Klabu ya Yanga, imemtangaza Patrick Mabedi raia wa Malawi kuwa kocha msaidizi wa kikosi hicho kinachoongozwa na Mjerumani, Romain Folz.
Mabedi amejiunga na Yanga kuchukua nafasi ya kocha Manu Rodriguez, aliyewasilisha barua ya kuomba kuvunja mkataba wake baada ya kupata changamoto ya afya.
Kocha huyo mwenye heshima kubwa nchini Malawi alipohudumu kama Kocha Mkuu wa Taifa hilo kuanzia mwaka 2023 hadi 2025, tayari amejiunga na Yanga leo Oktoba 13, 2025 na kuanza moja kwa moja mazoezi chini ya Folz, kwa ajili ya maandalizi kuelekea Malawi kwenye mechi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Striker hatua ya pili.
Mabedi ana leseni daraja A ya Ukocha ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambayo inamfanya akidhi pia Kocha Mkuu wa timu katika mashindano ya ndani na nje ya Tanzania.
Kocha huyo ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika ambao ameupata akiwa mchezaji na pia kocha.
Amecheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini ambako kuanzia 1998 hadi 2006 alikuwa Kaizer Chiefs ambako aliongoza kikosi kama nahodha na kuanzia 2006 hadi 2008 aliitumikia Moroka Swallows.
Kabla ya hapo aliitumikia Bata Bullets ya Malawi kwa muda wa miaka tisa kuanzia 1989 hadi 1998 alipopata fursa ya kujiunga na Kaizer Chiefs.
Mabedi anakuwa Kocha wa pili raia wa Malawi kuinoa Yanga akifuata nyayo za Marehemu Jack Chamangwana ambaye aliwahi kuitumikia timu hiyo na miaka ya nyuma na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2005 na 2006.
Ni kama Yanga imepiga ndege wawili kwa jiwe moja kwani imemchukua Mabedi muda mfupi kabla ya kukabiliana na Silver Striker ya Malawi katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Uzoefu wa Mabedi kwa soka la Malawi na wachezaji wake unaweza kuwa faida kwa Yanga katika mechi zake mbili baina ya timu hiyo.
Moja ya kauli ya Mabedi aliyowahi kuitoa ni: “Daima jaribu kutumia kikamilifu nguvu na uwezo wa kila mchezaji kwa manufaa ya timu.”