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini, kilimo na ufugaji.
Mgombea huyo amesema kuwa mkoa huo kuanzia na sekta ya ufugaji ameahidi watajenga machinjio matatu ya kisasa katika maeneo ya Nyawilimilwa, Nzera na Kakubilo pamoja ujenzi wa viwanda vya kuchakata mbegu za alizeti na vya kusindika matunda ili kukuza biashara na uchumi eneo hilo.
Kuhusu sekta ya afya, ameahidi Serikali yake itaendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa sasa na kuwa za kibingwa na kibobezi zitatolewa.
“Kwa upande wa tawi la JKCI, litajengwa Geita ili matibabu ya moyo yafanyike hapa na mikoa ya jirani na nchi jirani zitafuata matibabu hayo hapa. Tutaboresha hospitali ya wilaya kwa ujenzi wa jengo la upasuaji, chumba cha kuhifadhia maiti na zahanati 12,” amesema.
Katika sekta ya usafiri na usafirishaji, amesema ilani imewataka kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara, kuboresha uwanja wa ndege Chato na kujenga uwanja mpya hapa Geita Mjini,” amesema.
Samia ametaja ahadi nyingine kuwa ni kujenga majengo ya kudumu katika uwanja wa EPZA Bombambili ili yatumike wakati wa maonyesho na mikutano ya kimataifa ya madini.

Kwenye sekta ya kilimo, mgombea huyo ameahidi matrekta 10,000 yatakayosambazwa kote nchini na mikopo, kuuzwa kwa atakayeweza kununua pamoja na wakulima kulimiwa kwa nusu bei na kuendelea kutoa ruzuku ya chanjo kwa mifugo.
“Kwa upande wa wafugaji, katika miaka mitano ijayo tutaendelea kugawa ruzuku ya chanjo ili mifugo iwe salama na tumejitahidi kujenga majosho, mabwawa, pia, machinjio yenye hali nzuri ili kuweka afya za watumiaji wa nyama zinazochinjwa kwenye maeneo hayo,” ameongeza.
Awali, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (Femata), John Bina amesema wachimbaji wa madini ya aina zote nchini watamchagua Samia kwa sababu ameweka mazingira rafiki na wezeshi ya wao kutekeleza majukumu yao.
Ametaja miongoni mwa changamoto zilizokuwa zikiwakabili ni pamoja na kodi kero ambazo zimepunguzwa na kwa sasa wachimbaji wameondokana na adha hiyo.
“Wachimbaji wa madini aina zote nchini watakuchagua kwa sababu umewaheshimisha, zamani familia ziliamini anayechimba madini amepotea, lakini sasa ni tofauti na wameniambia nikuambie lazima tukulinde kwa wivu mkubwa kwa sababu umefanya mengi, tutakulinda kama tunavyolinda madini,” amesema.