‎TFS yaanza kutumia teknolojia kubaini moto kabla haujasambaa

Iringa. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia shamba la miti la Sao Hill, umeingia katika zama mpya za kidijitali kwa kutumia teknolojia bunifu za kisasa kudhibiti moto misituni, hatua inayotajwa kubadilisha kwa kiasi kikubwa mfumo wa usimamizi na ulinzi wa misitu nchini.

‎Teknolojia hizo zinazohusisha mifumo ya utambuzi wa mapema, ramani za satelaiti, sensa za joto na mifumo ya taarifa kwa wakati halisi (real-time alerts), zimeongeza uwezo wa TFS kugundua matukio ya moto kabla hayajasambaa na hivyo kupunguza uharibifu wa misitu na kupotea kwa miti.

‎Akizungumza na Mwananchi Oktoba 13, 2025, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS Sao Hill, Mussa Kitivo amesema teknolojia hiyo imekuwa suluhisho muhimu katika kudhibiti matukio ya moto ambayo awali yalikuwa yakisababisha uharibifu wa rasilimali.

‎“Kwa sasa tunapata taarifa mapema zaidi kupitia mifumo ya satelaiti na sensa, moto unadhibitiwa kabla haujasambaa na hii imepunguza sana uharibifu wa hekta za misitu na kuokoa miti mingi ambayo ingepotea,” amesema Kitivo.

‎Kitivo amefafanua kuwa TFS imeendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wake na wananchi juu ya matumizi ya teknolojia hizo na uchambuzi wa taarifa ili kuongeza ufanisi wa kazi za ulinzi wa misitu.

Mtaalamu wa mifumo ya kidigitali, Bashily  Msangi  na Mhifadhi Mwandamizi wa TFS–Sao Hill, Mussa Kitivo wakizungumza na Wananchi wa vijiji jirani vinavyozunguka shamba la miti Sao Hill Wilayani Mufindi huku wakiwaeleza  matumizi sahihi ya teknolojia ya kidigitali ya mfumo wa taarifa kwa wakati ili kudhibiti moto misituni.

‎Kwa mujibu wa taarifa za TFS, mfumo huo umeundwa kusaidia watendaji wake na wananchi wanaoishi karibu na misitu kutoa taarifa kwa haraka kupitia njia za kidijitali kama simu janja, programu maalumu za taarifa na mitandao ya mawasiliano ya dharura.

‎Kwa upande wake, mtaalamu wa mifumo ya kidijitali, Bashily Msangi amesema teknolojia hiyo si tu inarahisisha kugundua moto, bali pia inasaidia kufuatilia na kutambua chanzo cha moto, ikiwemo watu au shughuli zilizochangia tukio.

‎“Teknolojia hizi zinatupa taarifa sahihi, ikiwemo eneo lililoathirika, kasi ya moto na hali ya upepo na hii inarahisisha kupanga mikakati ya haraka ya kudhibiti moto,” amesema Msangi.

‎Aidha, TFS–Sao Hill imeanza kuhusisha wananchi kupitia mfumo wa taarifa za kijamii unaowawezesha kuripoti dalili za moto au shughuli hatarishi kwa kutumia simu zao.

‎Kwa mujibu wa TFS, hatua hii ni sehemu ya mpango wa kidijitali wa kitaifa wa kuboresha usimamizi wa misitu, sambamba na jitihada za Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.

‎Kupitia mfumo huo, Sao Hill imeweza kupunguza zaidi ya asilimia 60 ya matukio ya moto yaliyokuwa yakiripotiwa kila mwaka huku ushirikiano kati ya watumishi na jamii ukiongezeka maradufu.

‎TFS pia imetangaza mpango wa kupanua teknolojia hiyo katika mashamba mengine ya miti nchini, ikiwemo Mufindi, Njombe na Kilombero ikiwa ni sehemu ya ajenda ya kitaifa ya matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.