Tanzania Yashiriki Kongamano la Afya Duniani Jijini Berlin – Global Publishers



Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bw. Ismail Rumatila unashiriki Kongamano la Afya la Dunia linalofanyika kwa siku tatu jijini Berlin, Ujerumani kuanzia Oktoba 12 hadi 14, 2025.

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani. Mhe. Hassani Mwamweta anashiriki kongamano hilo linalofanyika chini ya kaulimbiu “Kuchukua Jukumu la Afya katika Ulimwengu unaogawanyika” (Taking Responsibility for Health in a Fragramenting World) limekusanya watu wa kada mbalimbali duniani wakiwemo viongozi wa Serikali, Taasisi za Kimataifa; Asasi za Kiraia; sekta binafsi; wataalam wa Afya; watafiti; wanasayansi; wanaharakati kujadili namna ya kupata ufumbuzi wa changamoto za kiafya zinazoikabili dunia.

 

Washiriki katika siku ya ufunguzi walijadili mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi katika sekta ya afya,; Umuhimu wa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, moyo, figo na kansa ambayo yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa idadi ya vifo duniani.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya duniani kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Janabi alikuwa mmoja wa wachangia mada hizo zilizokuwa zikiendeshwa kwa utaratibu wa panel.

Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imekuwa ikishiriki majukwaa kama haya kwa lengo sio tu la kupata wadau wakushirikiana nao kuimarisha sekta ya afya nchini, bali pia kujiimarisha kidiplomasia katika anga za kimataifa.