Ni Oktoba 14, 2025, imetimia miaka 26 tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipoagana na dunia na kuyaanza maisha baada ya kifo. Tangu kifo chake, Tanzania imefanya uchaguzi mkuu mara tano.
Oktoba 29, 2025, Tanzania itafanya uchaguzi mkuu kwa mara ya sita tangu Mwalimu Nyerere alipoondoka. Tanzania bado ni mali ya Watanzania.
Tanzania ni ardhi ya ‘yote yanawezekana’. Na huo ndiyo msingi alioujenga kwa wivu mkubwa.
Msingi ambao kila Mtanzania, bila kujali asili anakotoka, mwanzo wake, wala nasaba, anaweza kuwa yeyote. Kijana wa kimaskini mwenye umri wa miaka 24, Felix Mkosamali aliyesoma shule za kata akiwa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, anagombea ubunge na kushinda.
Vijana kutoka familia duni, Zitto Kabwe kwa David Kafulila, John Mnyika hadi Mwigulu Nchemba, wakafanikiwa kuwa wabunge. Tanzania, kila mtu anaweza kuwa yeyote, mradi unasimama imara, unazikimbiza ndoto. Tanzania mafanikio hayana mkondo, yanaweza kumkumbatia yeyote.
Vijana waliojitupa Kariakoo kama wabangaizaji, Sanda Yenga ‘Sandaland,’ Fred Ngajiro ‘Vunjabei’ na wengine, wanageuka mabilionea na kushinda zabuni za kusambaza vifaa vya michezo vya Klabu ya Simba. Ni mfano kuwa inawezekana kwa kila mtu.
Itazame Tanzania; Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika kisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mwalimu Nyerere, Rais wa pili ni Alhaji Hassan Mwinyi. Rais wa tatu ni Benjamin Mkapa wa nne, Jakaya Kikwete, wa tano, Dk John Magufuli na sasa (Rais wa sita) ni Samia Suluhu Hassan.
Anza Mwalimu Nyerere mpaka Samia, angalia nasaba zao uone kama kuna mwingiliano wa kiukoo. Unakuta hakuna. Kila mmoja miongoni mwa marais sita, kila mmoja njia yake ya ukuu wa kisiasa ameitengeneza mwenyewe.
Wapitie matajiri ambao wanatajwa kuongoza Tanzania, hesabu mmoja baada ya mwingine, halafu wachunguze viongozi wakuu waliopata kuongoza Tanzania. Humuoni mtoto wa kiongozi wala mwana ukoo wao.
Hayo yamewezekana kwa sababu Mwalimu Nyerere aliijenga nchi kwa misingi ya kumfaa kila mwananchi. Mtoto wa kimaskini kutoka Kizimkazi, Makunduchi, aliyesoma katika mazingira magumu, anaaminiwa kisha anatumwa kuliongoza Taifa.
Yanatokea hayo kwa sababu Mwalimu Nyerere baada ya kufanikisha uhuru, alihakikisha hakuna kundi linalohodhi mamlaka ya nchi. Yeyote awaye anaweza kuwa kiongozi. Mwana kutoka Buhigwe, Philip Mpango, leo hii ni Makamu wa Rais, Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania. Mwana wa Ruangwa kutoka familia hohehahe, Kassim Majaliwa, ndiye Waziri Mkuu.
Haikushindikana Mwalimu Nyerere kutamani kumwachia mwanaye mmoja mikoba ya urais baada yake kipindi anang’atuka. Hata hivyo, aliwaheshimu Watanzania kwamba Tanzania ni nchi yao na siyo mali binafsi ya familia ya Mwalimu Nyerere wa Butiama.
Mtoto wa kimaskini mwenye kulala na mifugo chumba kimoja mithili ya zizi, Reginald Mengi, anaanza biashara hadi kuwa tajiri mkubwa kwenye nchi. Mwana wa kapuku aliyeanza biashara kwa kuuza vitafunwa, Said Bakhresa leo ni bilionea wa kuogopwa.
Hayo yanawezekana kwa sababu Tanzania imelelewa kuwafanya, kuwaonesha na kuwadhihirishia wananchi wote kwamba wapo huru kuusaka uchumi wao. Biashara yoyote halali unayoiamini, inaweza kukutoa ulipo hadi kufika pakubwa kama utaifanya kwa nidhamu, huku ukifuata sheria ambazo zipo wazi kwa kila mtu.
Tanzania imelelewa kuwafanya, kuwaonesha na kuwadhihirishia wananchi kuwa wote wana haki na fursa sawa kwenye Taifa lao. Hakuna tabaka maalumu la wenye kuhodhi uchumi na lingine la wanaotumikishwa.
Inavutia sana kuwa raia wa Tanzania. Nchi ya kila Mtanzania. Tunu muhimu zaidi ya kulindwa ni Utanzania asili usiokuwa na ubaguzi wala ubinafsi. Utanzania wenye kumfanya kila raia asijione mnyonge awapo ndani ya nchi yake, maana yeye ni mtu huru.
