MSHAMBULIAJI wa Fountain Gate, Joshua Ibrahim, amesema baada ya kutoonekana tangu msimu huu umeanza kutokana na matatizo mbalimbali, kwa sasa mashabiki wake watarajie mambo mazuri, kwa sababu amejipanga vizuri ili kuendeleza kiwango chake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Joshua amesema baada ya majeraha mbalimbali aliyopitia, kwa sasa yupo fiti kukitumikia kikosi hicho kwa mechi zijazo, licha ya kukiri ushindani utakuwa ni mkubwa kutokana na aina ya wachezaji wazuri walio kikosini.
“Kwa msimu uliopita Fountain ilikuwa katika hali ya presha ya kushuka daraja, hivyo, tunahitaji kuondoa hilo lisijirudie tena, pia nahitaji kufunga zaidi mabao kwa sababu ndio kazi yangu iliyonileta hapa kama mshambuliaji,” amesema Joshua.
Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’, amesema ubora wa nyota huyo utaongeza sana ubunifu katika eneo la ushambuliaji la timu hiyo kwa kushirikiana na wenzake, ambao wamejumuika kikosini baada ya kuukosa mwanzo wa msimu kutokana na kukosa vibali na kuilazimu timu hiyo kucheza mechi tatu za awali na kupoteza zote ikiwa na kikosi cha wachezaji 14 tu.
Mechi za Ligi Kuu Bara ilizopoteza zote, ni bao 1-0, dhidi ya Mbeya City, Sept 18, 2025, ikachapwa 3-0 na Simba, Sept.25, 2025, kisha, 2-0 na Mtibwa Sugar, Sept28.

Joshua amejiunga na Fountain baada ya kuondoka Namungo aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari 2025, akitokea KenGold ya Mbeya ambayo imeshuka daraja kwa msimu wa 2024-25, ikitokea Ligi Kuu hadi Championship.
Alijiunga na KenGold Agosti 2024, akitokea Tusker FC ya Kenya ambako hadi anaondoka dirisha dogo, aliifungia timu hiyo mabao manne ya Ligi Kuu, huku kwa upande wa Namungo aliyoichezea kwa miezi sita akiifungia bao moja.
Mechi ya kwanza kwa nyota huyo kucheza itakuwa dhidi ya Dodoma Jiji, Oktoba 17, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati, Manyara, huku kikosi hicho kikipambana kurejesha furaha kwa mashabiki kutokana na kuanza vibaya msimu huu.