SAMIA KUWATUMA UPYA MAWAZIRI WA KISEKTA CHATO KUSINI

……………..

CHATO

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwatuma upya mawaziri wa kisekta ili kutoa mrejesho wa mgogoro wa mpaka kati ya Msitu wa hifadhi ya Biharamulo kwenye shamba la miti Silayo dhidi ya wananchi wa Jimbo la Chato Kusini.

Amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania katika Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2025, atahakikisha anawatuma tena mawaziri wake ili kuja kutatua mgogoro huo.

Amelazimika kutoa majibu hayo kwenye mkutano wa kampeni wilayani Chato mkoani Geita baada ya Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula, kumwomba asaidie kutatua mgogoro huo ambao umesababisha baadhi ya wananchi wa Jimbo hilo kukosa maeneo ya kulima na shughuli zingine za kibinadamu.

“Mheshimiwa mgombea na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wa Jimbo la Chato kusini wanakupenda sana, lakini pia wameniagiza nifikishe maombi yao kuhusiana na mpaka wa hifadhi wa shamba la Silayo na wananchi, wanaomba wapewe eneo ili walime”.

“Hata hivyo wanakushukuru sana kwa kuwapa Jimbo jipya la Chato kusini, Jimbo lenye utajiri wa dhahabu tunakushukuru sana mama” amesema Lutandula.

Aidha Lutandula amewomba Dkt. Samia  atakapo chaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, akipandishe hadhi kituo cha afya Bwanga na kuwa Hospitali ya wilaya ikiwa ni pamoja na mji wa Bwanga na Buseresere kupewa kipaumbele cha kuzifungua barabara za mitaa na zilizopo kufanyiwa ukarabati.

“Tunaomba sana barabara za mitaa kwenye mji wa Bwanga na Buseresere zitengenezwe ili angalau na sisi wananchi wa Chato Kusini tuwe tunaruka na kujidai kidogo katika mitaa yetu” amesema.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Samia akakubaliana na maombi hayo kwa madai ameyachukua ili kuona namna ya utekelezaji wake hali iliyosababisha wananchi wengi waliojitokeza kumsikiliza kumshangilia kwa shangwe na nderemo.

Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kukuamini Chama Cha Mapinduzi kwa kukipigia kura nyingi kutokana na dira na nia thabiti ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Awali aliyekuwa Katibu mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Bashuru Ally Kakurwa, akawakumbusha watanzania umuhimu wa kutunza amani ya nchi na kujiepusha na watu wenye nia ya kuwagawanya kisasa,kikanda na kikabila.

Kadhalika amemwombea kura nyingi za Urais gombea wa CCM Dkt. Samia huku akidai kuwa kumchagua mgombea huyo ni kuiweka nchi katika mikono salama.

Itakumbukwa kuwa mchakato wa kuligawa Jimbo jipya la Chato kusini liliibuliwa na diwani wa kata ya Bwera, Josephat Manyenye kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Chato, hoja iliyoungwa mkono kwa aslimia 100 kisha taratibu zingine kuendelea mpaka hapo Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) ilipoamua kuligawanya na kuwa na majimbo mawili ya Chato Kusini na Kaskazini.

                           Mwisho.