Hakuna Mtanzania zaidi ya mwenzake na hayupo aliye na upungufu kama mwananchi. Huo ndiyo Utanzania ambao umelelewa na Mwalimu Nyerere. Tanzania ambayo mtoto wa mwasisi wa Taifa hili, Makongoro Nyerere anakuwa mbunge mwaka 1995 kupitia chama cha NCCR-Mageuzi kisha ubunge wake unapingwa mahakamani.
Mwaka 1997, Makongoro anapoteza ubunge na haiwi habari kwamba huyo ni mtoto wa Baba wa Taifa, kwani Tanzania huru haikulelewa kutoa upendeleo usiostahili kwa yeyote. Ni kwa sababu hayupo Mtanzania zaidi wala Mtanzania pungufu.
Kama Mwalimu Nyerere angeamua kujipa upendeleo wa madaraka na umiliki wa mali, yeye na familia yake, marafiki zake au na waasisi alioshirikiana nao kudai uhuru, nchi isingeitwa huru, ingekuwa imehama kutoka wakoloni weupe (wazungu) hadi wazawa (weusi). Mwalimu Nyerere alisimamia misingi ya nchi kuwa huru na uhuru unadhihirika kwa kila Mtanzania.
Mwalimu Nyerere alileta Azimio la Arusha la mwaka 1967. Lengo lilikuwa na mengi yenye kuwafunga viongozi kudhani kuwa wao walikuwa wanastahili zaidi kuliko Watanzania wengine.
Hakuna kabila lenye Tanzania
Mwalimu Nyerere na Tanzania aliyoijenga; kila kabila popote lilipokuwa, alilifikia na kulielimisha thamani yake na ‘hisa’ zake kwenye Utanzania. Kila kabila lilioneshwa, lilitambuliwa na lilidhihirishiwa kuwa sehemu ya umiliki wa Tanzania. Na imeendelea kuwa hivyo mpaka sasa.
Kutoka Uhayani mpaka Ugogoni, Uchagani hadi Uheheni. Kwa Waha na Wangoni, Wanyamwezi kwa Wanyakyusa, Usukumani kwenda Umasaini, Wanyiramba na Wapare, Wayao na Wahangaza, Wabena kwa Wamang’ati.
Endelea kwa Wasambaa mpaka Wamburu, Wajita na Wakinga, Wazinza kwa Wazaramo, Waluguru na Wakurya, Wakwere kwa Wabondei, Wazigua na Wamakonde, kisha fikisha makabila yote zaidi ya 120, wote ni Watanzania walio na hadhi pamoja na fursa sawa.
Muhimu zaidi makabila yote yanaingiliana, Mndengereko kuolewa na Mbarbaig au Mzanaki kufunga ndoa na Muirak na mambo yanayotokea, sawasawa Mfyomi na Mrangi au Mgorowa na Msandawe kuzaa mtoto mwenye mwingiliano wa makabila mawili.
Ukiona vinaelea jua vimeundwa. Hivyo ipo kazi ilifanyika kuhakikisha vionjo hivi vya Utanzania vinakuwepo kisha Watanzania kuviishi kama mazoea. Mkerewe kuweka maskani Arusha na kuishi bila kunyooshewa kidole kwamba siyo kwao, Mfipa kufanya makazi yake Tanga pasipo kubughudhiwa na yeyote.
Ukiwa Mtanzania, unapotembelea au kuishi mkoa wowote unajiona upo nyumbani. Utakutana na watu wa makabila mengine ambao watakuwa ndugu na majirani zako. Maisha ya utafutaji riziki yanakukutanisha na watu wa makabila tofauti ambao wanakuwa ndugu na marafiki. Shuleni pia hivyohivyo. Huo ndiyo Utanzania wenye thamani.
Uhuru wa nchi umelelewa kwa misingi ya kila mmoja kujiona yupo huru kuabudu atakavyo na asijione mnyonge kwa imani yake na hatahukumiwa kwa sababu ya madhehebu anayoamini.
Utanzania umejengwa kwa misingi ya kuheshimiana, kuvumiliana na kuwapa watu uhuru wao wa kuabudu.
Kuanzia taasisi za umma mpaka za binafsi, ajira zinatolewa pasipo masharti ya dini. Kampuni ya Mkristo lakini waajiriwa wengi ni Waislamu. Shirika la Mwislamu lakini limejaza wafanyakazi Wakristo na wasioamini katika dini. Hiyo ndiyo Tanzania ya Mwalimu Nyerere.
Miaka 26 tangu kifo cha Mwalimu Nyerere, ni vizuri kumkumbuka kwa shukurani. Alijenga misingi ambayo ni rahisi kuiona kawaida. Ukipima mazingira ya mataifa mengine ya Afrika baada ya uhuru, utatambua Mwalimu alifanya nini kwa Watanzania. Asante sana Baba wa Taifa.