Ahmed Ally aeleza mwarobaini kutokomeza jezi feki

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameendelea na ziara yake mikoani yenye lengo la kutoa elimu kwa wanachama na mashabiki juu ya madhara ya kuvaa jezi feki, ambapo leo Oktoba 14, 2025 amewasili mkoani Morogoro na kufanya kampeni ya uhamasishaji katika maeneo mbalimbali ya mji huo.

Akizungumzia ziara hiyo, Ally amesema tafiti zilizofanywa na klabu hiyo zimebaini kuwa mashabiki wengi hawajui athari zinazotokana na kununua jezi feki, huku wengine wakikosa uelewa kuhusu manufaa ya kuvaa jezi halisi (Original) zinazouzwa rasmi na klabu.

“Tumeona wapo mashabiki wanaonunua jezi feki bila kujua kwamba kitendo hicho kinapunguza mapato ya klabu yao, pia wengi hawajui kwamba kununua jezi halisi ni mchango wao wa moja kwa moja katika kuimarisha klabu yao ndiyo maana tumepita mitaani kuwapa elimu hii,” amesema Ally.

Kwa mujibu wa Ally, kampeni hiyo imekuwa na mwitikio chanya kwani mashabiki wengi wameonesha hamasa kubwa kusikiliza elimu hiyo na kubadili tabia mara moja baada ya kupata uelewa.

“Tunafurahia kuona watu wakibadilika haraka, elimu hii ni endelevu na kila tunapopata nafasi tunawafikia mashabiki zaidi, tumejifunza mengi kupitia maoni yao na tunayaweka kwenye mipango yetu ili kuhakikisha kila shabiki ana sababu ya kununua jezi halisi,” ameongeza Ally.

Amesema baadhi ya sababu zilizotolewa na mashabiki wanaonunua jezi feki ni pamoja na ugumu wa maisha, kwani jezi halisi zinauzwa ghali takribani Sh45,000 wakati jezi feki zinapatikana kwa bei ya chini ya Sh20,000. 

Vilevile changamoto ya upatikanaji wa jezi halisi katika maeneo ya pembezoni imechangia kuongezeka kwa soko la bidhaa bandia.

Amesema klabu inachukua hatua za kuboresha mfumo wa usambazaji wa jezi halisi hadi maeneo ya vijijini ili kila shabiki azipate kwa urahisi. Pia inapanua kampeni ya uelewa kuhusu namna ya kutofautisha jezi halisi na bandia.

“Tunaongeza nguvu kwenye utoaji elimu ili shabiki wa Simba aweze kutofautisha kati ya jezi halisi na feki, mashabiki wanapswa kujua jezi halisi ina sehemu ya kuskani (scan code). Ukikuta haina jua hiyo ni feki,” amesema.