Aliyoahidi Samia kuchochea uchumi wa Kanda ya Ziwa

Bukoba. Katika kampeni zake Kanda ya Ziwa, mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ametoa ahadi kadhaa zinazolenga kuchochea uchumi na biashara.

Samia ametoa ahadi hizo katika mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara, akitilia mkazo ujenzi wa viwanda, kuboresha miundombinu ya usafiri, kuendeleza sekta za kilimo, madini, uvuvi na utalii, pamoja na kuboresha huduma za jamii.

Samia amezungumzia kwa uzito viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo, akisema ndicho kitakachotoa ajira na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika Kanda ya Ziwa.

Katika kusisitiza hilo, ametaja miradi ikiwamo ujenzi wa viwanda vya kuchakata maziwa wilayani Bukombe ili kuinua biashara ya maziwa na kipato cha wafugaji.

Ameahidi kujenga viwanda vya kuchakata mbegu za alizeti na matunda mkoani Geita kwa lengo la kuimarisha uchumi wa wakulima na kuongeza thamani ya mazao hayo.

Pia, kufufua viwanda vya zamani katika maeneo ya Sengerema, Buchosa na Manawa sambamba na kufufua Chama Kikuu cha Ushirika cha Mwanza ili kuwawezesha wakulima kupata masoko ya uhakika.

Ameahidi pia kuimarisha sekta ya viwanda vya vifaa tiba kama vile uzalishaji wa bandeji, pamba na shuka, bidhaa ambazo kwa sasa nyingi huagizwa nje ya nchi.

Kwa mujibu wa ilani ya CCM 2025/30, Serikali inayotarajiwa kuongozwa na Samia imelenga kuongeza ukuaji wa sekta ya viwanda kutoka asilimia 4.8 hadi 9 ifikapo mwaka 2030, hatua ambayo itachochea ajira, mapato na ushindani wa kiuchumi katika ukanda huo.

Miundombinu ya usafiri na usafirishaji

Kanda ya Ziwa ni kitovu cha biashara na usafirishaji wa ndani na nje ya nchi kupitia Ziwa Victoria na mipaka ya Kenya na Uganda.

Samia ameahidi kuboresha viwanja vya ndege vya Mwanza na Chato, pamoja na kujenga vipya vya Geita Mjini na Mugumu (Serengeti), ambavyo vitasaidia kukuza utalii na usafiri wa kibiashara.

Kuhusu reli, amesisitiza umuhimu wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Mwanza–Isaka (kilomita 314), ambao umekamilika kwa asilimia 63. Reli hiyo itakuwa na stesheni tano zitakazochochea biashara, huduma na ajira katika maeneo itakayopita.

Vilevile, ameahidi kuboresha barabara na kujenga maghala na masoko ya kisasa, ahadi aliyoitoa wilayani Mbogwe, ikilenga kuwezesha wakulima kuhifadhi na kuuza mazao yao kwa ufanisi.

Kanda ya Ziwa ni nyumbani kwa migodi mikubwa ya dhahabu na wachimbaji wadogo wengi.

Samia ameahidi Serikali itatoa mitaji kwa wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kukua na kuingia katika uchimbaji mkubwa.

Mbali na hayo, ameahidi kupanua maeneo ya wafugaji kutoka ekari milioni 3.4 hadi milioni 6 na kuyapima kwa ajili ya kumilikishwa rasmi, hatua itakayopunguza migogoro kati ya wafugaji na wakulima.

Katika uvuvi, ameahidi kuongeza vizimba vya ufugaji samaki katika Ziwa Victoria, kuimarisha viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi na kufunga uzio wa usalama ndani ya ziwa ili kudhibiti mamba na kulinda wavuvi.

Samia ameahidi pia kuanzisha vituo vya ufuatiliaji kwa kutumia ndege nyuki (drones) wilayani Maswa ili kudhibiti wanyama wakali wanaovamia mashamba na kuhatarisha maisha ya wananchi.

Mgombea huyo ameahidi kuendeleza eneo la Mugumu (Serengeti) kama kitovu cha utalii kutokana na fursa zilizopo na ukaribu wake na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Amesema Serikali itahamasisha uwekezaji wa hoteli, masoko na miundombinu ya utalii ili kuvutia wageni zaidi ndani na nje ya nchi.

Mbali na miradi ya kiuchumi, ameahidi kuboresha huduma za afya, ikiwemo ujenzi wa tawi la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Kanda ya Ziwa na kuendeleza hospitali zilizopo, ikiwamo Hospitali ya Rufaa ya Chato yenye vifaa vya kisasa vinavyohudumia wagonjwa kutoka mikoa jirani na nchi za Afrika Mashariki.

Pamoja na hayo, amezungumzia uendelezaji wa miundombinu ya elimu, miradi ya maji na huduma za barabara vijijini ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote.

Kwa ujumla, ahadi za Samia Kanda ya Ziwa zimejikita katika kuunganisha sekta za uzalishaji (kilimo, madini, uvuvi na utalii) na miundombinu ya viwanda na usafiri ili kujenga uchumi shirikishi.