Sintofahamu INEC ikiwaengua madiwani saba

Dar/mikoani. Kwa nini uamuzi huu sasa…? Ni swali wanalohoji wachambuzi wa masuala ya siasa na wagombea udiwani katika baadhi ya kata ambazo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewaengua na kufuta kata zingine 10.

Ukiwa ni uamuzi uliofanyika wiki mbili kabla ya uchaguzi Oktoba 29,2025  baadhi ya madiwani wameupokea uamuzi wakidai huenda kata zao hazikuwa zimerasimishwa.

Taarifa ya INEC iliyotolewa Oktoba 12, 2025, ikisainiwa na Mwenyekiti wake INEC, Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele, uamuzi huo umefikiwa baada ya tangazo la Serikali Na. 596 na Na. 600 la Oktoba 3, 2025.

Katika tangazo hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) alitangaza marekebisho ya mipaka ya maeneo ya utawala na kufuta kata kadhaa.

Kwa mujibu wa INEC, kata zilizofutwa ni Litapunga, Kanoge, Katumba, Mishamo, Ilangu, Bulamata, Ipwaga, Milambo, Igombemkulu na Kanindo.

Aidha, tume imetengua uteuzi na kuwaondoa katika orodha ya wagombea udiwani saba walioteuliwa katika kata husika ambao wote kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwemo Salehe Mrisho Msompola (Kata; Kanoge), Elius Wilson Elia (Kata: Katumba).

Wengine ni Mohamed Ally Asenga (Kata: Litapunga), Nicas Athanas Nibengo (Bulamata), Sadick Augostino Mathew (Ilangu), Rehani Simba Sokota (Ipwaga) na Juma Mohamed Kansimba (Mishamo).

Mchambuzi wa Masuala ya siasa, Prince Mwahijo amesema uamuzi wa INEC haukupaswa kuletwa sasa kwani tayari wagombea walishajipanga hivyo uamuzi huo unaibua maswali.

“Kwa nini uamuzi huu sasa….? madiwani wameathirika kwa sababu walishaanza kampeni sasa kilichofanyika ni kukoleza hali ya watu kukata tamaa kwenda kupiga kura kwenye uchaguzi, wanajenga mazingira ya watu kuendelea kuchanganyikiwa wakati huu wa uchaguzi,” amesema.

 Ameshauri kila hoja zinazoibuliwa na wananchi zijibiwe badala ya kuwapuuza.

Naye mchambuzi wa siasa na jamii, Kiama Mwaimu amehoji sababu za kufutwa sasa kwa kata hizo wakati tayari wagombea walishajipanga.

 “Kulikuwa na athari endapo wangefuta kata hizo baada ya miaka mikutano ijayo, kwa nini wafute sasa ….taarifa za kufuta hizi kata zilikuwepo na kuachwa hadi wiki mbili kabla ya uchaguzi,” amesema.

Mwaimu amesema uamuzi huo utakuwa umewaumiza madiwani, kwani watakuwa wamepoteza muda na fedha wakati wa kampeni na huku wananchi wakibaki na majeraha.

Kwa upande wake mkazi wa Nsimbo mkoani Ktaviu Joseph Mandi amesema kilichofanyika na wao hawafahamu bali wameona taarifa ya kutolewa kwa agizo hilo.

“Tumeshangazwa na uamuzi huu hutuna majibu ya nini kimetokea, lakini kata zilizofutwa ili uzifikie lazima uombee kibali hata ikitokea shida lakini kwa nini uamuzi huu sasa.”

Aliyekuwa mgombea udiwani kata ya Kanoge, Mohamed Asenga amesema amepokea kwa masikitiko taarifa hiyo akieleza kuwa haelewi msimamo wa INEC wanachoenda kufanya.

Amesema pamoja na yote, lakini bado hajapokea barua kutoka tume, akieleza kuwa ametumia gharama na muda mwingi kutafuta nafasi hiyo.

“Mchakato ulifanyika kuanzia kura za maoni, fomu zikatoka, kituo cha kura kikatengwa yote hayo INEC inashiriki, lakini ghafla na dakika za mwisho zinatoka taarifa hizo zenye kuumiza.”

“Tumetumia gharama kubwa ambazo kwa namna nyingine zingeweza kusaidia hata ada kwa watoto shuleni, sasa sijajua kama INEC watarejesha gharama zangu au vipi, binafsi ninasikitika sana” amesema Asenga.

Naye aliyekuwa mgombea udiwani Kata ya Katumba, Elius Eliah amesema amepokea vizuri maamuzi hayo na maelezo ya INEC yamejitosheleza na sasa anasubiri maelekezo mengine ya chama chake (CCM) na Serikali.

Amesema ni wazi Kata hiyo huenda haikuwa imerasimishwa kwa kuwa eneo lake lilikuwa tengefu kwa kambi ya wakimbizi kama ilivyofafanuliwa vyema na Tume, hivyo anaamini Serikali itafanya uamuzi mwingine ikishajiridhisha.

Kwa upande wake Saleh Msompole aliyekuwa mgombea Kata ya Kanoge, amesema anaheshimu maamuzi na maelekezo ya INEC hivyo yeye kama mpiga kura ataangalia kituo atakachoweza kupiga kura Oktoba 29.

“Binafsi naheshimu sana mamlaka na kwa kuwa sheria imesema hivyo kupitia viongozi wetu wa Serikali chini ya Waziri mwenye dhamana, nimepokea vyema maamuzi.”

“INEC imetaja vituo ambavyo vimetengwa hivyo mimi kama mpiga kura nitachagua sehemu mojawapo ya kutimiza haki yangu kikatiba, niwaombe pia wananchi wangu tupokee mabadiliko hayo” amesema Msompole.

Kufuatia uamuzi huo INEC imesema, kufutwa kwa kata hizo kumelazimu kuondoa vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwa kwenye kata zilizofutwa.

“Tume imeanzisha vituo vipya 292 vya kupigia kura katika kata jirani na kata zilizofutwa kuwawezesha wapiga kura kutoka katika maeneo yaliyofutwa,” imesema INEC.

Ikieleza zaidi INEC imesema wapiga kura 106, 288 waliokuwa kwenye vituo vilivyofutwa wamehamishiwa kwenye vituo 292 vya kupigia kura vilivyoanzishwa kwenye Kata za Mtapenda, Uruwira, Nsimbo, na Ugala zilizopo Halmashauri ya wilaya ya Nsimbo mkoa wa Katavi.

“Kata nyingine walizohamishiwa ni Sasu, Ilege, Uyowa, Makingi na Silambo zilizopo Halmashauri ya wilaya ya Kaliua mkoa wa Tabora na Kata ya Tongwe iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Katavi,” imesema taarifa hiyo,

Tume hiyo imetoa wito kwa wananchi kuzingatia mabadiliko haya ya maeneo ya uchaguzi ili waweze kutumia haki yao ya msingi kushiriki kupiga kura siku ya uchaguzi.