Dar es Salaam. Wakati Taifa linapoadhimisha kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuwekeza katika watu na maendeleo endelevu kupitia safari ya baiskeli inayounganisha Watanzania kwa dhana ya umoja, huduma na matumaini.
Kwa mwaka wa tatu mfululizo, Vodacom imekuwa mdau mkuu wa safari maarufu ya Twende Butiama Cycling Tour, ambayo imekua kutoka wazo dogo la kumuenzi Mwalimu Nyerere hadi kuwa jukwaa la kitaifa la ujumuishwaji, afya, elimu na uhifadhi wa mazingira.
“Ni heshima kubwa kwa Vodacom Tanzania kuunga mkono Twende Butiama Cycling Tour kwa mwaka wa tatu mfululizo. Safari hii inaakisi roho ya umoja, ustahimilivu na dhamira ya kitaifa. Ilichokuwa mbio za kumbukumbu sasa ni harakati ya matumaini kwa maelfu ya Watanzania,” anasema Philip Besiimire, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania.
Mwaka huu pekee, jumla ya wapanda baiskeli 316 walishiriki, wakiwemo 207 waliopanda nchi nzima na 109 walioungana kwa njia ya mtandao kutoka nchi 19. Miongoni mwao, walikuwapo wanawake 36 na vijana 23 wenye umri chini ya miaka 25. Kwa pamoja, walipiga zaidi ya kilomita 1,500 wakipitia mikoa 11 nchini.
Kila mzunguko wa gurudumu ulisimama kama ishara ya mshikamano na matumaini mapya kwa taifa, kwani kupitia harakati hii, zaidi ya Watanzania milioni 2.46 walifikiwa na elimu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs).
Wanafunzi 15,650 wamenufaika kwa mazingira bora ya kujifunzia na vifaa saidizi, huku miti 80,000 ikipandwa kurejesha uhai wa Msitu wa Kahe ulioko katika nyayo za Mlima Kilimanjaro.
“Takwimu hizi si namba tu, ni kipimo cha ushirikiano, uwajibikaji na matokeo halisi ya dhamira yetu ya pamoja. Tunapoadhimisha miaka 25 ya Vodacom Tanzania, Twende Butiama inasimama kama kielelezo hai cha malengo yetu kuwawezesha watu, kulinda sayari na kudumisha imani,” anasema Besiimire.
Kwa Besiimire, Twende Butiama si tu tukio la michezo, bali ni wito wa kuchukua hatua kujenga Tanzania yenye afya, elimu bora na ustawi endelevu, na ndiyo maana kampuni hiyo inajitahidi kugusa maisha halisi ya watu.
Katika tukio hilo mwaka huu, Vodacom iliungana na washirika wake— Stanbic Bank Tanzania, Afroil Tanzania, ABC Impact, ABC Bicycles, Youth of United Nations (YUNA) Tanzania Chapter, Butiama Tourism and Conservation, Cycling Lovers Club na Darvelo Cycling Club kuhakikisha safari hii inaendelea kufika mbali zaidi.
Kwa pamoja, wanajenga urithi wa maendeleo kwa njia ya vitendo, kijiji kwa kijiji, mti kwa mti, na kilomita kwa kilomita.
Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania, Manzi Rwegasira, anasema ushiriki wao katika mpango huu ni sehemu ya kutimiza falsafa ya benki hiyo ya ukuaji shirikishi.
“Twende Butiama si tukio la baiskeli pekee, ni alama ya umoja, utumishi na uwajibikaji wa pamoja,” anasema Rwegasira na kuongeza; “Kila kilomita inayopigwa inaleta Tanzania karibu zaidi na maendeleo.”
Mwaka huu, Stanbic Bank inaadhimisha miaka 30 ya kuhudumia Watanzania, huku Vodacom ikitimiza miaka 25 ya kuunganisha taifa. Kwao, hii si tu sherehe, bali ni kumbukumbu ya watu na jamii zilizoifanya safari yao iwe na maana.
“Kuunga mkono Twende Butiama ni namna tunavyogeuza maadhimisho kuwa hatua.
“Tunaamini ukuaji lazima uwe wa pamoja. Ndiyo maana sehemu ya faida zetu huwekezwa kwenye elimu, afya na mazingira maeneo yanayoakisi maadili yetu,” anasema.
Mkurugenzi wa Mahusiano ya Nje wa Vodacom Tanzania, Zuweina Farah, anasema kwa mtazamo wa Vodacom, maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanafanikiwa pale ambapo Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kijamii na wananchi wanashirikiana kwa malengo ya pamoja kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
“Dunia ya maendeleo ni kama mashua inayosafiri baharini. Ili isonge mbele, kila abiria lazima achukue kasia na kushirikiana. Twende Butiama ni mfano wa mashua hiyo, inayobeba madaktari, walimu, vijana, wanamichezo na wanajamii wanaoendesha mabadiliko halisi,” anasema Farah, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Vodacom Foundation.
Farah anaeleza kuwa katika safari hiyo, wananchi hupata huduma za afya bure, watoto wenye ulemavu hupatiwa vifaa vya kujifunzia, na jamii huungana katika shughuli za upandaji miti ili kurejesha uhai wa mazingira.